Wanawake Dodoma waweka wazi ukatili wa kijinsia wanaokabiliana nao
Sidi Mgumia, TAMWA
Aghalabu wanawake walio wengi huhofia kueleza changamoto wanazokabiliana nazo kwa uwazi.
Hata hivyo, mdahalo uliofanyika mkoani Dodoma, kuhusu ukatili wa kijinsia, uliwapa wanawake ujasiri wa kueleza kinagaubaga matukio ya ukatili wa kijinsia wanayokumbana nayo.
Mafunzo yaliyotolewa na Chama Cha Wanahabari Wanawake Tanzania, (TAMWA) kuhusu ukatili wa kijinsia, madhara yake na na wapi wakatoe taarifa, baada ya kufanyiwa ukatili yaliwapa ujasiri wa kuzungumza.
Mdahalo huo uliwakutanisha zaidi ya washiriki 50 wakiwemo wanawake, wanafunzi, walimu na viongozi wa jamii kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu ukatili wa kijinsia, kuhimiza utoaji wa taarifa na kujadili namna ya kulinda makundi yaliyo katika mazingira hatarishi.
Miongoni mwa washiriki waliopata nafasi ya kuchagia mada mbalimbali ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake Wakulima Chamwino (JUWACHA), Janeth Nyamayahasi ambaye alisimama na kueleza jinsi jamii ilivyozoea baadhi ya vitendo vya ukatili bila kuviona kama ukiukwaji wa haki za binadamu.
Alieleza kuwa wanawake wengi wamekuwa wakivumilia vitendo vya ukatili kwa muda mrefu wakiamini ni sehemu ya maisha ya kawaida, hali ambayo imewafanya wengi kushindwa kutafuta msaada au kuripoti matukio wanayokumbana nayo.
“Wanawake wengi wana hali mbaya kiuchumi, wanamtegemea mume, kwa hiyo hata wakifanyiwa ukatili, hawawezi kuripoti wanakaa kimya,” amesema, Nyamayahasi
Kauli hiyo iliakisi moja ya matokeo makubwa ya mdahalo huo, kwamba kadiri elimu inavyoendelea kutolewa ndivyo wananchi wanavyoanza kutambua kuwa baadhi ya mambo waliyochukulia kuwa ya kawaida kwa miaka mingi ni aina za ukatili wa kijinsia.
Agnes Chizoza, kiongozi wa Jukwaa la Wanawake Vijana, Chamwino anasema, kwa miaka mingi changamoto ya ukatili wa kijinsia imeendelea kuathiri maendeleo ya jamii.
Chizoza anasema, wanawake vijana wanakabiliwa na ukatili hasa wa rushwa ya ngono wanapokwenda kuomba ajira au wawapo katika ajira.
“Sababu mbalimbali zimetajwa kuchangia hali hiyo ikiwemo umasikini, utegemezi wa uchumi, matumizi mabaya ya pombe, mila kandamizi na kiwango cha chini cha elimu,”anasema
Hata hivyo, jambo lililojitokeza wazi katika majadiliano hayo ni kwamba juhudi za utoaji elimu zimeanza kueleta mabadiliko ya mtazamo ndani ya jamii.
Akifungua mdahalo wa wanawake wa Chamwino, Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania {TAMWA}, Dkt. Rose Reuben aliwataka washiriki kutumia nafasi hiyo kujifunza na kuwa sehemu ya mabadiliko.
“Kuna ukatili wa aina nyingi na kila mmoja amepitia kwa aina yake. Tupo hapa kujifunza ili kupata maarifa zaidi na kwa pamoja tuendelee kupaza sauti zetu,” anasema
Katika siku ya kwanza ya mdahalo yaliyofanyika katika shule ya Chiona iliyoko Wilayani Bahi mkoani Dodoma, wanafunzi walionesha kuwa na uelewa mzuri kuhusu ukatili wa kijinsia na namna ya kutafuta msaada wanapokumbwa na vitendo hivyo.
Washiriki walibainisha kuwa elimu inayotolewa mashuleni na katika jamii imechangia watoto wengi kupata ujasiri wa kutoa taarifa kuhusu vitendo vya ukatili tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma ambapo wengi walikaa kimya kwa hofu au kutokujua pakupeleka malalamiko yao.
Afisa Elimu kutoka Dodoma, Kumburusa Elias alisema jamii inapaswa kuhakikisha watoto wa kike wanapata haki ya elimu bila vikwazo.
“Usikubali mtoto wako wa kike akatishwe elimu na baba kwa kigezo cha kuolewa. Tafuta namna yoyote kwa siri utoe taarifa zitakazomsaidia kupata haki yake,” alisema
Mbali na elimu kwa watoto, mdahalo huo ulitoa nafasi kwa wanawake kujifunza kuhusu haki zao za kiuchumi ambapo Afisa Maendeleo wa Jiji la Dodoma, Neema Majura aliwahimiza wanawake kutumia vikundi vya kijamii na kiuchumi kama njia ya kujikomboa dhidi ya utegemezi unaoweza kusababisha ukatili.
“Tuna fursa za vikundi tuzitumie kuepuka ukatili wa kiuchumi. Sio kila kitu lazima umuulize baba. Tazitafute fursa na tuendelee kuwa mabalozi wazuri kupinga ukatili,” alisema
Mwenyekiti wa JUWACHA, Janeth Nyamayahasi alisisitiza kuwa hata wanawake wenyewe wakati mwingine hushiriki kuendeleza ukatili bila kujua.
“Wakati mwingine sisi wenyewe tunafanya ukatili bila kujua kwamba huu ni ukatili. Tuitumie fursa hii kujifunza ili tukasaidie na wengine kwenye jamii zetu,” alisema
Kwa upande wa vyombo vya sheria, Dawati la Jinsia na Watoto la Jeshi la Polisi lilitumia jukwaa hilo kueleza huduma zinazotolewa kwa waathirika wa ukatili.
Mrakibu wa Polisi na Mkuu wa Dawati la Jinsia Dodoma, Christa Yombo alisema wananchi hawapaswi kuogopa kutoa taarifa kwa sababu usiri na weledi huzingatiwa.
“Tunafanya kazi kwa usiri na weledi kusaidia wahanga wa ukatili wa kijinsia. Unapaswa ujiamini kabisa unapotoa taarifa yako kwani itabaki ni siri,” alisema
Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) Agness John amesema kua anaungana na wengine kutokomeza ukatili wa kijinsia kwa kuhamasisha watu wasinyamaze, wafuatilie kesi zao, kuacha kuwakandamiza wanaoathirika.
Mdahalo huo pia ulionesha umuhimu wa vyombo vya habari katika kuelimisha wananchi na kuhamasisha mabadiliko ya tabia. Waandishi wa habari walihimizwa kuendelea kuripoti masuala ya ukatili wa kijinsia kwa kuzingatia maadili ya taaluma na kulinda utambulisho wa waathirika.
Kwa ujumla majadiliano ya Bahi na Chamwino yameonesha kuwa elimu ni silaha muhimu katika kupambana na ukatili wa kijinsia. Kadri jamii inavyoendelea kupata maarifa ndivyo inavyozidi kupata uwezo wa kutambua, kuripoti na kupinga vitendo vya ukatili.
About the Author
Wino Tanzania
Author
WINO Tanzania is a nonprofit, non-government, media organization registered on 11th August 2022 under non-Government Organizational Act of 2002, with Registration No. 00NGO/R/3681. WINO seeks to bridge the gaps in a media industry in Tanzania, by providing grants for Investigative Journalism, training and mentorship programs so as enable them to perform with greater professionalism and hence impact journalism
