
Vikao vya Baraza la Wawakilishi wa Zanzibar vinavyoendelea vimeibua hisia kali kuhusu Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar, baada ya baadhi ya wawakilishi kulalamikia kuwa fursa za Wazanzibari zinaporwa au kuchukuliwa na watu kutoka Tanganyika.
Kauli hizo zimekuja wakati kukiwa na mjadala wa kwa nini raia wa upande mmoja (Tanzania Bara/Tanganyika) wanapokumbana na milango iliyofungwa au vikwazo wanapokwenda upande wa pili (Zanzibar), huku Wazanzibari wakifurahia uhuru mkubwa upande wa Bara.
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa mwaka 1964 na kuzaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umekuwa mfano wa kuigwa barani Afrika kwa kudumisha amani na utulivu.
Hata hivyo, ukiacha picha ya nje ya “Tanzania Moja,” kiuhalisia kuna mambo mengi ya kiutendaji, kisheria, na kiuchumi yanayouanya muundo huu kuonekana wa kusuasua—au kwa lugha rahisi, shaghalabaghala.
Sekta ya Afya: Vikwazo vya Vitambulisho vya Matibabu

Kauli ya hivi karibuni imetolewa na Kaimu Waziri wa Afya Zanzibar, Saada Mkuya Salum aliyekuwa akijibu hoja kwenye Baraza la Wawakilishi Zanzibar Juni 9, 2026 akisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haiwezi kugharamia matibabu kwa Watu wasio Wazanzibar.
Waziri Saada alisema kupitia Mfuko wa Huduma za Afya wa Zanzibar (ZDHSF), wanaotakiwa kuhudumiwa ni Wanzibari peke yao.
Alieleza kuwa bajeti ya Zanzibar ya takriban Sh8 trilioni haiwezi kubeba mzigo wa kutibu watu milioni 60 wa Tanzania nzima.
“Mtu ambaye si Mzanzibari, anakwenda katika hospitali zetu, anaonyesha kadi ya matibabu… Sasa hivi tunataka yeyote anayekuja na kadi ya matibabu inayotolewa kupitia Sheha wake, athibitishe kuwa yeye ni Mzanzibari kwa kuonyesha Kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi (ZANID).”
Hatua hii inamaanisha kuwa utambulisho wa “Utanzania” pekee hautoshi kupata huduma za afya visiwani humo, jambo linalokiuka dhana nzima ya udugu wa Muungano.
Hata hivyo, akihojiwa na DW Juni 10, 2026, Saada Mkuya alidai kuwa kauli yake imepotoshwa.
“Sisi Zanzibar kwa sababu kama unavyojua toka mapinduzi 1964 ilikuwa inatangaza matibabu bure na elimu bure ndio tunajua tulikuwa na hiyo theme ya matibabu bure na elimu bure.
“Kuna kitu tukichokitoa tulikuwa tunakiita Matibabu Kadi, hiyo Matibabu Kadi inasajiliwa kwa Sheha au Shehia husika kwamba wewe ni Mzanzibar unaandika maelezo yako halafu yule Sheha anatoa hiyo matibabu kadi kwenda hospitali. Lakini tuligundua Masheha wetu ambao hawako waaminifu kutokana na maelekezo waliyopewa,” alisema.
Alipoulizwa kama kuna takwimu za watu kutoka Bara wanagharimu Zanzibar kwa kiasi gani, alijibu:
“Nataka niliweke vizuri, sikuwahi kutaja sehemu kwamba Watu kutoka Bara ndio wanakuja, tunachokitaka kwamba tuweze kuwa na sustainable financing ya kugharamia huduma za Afya, tuweze kulipa vipimo, tuweze kulipa dawa, tuweze kulipa wataalamu, tuweze kulipa mambo yote yanayohusiana masuala ya afya, sikuzungumza mahala popote kwamba kuna Watu kutoka Bara nimesema Wasio Wazanzibar.”
Soko la Ajira na Uhifadhi wa “Wazawa”

Kauli nyingine ilitolewa na Naibu Waziri wa Vijana, Ajira na Uwezeshaji wa Zanzibar Hassan Khamis Hafidh, wakati akichangia Makadirio ya Mapato na Matumizi Bajeti ya Vijana katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar Juni 6, 2026, akisema licha ya visiwa hivyo kuwa na hoteli nyingine za utalii, walioajiriwa ni wageni (kutoka Bara).
“Zanzibar nzima kuna hoteli zilizosajiliwa 1,184, hoteli zilizosajiliwa, zipo na ukienda mheshimiwa Spika, wanaofanya kazi katika hoteli zile sio wazawa kweli. Ukweli nani anabisha?
“Sasa jukumu letu kama Wizar aya Vijana ni kufanya mapinduzi kwamba sasa waliokuwemo mle sio wazawa, wawe wazawa. Mniachie kazi hiyo naiweza,” alisema.
“Jukumu la Wizara hii ya Vijana ni kuhakikisha vijana wanapata kazi katika mahoteli,” aliongeza.
Alitoa mfano wa hotelimoja visiwani humo, akisema ina wafanyakazi wafanyakazi 156, ambapo kati yao vijana wa Kizanzibari walikuwa 27.
Hata hivyo, akifafanua hoja yake kupitia mahojiano maalum na Ayo TV Juni 10, Hassan alisema hakutaja neno Tanganyika wala Vijana Kitanganyika kwamba watafukuzwa katika hoteli kama ambavyo imesambazwa kwenye mitandao ya Kijamii.
