
Tanzania imeshindwa kupata hukumu ya hatia kwa washukiwa wa biashara haramu ya binadamu katika kipindi cha taarifa, licha ya kuongeza juhudi za uchunguzi na utambuzi wa waathirika wa uhalifu huo, kwa mujibu wa Ripoti ya Mwaka 2026 kuhusu Biashara Haramu ya Usafirishaji Binadamu.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa Serikali ilichunguza kesi 30 za biashara haramu ya binadamu, ikilinganishwa na kesi saba katika kipindi kilichotangulia.
Hata hivyo, ilifungua mashtaka mapya dhidi ya washtakiwa wanane na haikupata hukumu yoyote ya hatia, tofauti na hukumu nne zilizotolewa katika kipindi kilichopita.
Kutokana na juhudi zilizoongezeka, Tanzania imeendelea kuainishwa katika Kundi la Pili (Tier 2), linalomaanisha kuwa haijafikia viwango vya chini vinavyohitajika kutokomeza biashara haramu ya binadamu, lakini inachukua hatua muhimu kukabiliana na tatizo hilo.
Kwa upande wa ulinzi wa waathirika, Serikali iliwatambua watu 58 walioathirika na biashara hiyo na kuwapeleka 53 kupata huduma za msaada. Kati yao, watu 41 walinyonywa kupitia kazi za kulazimishwa, 10 kupitia biashara ya ngono, huku saba wakihusishwa na aina nyingine za biashara haramu ya binadamu ambazo hazikubainishwa.
Waathirika hao walijumuisha watu wazima 40, wote wakiwa wanawake, na watoto 18, wakiwamo wavulana watatu na wasichana 15. Raia wa Tanzania walikuwa 50, huku wengine wanane wakitoka Burundi, Rwanda, Indonesia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Serikali ilitumia Sh1.4 bilioni kwa huduma za waathirika, zikiwamo malazi, matibabu, ushauri nasaha, msaada wa kisheria na kurejesha waathirika nchini. Kiasi hicho kiliongezeka kutoka Sh663 milioni katika kipindi kilichotangulia.
Hata hivyo, taarifa inaonyesha kuwa rushwa na madai ya baadhi ya maafisa wa umma kuhusika katika biashara haramu ya binadamu vinaendelea kuwa changamoto kubwa katika juhudi za kukabiliana na uhalifu huo.
Serikali haikuripoti mashtaka mapya wala hukumu dhidi ya wafanyakazi wa umma wanaotuhumiwa kuhusika na uhalifu huo.
Wakati huohuo, maafisa 10 wa uhamiaji waliokuwa wamesimamishwa kazi katika kipindi kilichotangulia waliendelea kuchunguzwa kuhusu uwezekano wa kuhusika katika ukiukaji wa taratibu za ajira za kulazimishwa wakati wa kutoa pasipoti kwa zaidi ya wasichana 30 wa Kitanzania waliokuwa wakielekea Falme za Kiarabu kufanya kazi za majumbani.
Taarifa pia inaeleza kuwa mitandao ya kijamii na matangazo ya ajira za uongo vinazidi kutumiwa kuwarubuni Watanzania kwa ahadi za ajira zenye maslahi makubwa nje ya nchi.
Baadhi ya waathirika huingia katika mikataba ya unyonyaji baada ya kushawishiwa kwa ahadi za kulipiwa usafiri, malazi na nyaraka za safari, kisha kulazimishwa kufanya kazi ili kulipa gharama hizo.
Watanzania wamekuwa katika hatari ya kunyonywa katika nchi mbalimbali za Afrika, Mashariki ya Kati, Asia na Urusi. Baadhi yao wamerubuniwa kwa ahadi za ajira za ulinzi, ujenzi au mafunzo ya ufundi, lakini baadaye kukabiliwa na mazingira mabaya ya kazi na kulazimishwa kushiriki katika shughuli ambazo hawakukubaliana nazo.
Katika kukabiliana na changamoto hizo, Serikali imeongeza wafanyakazi 48 katika Sekretarieti ya Kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu (ATS), imeendesha kampeni za uhamasishaji kuhusu matumizi salama ya intaneti na kutoa mafunzo kwa maafisa wa sheria kuhusu uchunguzi wa ushahidi wa kielektroniki.
Pamoja na hatua hizo, Tanzania bado haina mpango kazi wa kitaifa uliopitishwa wa kupambana na biashara haramu ya binadamu. Pia, taarifa inaeleza kuwa Serikali haina mfumo mmoja wa kitaifa wa kukusanya takwimu za uhalifu huo, hali inayoweza kusababisha baadhi ya matukio kutoripotiwa.
Taarifa inasisitiza kuwa umaskini, ukosefu wa ajira kwa vijana na udhaifu wa mifumo ya ulinzi wa waathirika vinaendelea kuongeza hatari ya watu kuingia katika biashara hiyo. Watoto na vijana walio katika mazingira magumu ni miongoni mwa makundi yanayoathirika zaidi.
Kwa ujumla, ingawa Serikali imeongeza juhudi za kuchunguza kesi, kuwatambua waathirika na kutoa huduma, kutokuwepo kwa hukumu za hatia katika kipindi husika, pamoja na changamoto za rushwa na udhaifu wa mifumo ya ulinzi, kunaendelea kuzuia mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu nchini.
