
Mwandishi wetu
Baada ya kukabidhi ripoti yake kwa Rais Samia Suluhu Hassan Aprili 23, Tume ya Uchunguzi wa Uvunjifu wa Amani Oktoba 29, 2025 inayoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Othman Chande imerudi kwa waandishi wa habari kufafanua baadhi ya mambo yanayohojiwa na wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari Aprili 28, 2026, mmoja wa wajumbe wa tume hiyo, Jaji Mkuu mstaafu Profesa Ibrahim Hamisi Juma amelalamikia suala la utoahji wa maoni, akisema japo kuna uhuru wa maoni, lakini kuna kundi linalotaka maoni yake yasikike peke yake.
Amesema wamepokea simu zaidi ya 300 za matusi kutoka kwa wananchi tangu walipokabidhi ripoti yao kwa wananchi, huku akidai kuwa wapo watu wanaoshambulia wengine kama nyuki kila wanapotoa maoni yao mitandaoni.
Kauli hii ni ishara ya mapokeo ya Watanzania kuhusu tume hiyo, kwamba hawana Imani nayo. Suala la kutokuwa na Imani lilianza mapema kabisa wakati wa uundwaji wa tume hiyo, ambapo watu walitarajia Serikali ingeruhusu tume huru ya kimataifa kuchunguza.
Wito huo pia ulitolewa na mataifa ya Ulaya yaliyoguswa na matukio ya mauaji na majeruhi wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025. Vilevile vyama vya CHADEMA na ACT Wazalendo vilikataa kuitambua tume hiyo vikitoa sababu pamoja na nyingine kwamba hata Rais Samia Suluhu Hassan anayeiunda pia ni mlalamikiwa wa matukio hayo, hivyo hawezi kujichunguza.
Kwa hiyo tangu tume hiyo inaanza kazi, ilikuwa imekosa uhalali wa kisiasa. Pamoja na ukweli kwamba iliundwa kisheria na hata Mahakama Kuu iliihalalisha baada ya baadhi ya watu kuishitaki mahakamani, lakini bado huku mitaani, wananchi hawana Imani nayo, ndiyo maana baadda ya kutoa ripoti, wananchi wanarusha salamu za matusi kama alivyosema Jaji Ibrahim Juma.
Mbaya zaidi, tume hiyo imeendeleza makosa yaleyale kwa kutoa kauli zinazowakwaza wananchi. Angalau wangejitahidi kuficha kutokuaminika kwao kwa kuleta hoja zenye mashiko, lakini wameshindwa kuwashawishi wananchi.
Kwa mfano, taarifa aliyoitoa Jaji Chande wakati akiwasilisha ripoti yake kwa Rais Samia, ilionyesha kuwa wamekwepa maswali ya msingi yaliyokuwa yakisubiriwa na wananchi.
Maswali makubwa yanayohojiwa na wananchi ni pamoja na kwa nini hakuna watu waliotajwa kuhusika na mauaji ya watu 518? Je, hao walijiua wenyewe? Nani anawajibika kwa yaliyotokea Oktoba 29, 2025?
Tume inasema maandamano yalipangwa na yaliratibiwa, lakini haiwataji waliopanga na kuratibu! Tume inadai kulikuwa na kambi 28 za mafunzo, lakini haisemi siko wapi na uthibitisho wake uko wapi. Wakasema moja ya kambo ilikuwa mita 10 tu kutoka kituo cha polisi, lakini hawakitaji. Kwa hiyo Polisi au vyombo vya usalama havikujua lolote kuhusu kambi hizo?
Katika maelezo yao, wanasema wasingeweza kutaja majina ya wahusika kwa kuwa waliotajwa wangekwenda mahakamani kuweka zuio, kwani hawakuitwa kuulizwa kwanza; sasa kama tume ilikuwa na nguvu za kimahakama kudai ushahidi mahali popote, ilishindwaje kuwaita hao wanaotajwa kuwauliza? Hayo mamlaka ya kimahakama waliyokuwa nayo waliyatumiaje?
Kwa mfano, Tume ilishindwa kuwaita viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama kama polisi, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), Magereza, na Uhamiaji na uhoji uhusika wao?
Tume ilishindwa kuviita vyama vya siasa au asasi za kiraia au watu wanaodaiwa kuchochea uharibifu? Nini kinafichwa?
Halafu wanasema wamependekeza kuundwa kwa tume nyingine ndiyo ichunguze huo uhalifu? Sasa tue hiyo nyingine itatumia sharia gani nyingine itakayowawezesha kutaja watu?
