
Ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Urusi imefungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya Tanzania na Russia, huku nchi hizo zikikubaliana kushirikiana katika maeneo tisa ya kimkakati yenye thamani ya uwekezaji inayokadiriwa kufikia Sh5.25 trilioni. Makubaliano hayo yanahusisha sekta za kilimo, nishati, madini, viwanda, biashara, usafirishaji, uchumi wa kidijitali, elimu, afya na utalii.
Kwa mtazamo wa haraka, hatua hii inaweza kuonekana kama ishara ya Tanzania kuimarisha uhusiano wake na Russia katika kipindi ambacho dunia imegawanyika zaidi kutokana na mvutano wa kijiografia kati ya Urusi na mataifa ya Magharibi. Hata hivyo, uchambuzi wa kina wa maslahi ya Tanzania unaonesha kuwa hakuna sababu ya kutafsiri ushirikiano huo kama mabadiliko ya kimkakati ya Tanzania kuelekea kambi ya Russia. Kinyume chake, Tanzania inaendelea kufuata sera yake ya muda mrefu ya kutofungamana na upande wowote na kujenga ushirikiano unaotegemea maslahi ya taifa.
Diplomasia ya Kutofungamana na Upande Wowote
Kauli ya Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, kwamba hakuna dalili zozote za Tanzania kuchagua upande mmoja dhidi ya mwingine katika siasa za kimataifa, inaakisi uhalisia wa diplomasia ya Tanzania. Serikali inaonekana kutafuta fursa za kiuchumi popote zinapopatikana, iwe ni Mashariki au Magharibi.
Takwimu za uwekezaji zinaeleza kwa uwazi zaidi. Nchi zinazoongoza kwa uwekezaji mkubwa nchini Tanzania ni China, Uingereza, Marekani, Mauritius, India, Vietnam, Umoja wa Falme za Kiarabu, Kenya, Australia na Misri. Orodha hii inaonyesha kwamba uchumi wa Tanzania umeunganishwa kwa kiwango kikubwa na mataifa mbalimbali kutoka mabara tofauti. Russia haimo miongoni mwa wawekezaji wakubwa nchini, jambo linaloonyesha kuwa hata kama ushirikiano mpya utafanikiwa, itachukua muda mrefu kabla ya kuwa na uzito unaoweza kulinganishwa na washirika waliopo tayari.
Mataifa yenye uwekezaji mkubwa Tanzania
🌏 ASIA & PASIFIKI [▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓] China, India, Vietnam, Australia
🇬🇧 MAGHARIBI [▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓] Uingereza, Marekani
🌍 AFRIKA & GHUBA [▓▓▓▓▓▓▓▓▓] Mauritius, Kenya, Misri, UAE
URUSI Haipo kwenye 10 Bora
Aidha, mchango wa misaada ya maendeleo unaendelea kuonyesha utegemezi mkubwa wa Tanzania kwa washirika wa jadi wa Magharibi. Marekani pekee hutoa zaidi ya Sh1.7 trilioni kwa mwaka katika sekta za afya, elimu, kilimo na utawala bora. Uingereza, Umoja wa Ulaya, Ujerumani, Japan, Canada, Sweden, Norway na Uswisi pia zina mchango mkubwa katika kufadhili huduma za kijamii na miradi ya maendeleo. Hata China, ambayo imekuwa mshirika muhimu wa kiuchumi wa Tanzania, bado kiwango chake cha misaada ni kidogo ukilinganisha na mataifa ya Magharibi.
Hii ina maana kwamba kwa sasa, Urusi haiwei kuchukua nafasi ya mtandao mpana wa washirika wa Tanzania katika uwekezaji, biashara, misaada ya maendeleo na teknolojia. Uhalisia wa uchumi wa Tanzania unahitaji ushirikiano na pande zote. Marekani na Ulaya ni masoko muhimu ya bidhaa za Tanzania, China ni mshirika mkubwa wa miundombinu na biashara, nchi za Ghuba zinawekeza katika bandari na usafirishaji, huku India ikiwa mshirika muhimu katika dawa na viwanda.
Changamoto ya Utekelezaji wa Mikataba
Makubaliano yaliyosainiwa wakati wa ziara ya Rais Samia yanaonyesha zaidi mwelekeo wa kujenga uwezo wa ndani kuliko utegemezi wa kisiasa. Ushirikiano kati ya vyuo vikuu vya Tanzania na Urusi katika sayansi ya data, mifumo ya anga, elimu ya juu na mafunzo ya ufundi unaweza kusaidia Tanzania kupata ujuzi unaohitajika katika uchumi wa kisasa. Vivyo hivyo, ushirikiano katika afya na utalii unaweza kuongeza fursa mpya za maendeleo.
