
Mwandishi wetu, Wino
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limetimiza miaka 40 tangu lilipoanzishwa mwaka 1986 likipitia vicheko na machozi.
Safari ya baraza hilo inafananinshwa na ukuaji wa mtoto mdogo mpaka anapofikia utu uzima akijifunza tabia njema.
Tangu kuanzishwa kwa NEMC, bodi tisa zimeundwa ili kulisimamia baraza.
Akizungumzia safari hiyo Mei 28, jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi ya tisa ya NEMC, Mhandisi Mwanasha Tumbo ametoa shukrani kwa viongozi waliotangulia kuiongoza taasisi hiyo tangu ilipokuwa change.
“NEMC ilikuwa mtoto na sasa ina miaka 40, imekuwa mtu mzima, tukichukua mfano huo mtoto anapoanza kulelewa mpaka anakuwa, wale wenzetu wamefanya kazi kubwa kuhakikisha baraza limefika hapa ilipo.
Mwanasha aneleza kuwa Tanzania inaendelea kukua, hivyo athari ya matumizi ya vitu mbalimbali ambavyo vinaharibu mazingira yetu nayo inaenda kukua katika kasi hyo hiyo.

“Katika miaka 40 iliyopita nchi hii haikuwa jinsi ilivyo, kuna uharibifu mkubwa wa mazingira, kwa maana ya uchafuzi wa mazingira umeongezeka na vilevile kuna uharibifu wa ukataji miti pia umeongezeka.
“Hali hii inachagizwa na ukuaji wa maendeleo ya kiuchumi miradi inayo jengwa ndani na nje ya nchi na yenyewe kwa njia moja au nyingine yanaongeza uchafuzi wa mazingira katika nchi yetu kwa upande wa mabadiliko ya tabia nchi,” amesema.
Anaelezea zaidi kuwa kuongezeka kuharibika kwa mazingira kutokana na uchafuzi unaofanyika, kunasababisha ukosefu wa bioanuai, kitu amabacho kiasili kinatakiwa kiwepo ili kuwe na uendelevu wa mazingira yatakayotuwezesha sote kuishi.
Mwanasha anatanabaisha kuwa pamoja na uchafuzi uliopo na mambao mengine, bodi zilizopita zilichukua hatua mbalimbali mpaka kuifikisha NEMC mahali ilipofikia.
Anasema kutokana na hatua hizo, kumekuwa na maendeleo ya viwanda na maendeleo ya kiuchumi, ambayo yamezingatia vigezo vya mazingira na kama hatua zisingechukuliwa, yangeharibu mazingira.
“Sisi kama bodi ya tisa sasa jukumu letu kubwa tunaenda kusimamia, tunajua sasa hivi teknolojia zimekuwa, tulikotoka kama tulikuwa tunaenda kusimamia kwa miguu, tunahitaji sasa kutumia teknolojia kusimamia suala la uzingatiaji wa masuala ya usimamizi wa mazingira,” anasema
Hata hivyo, anasema bado kuna changamoto ya uelewa mdogo katika utunzaji wa mazingira, licha ya kuwepo kwa matumizi ya teknolojia ya digijitali.
Kutokana na changamoto hiyo anasema wanatoa kipaumbele cha utoaji wa elimu ya mazingira kwa jamii.
“Tunapozungumzia suala la taka au nchi chafu, kama watu hawana elimu hawawezi kuelewa kwa nini tunahitaji nchi iliyosafi.
“Tunapozungumza uchafuzi wa hewa wasipokuwa na elimu hawawezi kujua kwa nini asitumie kuni atumie nishati safi, kwa hiyo tunahitaji bado kuendelea kutoa elimiu na hili ni jambo pia tunaenda kulipa msukumo zaidi kwenye jamii,” amesema.
Amesema katika maadhimisho ya miaka 40, wamewatembelea wale wanaochakata taka, wanaofanya usafi, wanaopanda miti na wenye viwanda kuhakikisha mazingira yanaendelea kuwa salama.
NEMC ilivyoanza kwa machozi

Mhandisi Bonaventure Thobias Baya, aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa awamu ya tatu wa NEMC, amesema wamekuwa wakipambana na changamoto na kuzitatua.
Mhandisi Bonaventure aliyekuwa Mkurugenzi wa idara tofauti za NEMC tangu mwaka 1997, kabla ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu mwaka 2007 hadi mwaka 2017 alipostaafu, ametaja miongoni mwa changamoto hizo kuwa ni ufinyu wa nafasi ya ofisi.
“Hii ilikua chamgamoto kubwa kwa upande wangu, kwani tulikuwa katika jengo la Tanroads (Wakala wa Taifa wa Barabara) na tunakaa kwenye korido moja, upande mmoja alikuwa anakaa mpangaji mwingine na sisi tuko upande mwingine.
“Unaweza ukafikiria taasisi ya serikali kuwekwa katika korido, lakini hata hivyo NEMC ilikuwa bado inakua ilikuwa haijafikia ilipo sasa hivi, ilikuwa na wafanyakazi wachache, vitendea kazi vichache, halafu utendaji wa baraza kwa ujumla ulikuwa bado haujakomaa,” anasema.
