

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimewasilisha majibu rasmi kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kikipinga vikali tuhuma za ukiukwaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa na kukataa tishio la kusimamishwa kwa usajili wake au kutozwa faini.
Katika barua hiyo ya kurasa 30 iliyowasilishwa Mei 19, 2026 na kutiwa saini na Katibu Mkuu wa chama hicho, John John Mnyika , CHADEMA imebainisha kuwa barua ya Msajili yaMei 7, 2026 ina kasoro kubwa za kisheria na inalenga kukandamiza uhuru wa kisiasa na haki za kikatiba.
CHADEMA imeeleza kuwa barua ya Msajili ina kasoro inayojulikana kisheria kama duplicity. Chama kinahoji kuwa hatua ya Msajili kudai maelezo kuhusu tuhuma za uvunjifu wa sheria, na hapo hapo kutaka chama kitoe utetezi wa kwa nini kisifungiwe au kutozwa faini kabla hata tuhuma hizo hazijathibitishwa, ni kukiuka misingi ya haki ya kujitetea inayolindwa na Ibara ya 13(6)(a) ya Katiba ya nchi.
Wakifafanua tuhuma za Msajili kuhusu John Heche (Makamu Mwenyekiti Bara), CHADEMA wamesema maandamano ya amani ni haki ya kikatiba (Ibara ya 20(1)) na si uchochezi. Aidha, imesisitiza kuwa kama kuna kosa la kuingilia au kudharau Mahakama, mamlaka hayo yanamilikiwa na Mahakama yenyewe au DPP na si Ofisi ya Msajili.
Kuhusu Oliver Kisaka aliyedaiwa kutoa kauli za uchochezi wa kutumia nguvu. CHADEMA imebainisha kuwa neno mageuzi linaweza kuwa la kikatiba na la amani, na kwamba tafsiri ya Ofisi ya Msajili inaminya uhuru wa mawazo unaolindwa na Ibara ya 18 ya Katiba.
