
Mwandishi Wetu, Wino Tanzania
Wakati takwimu zikionyesha kuwa wanaume ndio wanaochangia kwa kiwango kikubwa ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto, imebainika sasa kuwa wanaume wenyewe ndio waathirika wakubwa wa matukio hayo.
Utafiti uliofanywa na Idara ya Elimu ya Jamii (Department of Sociology) kwa kushirikiana na vitengo vya kitaaluma vya masuala ya jamii na jinsia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) unaonyesha kuwa taarifa za ukatili wa kijinsia dhidi ya wanaume zimeongezeka kwa kiasi kikubwa.
Ongezeko hili linatokana na mabadiliko ya mitazamo ya kijamii na uwepo wa mifumo ya kusaidia wahanga. Utafiti huo unafichua kuwa wanaume wengi hukumbana na aina mbalimbali za ukatili katika mahusiano ya karibu, ikiwemo ukatili wa kisaikolojia, vipigo, udhibiti wa kiuchumi, na unyanyasaji wa kihisia.
“Kuwepo kwa mifumo dume na hofu ya kuchekwa (stigma) ndani ya jamii yetu kunawafanya wanaume wengi wanaokumbana na ukatili wa kisaikolojia au kihisia kuchagua kukaa kimya na kuteseka kwa siri, badala ya kujitokeza na kuripoti ili kupata msaada,” anasema Simon Mashauri, Mkurugenzi wa CVS Tanzania, wakati wa mdahalo wa kijinsia ulioandaliwa na TAMWA kwa kushirikiana na GIZ.
Hali hii ya ukimya inaonyesha jinsi jamii yetu inavyoendelea kuwafunga wanaume katika pingu za mifumo ya kiume inayodai kuwa “mwanaume ni mwelewa” au ‘mwanaume hawezi kulia.’
Hata hivyo, tatizo linazidi kuenea zaidi kwenye mahusiano ya ndani. Wapo wazazi wanaowashawishi watoto wao (hasa wavulana) wajifelishe katika mitihani ili wasifaulu, ili mradi mtoto akimaliza shule aende akafanye kazi za ndani au biashara tu.
“Wazazi wengine wanaamini kuwa elimu ya juu inawafanya vijana wawe wazururaji na wasio na tija nyumbani,” anasema Beatus Kipfumo, Kaimu Afisa Elimu wa Lushoto, wakati wa mdahalo wa kijinsia ulioandaliwa na TAMWA kwa kushirikiana na GIZ.
Takwimu za Jeshi la Polisi, kwa mwaka 2025, zinaonyesha kuwa katika Mkoa wa Iringa, matukio ya ukatili wa majumbani dhidi ya wanaume yaliongezeka kutoka asilimia 19 hadi asilimia 27.
Vilevile, taarifa za Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum zinaonyesha kuwa zaidi ya wanaume 1,500 waliripotiwa kuwa waathirika wa ukatili wa kingono. Aidha, taarifa za Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) zinaonyesha ongezeko la visa vya wanaume kupoteza maisha kutokana na migogoro ya kifamilia na ukatili unaofanywa na wenza wao.
Dhana ya kuwa wanaume ndio wanaochagiza matukio ya ukatili wa kijinsia, ndiyo iliyosababisha kuwepo kwa kauli kama: “Wanaume wote ni mbwa.”
Kauli hii si ngeni katika jamii yetu ya Kitanzania na hata duniani kwa ujumla. Mara nyingi husikika katika mazungumzo ya kawaida, mitandao ya kijamii na mijadala mbalimbali inayohusu mahusiano na ukatili wa kijinsia.
Kwa wengi, kauli hii hutumiwa kuelezea tabia za baadhi ya wanaume wanaohusika katika vitendo vya ukatili, unyanyasaji na ukandamizaji dhidi ya wanawake. Hata hivyo, swali la msingi linabaki kuwa: Je, ni sahihi kuwahukumu wanaume wote kwa matendo ya baadhi yao?