Anafafanua kuwa, wakati huo kazi iliyokuwa inafanywa na baraza ya usimamizi wa mazingira ilikuwa imekosa nguvu, kwa kukosa vitendea kazi na ukosefu wa kanuni na hata idara ya tathmini ya mazingira ilikuwa haijaundwa.
Anaendelea kusema wakati NEMC inaanza ilikuwa chombo cha ushauri, mnamo mwaka 2004 sheria ya mazingira ilipoanzishwa, NEMC ilipewa meno ya kuweza kushtaki au kushtakiwa, kwa hiyo, sura ya usimamizi wa mazingira ikawa ni ya kisheria zaidi kuliko ushauri.
“Kwa hiyo mchakamchaka, mwendo na safari ya kuanza kusimamia mazingira ilianza na mimi nikiwa ofisini kazi yangu ni kuleta ufahamu wa jamii kuhusu sheria ya mazingira, lakini ilikuwa kujenga uwezo wa watendaji ndani ya baraza, kuhakikisha kwamba tunajua na watu wanajua jinsi ya kusimamia sharia,” amesema.
Maendeleo mengine katika NEMC ilikuwa ni uanzishwaji wa idara nyingine ya Tathmini ya Mazingira (EIA) ili kuhakikisha uwezo wa watu unajengwa kutoka katika kada zote kuanzia chini mpaka juu.
Mhandisi Bonaventure ameishukuru serikali iliyompa nafasi ya kwenda kusoma nchini Uingereza na Marekani kwa vipindi tofauti na kupata ujuzi na uzoefu tofauti ambao ulimwezesha kukusanya uwezo mkubwa wa kuendesha baraza hilo.
Anasema alihakikisha sera na kanuni za mazingira zinaboreshwa na baraza likaanza kupata nguvu na kuelewa majukumu yake vizuri.
“Kupitia bodi tuliokuwa nayo, na uelewa wangu na uzoefu nilioupata, nilitoa ushauri kwenye bodi kwamba tuipanue NEMC kiutendaji, tukaanzisha ofisi za kanda tukianza na ofisi za Mwanza na Arusha na Mbeya.
“Kwa sasa zimeongezeka na ni modeli nzuri sana ya usimamizi wa mazingira na wazo hili nililitoa kwenye nchi zote mbili ambazo nilikuwa nimefanya kazi na kusoma huko,” amesema.
Lini NEMC itakuwa Mamlaka?
Kuhusu hamu ya kuifanya NEMC kuwa mamlaka, Mhandisi Bonaventure anasema wakati wake alianza mchakato wa hilo, lakini hafahamu kwa nini mpaka sasa halijakamilika.
Anasema NEMC ilipoanzishwa ilikuwa ni mshauri na si mtekelezaji wakati kiuhalisia NEMC inawajibika ipasavyo.
“Ni suala linaloleta mchanganyo na hata inaweza ikaleta fikra ya kutokukomaa mbele wadau wa mazingira wa mataifa na pia kuleta fikra hasi ya udogoshaji kwa wafanyakazi wake.
“Nguvu ya NEMC ni kubwa ni sawa na vyombo vingine na labda inautendaji bora kuliko tasisi nyingine katika kusimamia eneo hili la mazingira,” anasema.
Kwa kipindi chote alichofanya kazi NEMC, Bonaventure anajivunia kwamba baraza hilo limejengeka vizuri.
“Nawashauri isichuke tena miaka 40 ijayo kujipima ni muda mrefu sana huwezi kupata tathimini iliyosahihi, kuwe na kipindi kifupi hata nusu ya arobaini au kumi utapata mrejesho ulio sahihi,” anasema.
Mwelekeo mpya NEMC
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Immaculate Sware Semesi ametoa rai kwa Watanzania kuadhimiha miaka 40 kwa kutunza mazingira ili kufikia Dira ya mwaka 2050.
“Tunataka iwe taasisi ambayo inayojulikana barani Afrika na duniani kama taasisi kuu katika usimamizi uratibu na uhifadhi wa mazingira.
“NEMC tunakwenda kufanya kazi kijiditali kwa kutumia mifumo ili kurahisha uratibu wa usimamizi na ufuatiliaji wa masuala ya mazingira nchini na pia tunakwenda kuunganisha juhudi mbali mbali za kazi za NEMC katika kipindhi cha miaka 40 kwa kutumia uzoefu wa zamani,” amesema
Ameeleza kuwa NEMC imaeanzisha mfumo mahsusi wa kisasa wa Mfumo wa Ufuatiliaji Uratibu wa Usimamizi wa Mazingira wa kiditali (TOCEMS), kwa ajili ya kufuatilia na kuratibu hali ya mazingira shemu zote nchini kwa mara moja na kwa urahisi.
“Kupitia mifumo ya TOCEMS, pia tutahusisha vijana katika kuleta ubunifu zaidi ili kuleta elimu na kuleta ari ya mabadiliko ya tabia ili tujue kwamba mazigira yetu ni uhai tunatakiwa tuayalinde, tuyatunze ili yayatutunze,” amesema.
Mfumo huo umezinduliwa Mei 28, katikia ukumbi wa mikutano wa kimataifa JNICC jijini Dar es Salaamna Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba katika kuelekea kilele cha miaka 40 ya NEMC Mei 29.