Lakini mafanikio ya makubaliano haya yatategemea utekelezaji wake. Tanzania imewahi kusaini mikataba mingi ya kimataifa ambayo haikuzalisha matokeo yaliyotarajiwa kutokana na changamoto za utekelezaji. Kwa hiyo, kipimo halisi cha mafanikio ya ziara ya Russia hakitakuwa idadi ya hati zilizosainiwa bali kiasi cha uwekezaji kitakachoingia nchini, ajira zitakazozalishwa, teknolojia zitakazohamishwa na thamani ya biashara itakayoongezeka.
Mvutano wa Kidiplomasia na Mataifa ya Magharibi:
Ziara hii imekuja wakati ambao nchi za Marekani na Ulaya zimeanza kutafakari uhusiano wake na Tanzania kufuatia vurugu za Uchaguzi Mkuu na matukio mengine ya uvunjifu wa haki za binadamu.
Kwa mfano, tayari Marekani imeshatoa tamko la kutafakari upya uhusiano wake wa kidiplomasia na Tanzania, huku Maseneta wawili wa nchi hiyo wakiwasilisha muswada bungeni unaoitaka serikali yao kutathmini upya uhusiano wake na Tanzania kutokana na madai ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na ukandamizaji wa kisiasa ulioripotiwa baada ya Uchaguzi Mkuu. Endapo muswada huo utapitishwa na bunge lao, utaiweka Tanzania katika wakati mgumu na pengine kuingia kwenye kundi la nchi zenye vikwazo vya Marekani.
Kura zilizopigwa katika kamati mbili za Bunge la Ulaya
Ndio (Kusitisha): 81 Kura (94.2%)
◑ Waliojizuia: 4 Kura (4.6%)
○ Hapana: 1 Kura (1.2%)
[▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓▓░░▒]
│───────────────────────────────────│ │
94.2% Ndio (Kusitisha) │ └─ 1.2% Hapana
└──── 4.6% Waliojizuia
Kama hiyo haitoshi, wabunge wa kamati mbili za Bunge la Ulaya (Mambo ya Nje na Maendeleo) walipiga kura kuidhinisha azimio la kusitisha msaada wa maendeleo wa Euro milioni 156 (takriban Shilingi bilioni 440 za Tanzania). Kura hiyo ilipita kwa wabunge 81 kuunga mkono, 1 kupinga na 4 kutopiga kura. Sababu kuu zilizotolewa na wabunge hao ni pamoja na malalamiko kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu, hatua za kukandamiza demokrasia, kukosekana kwa uhuru wa maoni, na mvutano wa kuzuiliwa kwa wanasiasa wa upinzani.
Japo Serikali ya Tanzania emefafanua kuwa hatua hiyo sio ya mwisho, lakini malalamiko hayo ni ya muda mrefu na huenda Bunge la Ulaya litaridhia mapendekezo ya kamati hiyo.
Kwa kuzingatia orodha ya nchi zinazotoa misaada na nchi zenye uwekezaji mkubwa nchini Tanzania, Serikali inapaswa kulinda uhusiano wa kidiplomasia na mataifa ya Magharibi kama mboni ya jicho ili kuendelea kufaidika na fursa za kibiashara na uwekezaji. Cha kufanya hapo ni kusikiliza malalamiko yao, ambayo kimsingi ni kurejea kwenye makosa yaliyotokea katika michakato ya uchaguzi na kuwawajibisha watendaji wa Serikali wanaotuhumiwa kwa uvunjifu wa haki za binadamu.
Nini kifanyike?
Katika mazingira ya sasa ya dunia, Tanzania haina sababu ya kutafuta “kimbilio” kwa taifa lolote. Nguvu yake iko katika uwezo wa kushirikiana na kila upande bila kupoteza uhuru wake wa kisera. Huu ndio urithi wa sera ya kutofungamana na upande wowote iliyoasisiwa tangu enzi za Mwalimu Julius Nyerere, na ambao unaendelea kuwa na umuhimu mkubwa katika dunia ya leo yenye ushindani mkubwa wa kisiasa na kiuchumi.
Kwa hiyo, ziara ya Rais Samia nchini Urusi inapaswa kutazamwa kama juhudi za kupanua fursa za maendeleo, si kama ishara ya Tanzania kuhama kutoka upande mmoja wa dunia kwenda mwingine. Russia inaweza kuwa mshirika muhimu katika baadhi ya sekta, lakini kwa sasa sio kimbilio la Tanzania. Kimbilio halisi la Tanzania ni diplomasia inayoweka mbele maslahi ya taifa, uchumi unaovutia uwekezaji kutoka kila upande, na sera za maendeleo zinazowanufaisha wananchi wake bila kujali zinatoka Mashariki au Magharibi.