Afisa Tarafa Wilaya ya Ubungo, Beatrice Mbawala aliposhiriki moja ya midahalo ya ukatili wa kijinsia alisema; “ Mabadiliko yanaweza kutokea ikiwa wanaume watapewa kipaumbele katika kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto katika jamii,”
Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa wanaume wanatajwa kwa kiwango kikubwa kama wahusika wa vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake.
Kwa mujibu wa tathmini ya Benki ya Dunia kuhusu ukatili wa kijinsia nchini Tanzania, asilimia 42 ya wanawake ambao hawajaolewa walimtaja mpenzi wa sasa au wa zamani kama mhusika wa ukatili walioupata. Asilimia 31 walitaja marafiki au watu wanaowafahamu, huku asilimia 7 wakitaja watu wasiowafahamu. Aidha, katika taasisi za umma na serikali, wanaume walio katika nafasi za uongozi wameonekana kutajwa mara nyingi katika matukio ya unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wafanyakazi wanawake walio chini yao.
Takwimu hizi zinaonyesha wazi kuwa wanaume wanapaswa kuwajibika katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia. Hata hivyo, takwimu hizi pekee haziwezi kutumika kuhalalisha dhana kwamba wanaume wote ni wakatili.
Mfano mmoja unaogusa hisia ulielezwa na Mwalimu Peasis Kitela wa Shule ya Msingi Tanga wakati wa mdahalo wa kijinsia ulioandaliwa na TAMWA kwa kushirikiana na GIZ. Akisimulia tukio lililotokea katika eneo lao alisema:
“Tulipata kisa cha binti wa darasa la pili ambaye alikuwa hafiki shuleni. Wazazi wake walidhani yuko shule. Baada ya kufuatilia, ilibainika kuwa kutokana na kukosa fedha za chakula, alikuwa akienda bondeni ambako vijana wakubwa walimshawishi kwa kumpa miwa na shilingi mia mbili, kisha wakamfanyia ukatili wa kijinsia.”Amesema Mwalimu Kitela
Kisa hiki ni mfano mmoja tu kati ya mengi yanayoonesha namna baadhi ya wanaume na vijana wa kiume wanavyoshiriki katika vitendo vya ukatili wa kijinsia. Matukio kama haya ndiyo yanayochochea hisia hasi dhidi ya wanaume na kuzalisha kauli za jumla zinazowahusisha wanaume wote.
Kwa kutambua hali hiyo, Jeshi la Polisi kupitia Madawati ya Jinsia na Watoto limeendelea kuhamasisha jamii kuondokana na dhana kwamba huduma hizo ni kwa ajili ya wanawake pekee. Maafisa wa madawati hayo wamekuwa wakisisitiza kuwa wanaume wanaopitia ukatili wanapaswa kuripoti matukio hayo bila hofu, kwani sheria na mifumo ya ulinzi ipo kwa ajili ya kila mwananchi.
Kwa msingi huo, matumizi ya kauli za jumla kama “wanaume wote ni mbwa” hayasaidii kutatua tatizo la ukatili wa kijinsia.
Badala yake, kauli hizo hujenga chuki, huondoa utu wa baadhi ya wanaume wasiohusika na vitendo hivyo na wakati mwingine huweza kuwa aina ya ukatili wa kihisia na kisaikolojia. Akizungumza kuhusu suala hili, Ichaeli Maro anasisitiza kuwa matumizi ya lugha inayowahukumu watu kwa misingi ya jinsia zao hayachangii kutafuta suluhisho la tatizo, bali huongeza mgawanyiko katika jamii.
Wakati huo huo, wataalamu wa masuala ya jinsia wanaendelea kusisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wanaume katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Kwa mujibu wa Sylvia Daulinge, Meneja wa Mikakati wa TAMWA, suluhisho la kudumu la ukatili wa kijinsia linahitaji ushirikiano wa kila mtu. Anabainisha kuwa wanaume wanapaswa kuwa sehemu ya mabadiliko kwa kukemea ukatili, kuripoti matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu, kuelimisha vijana kuhusu usawa wa kijinsia na kujenga mahusiano yanayoheshimu utu wa kila mmoja.
.