Huko ni kusongeza muda ili kuwalinda wahalifu, kwa sababu mwelekeo wa tume hii unaonyesha kufunika kombwe ili mwanaharamu apite.
Suala lingine linalokera wananchi kwenye ripoti hiyo ni suala la watu kupotea na kupotezwa, ambapo tume hiyo inalidogosha mno, wakati ni jambo zito katika jamii. Jaji Chande alisema taarifa za Polisi zinaonyesha watu 758 walipotea katika kipindi cha miaka mitatu na baada ya uchunguzi, watu 503 walipatikana (asilimia 66), watu 265 bado hawajulikani walipo (asilimia 34).
Akitaja sababu za watu kupotea kwa wale waliopatikana, Jaji Chande alisema ni pamoja na kulipizana kisasi, uhalifu, kukwepa mkono wa sharia, Imani za kishirikina, waliondoka bila taarifa kwao, usafirishaji wa binadamu haramu.
Kwa sababu hizo, watu wanajiuliza, mbona sababu za kisiasa hazitajwi? Mbona kuna ripoti nyingi za wakosoaji wa serikali waliopotezwa hazisemwi? Kwa mfano, kina Mdude Nyagali, Deusdedith Soka na wenzake, Simon Kangoye, Humphrey Polepole, mbona sababu zao hazitajwi?
Jaji Chande na wenzake wamekwepa suala hilo, wanazungumzia sababu ndogo ndogo na kuonyesha kwamba polisi inafanya kazi kubwa kuwarejesha wanaopotea. Halafu anataka kuonyesha kuwa, suala la watu kupotezwa ni la kawaida duniani, anaposema hata Ulaya watu wanapotea.
Huo ni ushahidi mwingine kwamba tume hii haiko huru, maana wanajua wakitaja sababu za kisiasa watamkwaza rais aliyewateua?
Kuhusu pendekezo la kuundwa kwa tume ya kimataifa, Jaji Chande akatetea tume yake akisema hata nchi nyingine zinaunda tume zake. Tulitarajia kwa mfano, Jaji Chande anayesemwa kuwa ana uzoefu wa kimataifa katika tume za uchunguzi, yeye ndiye atoe mwongozo wa hiyo tume ya kimataifa kama ingeundwa, lakini tena tunasikia tume hiyo ikikosoa uwepo wa tume ya kimataifa.
Kingine ni pale mjumbe wa tume hiyo, Jaji Hamisi Juma aliposema kuwa baadhi ya picha walizotumiwa zilikuwa zimechezewa na nyingine ni za Gaza. Hiyo nayo imeonyesha dharau kwa wananchi, kwa sababu wao ndiyo walishuhudia mauaji yakifanyika, iweje leo useme ilikuwa Gaza? Hao watu 518 wameuawaje sasa? Labda kama kuna video ya Waarabu waliyotumiwa.
Tume hii ilipaswa kueleza mbivu na mbichi, nini kilikuwa chanzo, nani alihusika na wanapendekeza nani achukuliwe hatua. Sasa tume hii imekuja kupaka mafuta, halafu wanatarajia kutakuwa na maridhiano. Maridhiano gani wakati ukweli haujaelezwa?
Kutojibiwa kwenye maswali muhimu ndiyo uthibitisho kuwa Tume ya Jaji Chande haikuwa na uhuru na ndiyo maana Rais Sakia alisema ile ripoti ni mali ya Rais, maana yeye ndiye aliyewatuma. Wapo wanaoikosoa tume hiyo, wakisema kwamba haiwahusu wananchi, bali ni suala la rais peke yake.
Pengine kwa kutaka kukwepa lawama, wamependekeza tume nyingine iundwe ili ibebe msalaba wa maswali wanayoulizwa.
Kwa ujumla Tume ya Jaji Chade haijakidhi matakwa ya wananchi, badala yake ietumika kusafisha waliohusika na matukio ya vurugu za Oktoba 29 na kufunika funika mambo ilimradi mambo yaendelelee kama kawaida.
Ikumbukwe kwamba matokeo ya tume hii ndiyo yatatumika kwenye uundwaji wa tume ya maridhiano, sasa unaridhianaje na watu ambao hawakuamini? Ili uwakusanye wananchi waridhiane ni lazima waamini na wakubaliane katika msingi, vinginevyo maridhiano hayo yatakuw ani ya kulazimisha na hueda yasifanikiwe kabisa.