“Nikasema kwa data kabisa katika ajira hizi za mahoteli, Vijana wetu wa Kizanzibar hawamo katika ajira zile, wapo Watu mbalimbali kutoka Nje ya Zanzibar na Nje ya Tanzania waliokuwemo katika ajira huo ndio ukweli uliopo,” alisema.
Akikoleza mjadala huo, Zainab Shomari, mwakilishi wa wanawake CCM Zanzibar, alisema, “Ukienda kwenye mahoteli yale utawakuta kwamba wanafanyakazi zile ndani ya hoteli, Wazanzibari ni wachache mno. Kisingizio wanasema hawana elimu.”
Mwakilishi wa jimbo la Ole, Seif Hamad Suleiman alilalamika kuwa Wazanzibari wanabaguliwa kwenye ajira.
“Zipo kampuni zinakuja kufanyakazi Zanzibar lakini kwa masikitiko makubwa na bahati mbaya sana, wanufaika wa ajira kwenye kampuzi zile sio Wazanzibari wala sio vijana wa maeneo yale. Leo ukienda kufanya utafiti, wafanyakazi wengi ni wageni kutoka Tanzania Bara, jambo hilo sio sahihi.
“Vijana wa Ole wako pale, vijana wa Vitongoji wapo pale, vijana wa Wawi wanazipataje ajira zile na wanazo sifa za kuajiriwa?” alihoji.
Hata makahaba wanatoka Bara?
Akijibu swali kuhusu biashara ya ukahaba visiwani humo Juni 10, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar, Hamza Hassan Juma alisema kumekuwa na juhudi zinazoshirikisha Jeshi la Polisi kuiwakamata watu wanaofanya biashara hiyo, japo alisema changamoto ni namna ya kupata ushahidi.
“Biashara zao huwa wanazifanya barabarani. Kwa hiyo wakati mwingine kumkamata mtu anapita barabarani bila kumkamata na ushahidi fulani inakuwa ni changamoto moja. Lakini mazingira hasa ya mavazi ndio yale mazingira ambayo yanatufanya tunamtuhumu mtu halafu tunakuwa tunamchukulia zile hatua za kisheria,” alisema.
Kuhusu swali kwamba wanatokea wapi, Waziri Juma alisema, “Mheshimiwa mwenyekiti, wengi ambao tuliokuwa tukiwakamata katika operesheni zile, wengi ni vijana kutoka Tanzania Bara na wengine hata Kenya.
“Kwa hiyo hatujawahi kuwakuta hasa vijana wa Kizanzibari katika maeneo yale kwa sababu mara nyingi tunapowakamata tunapofanya operesheni wanapelekwa polisi, siku ya pili moja kwa moja huwa wanapelekwa mahakamani kwa sababu na ule ushahidi hasa hata na yale mavazi ambayo aliyoyavaa. Kwa hiyo mavazi kama yale kwa vijana wetu wa Kizanzibari hawa… sio rahisi kuweza kuwakuta,” alisema.
Kama Wazanzibari wanahoji, kwa nini Watanganyika nao wasihoji?
Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi ameandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa X akisema kama wabunge Wawakilishi wameonekana kupigania misingi ya Uzanzibari ni wakati wa Watanganyika nao kuzungumza kwa uwazi, kuhoji kwa uhalali na kujadili kwa kina masuala yanayohusu haki, hadhi na maslahi ya Tanganyika.
Je, Watanganyika hawana haki ya kuhoji na kulinda bandari zilizopo ndani ya Tanganyika, misitu na rasilimali za mazingira za Tanganyika, rasilimali za asili zilizopo katika eneo la Tanganyika, hadhi, haki na umiliki wa ardhi ya Tanganyika?” amehoji.
Amehoji pia nafasi, haki na uwepo wa watu wasio Watanganyika katika idara na taasisi ambazo si za Muungano, uhalali wa viongozi wasio Watanganyika kuingia au kusaini mikataba inayohusu rasilimali za Tanganyika, hususan pale ambapo baadhi ya masuala hayo tayari yameondolewa katika eneo la Muungano kwa upande wa Zanzibar.
Pia amehoji mchango wa Zanzibar katika kugharimia gharama za uendeshaji wa shughuli za Muungano na Ulipwaji wa Deni la Taifa.
“Ikiwa ni halali kwa Wazanzibari kujadili, kuhoji na kulinda maslahi ya Zanzibar kwa misingi ya utambulisho wao wa kisiasa na kikatiba, kwa mantiki hiyo hiyo haipaswi kuwa kosa kwa Watanganyika kuhoji, kujadili na kutetea maslahi ya Tanganyika,” amesema.
Akizungumza Juni 10 jijini Dodoma, Ado shaibu Mbunge wa Tunduru Kaskazini amesema bila muundo wa Muungano kufanyiwa mapitio, malalamiko ya Wazanzibari na Watanganyika hayatakoma.
“Ni wakati muafaka sasa kwa serikali kukubali kwamba muundo wetu wa sasa wa muungano unaleta mikanganyiko na ni vizuri kufanya mapitio ya muundo huu kupitia mchakato wa katiba mpya ili tuwe na muundo wa serikali tatu kama ulivyopendekezwa kwenye rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba almaarufu rasimu ya Jaji Warioba.
“Hili ndilo litalokata mzizi wa fitina. Bila hivyo, Watanzania wataendelea kulalamika, Watanganyika wataidai Tanganyika yao, na hakuna nguvu yoyote inayoweza kuwarudisha nyuma Watanganyika kuidai Tanganyika yao.”
