
Siku chache kabla ya kifo chake, Diana Edward Sajilo alikuwa na mambo mawili yaliyokuwa yakimkabili kwa wakati mmoja; kwanza maandalizi ya mitihani na kutafuta fedha za ada ili aweze kuendelea na masomo yake.
Mwanafunzi huyo wa Chuo Kikuu cha Kampala International University in Tanzania (KIUT), aliyekuwa akisomea udaktari (MD), alikuwa amerejea Dar es Salaam baada ya kusafiri kwenda Dodoma, huku akiwa katika maandalizi ya mitihani yake.
Lakini mipango hiyo ilikatishwa ghafla baada ya Diana kupoteza maisha katika mazingira ambayo familia yake inasema yanahusishwa na uhusiano wake wa kimapenzi na mwanaume aliyemtaja kuwa Dickson Msigwa.
Diana alikutwa amefariki ndani ya chumba alichokuwa amepanga Mzambarauni, Gongolamboto, Dar es Salaam, baada ya familia yake kumtafuta kwa muda na hatimaye kuvunja mlango wa nyumba hiyo.
Mtu anayehusishwa na Diana, kwa mujibu wa ndugu na marafiki waliozungumza kuhusu tukio hilo, hakuwapo eneo hilo wakati mwili ulipogundulika na hadi wakati wa maelezo yao alikuwa hajakamatwa.
Familia inasema polisi wameanza uchunguzi wa tukio hilo.
Alikuwa akitafuta ada
Kwa mujibu wa kaka yake, Thomas James, Diana alikuwa amemweleza kuhusu changamoto ya ada na kumuomba msaada ili aweze kufanya mitihani.
Thomas anasema walikuwa wamepanga kukutana Ijumaa ili amkabidhi fedha ambazo alikuwa ameahidi kumtafutia.
Siku chache kabla ya hapo, walikutana Jumatano Septemba 30 na kuzungumzia namna ya kumsaidia kupata fedha hizo.
Thomas anasema alikuwa akitafuta fedha hizo kupitia wapangaji wake na alikuwa na matumaini kwamba ifikapo Ijumaa angeweza kumpatia kiasi cha kumsaidia Diana kurejea chuoni.
Alisema Ijumaa asubuhi alipata fedha kutoka kwa mmoja wa wapangaji wake na akaamua kumpigia simu mdogo wake ili aje kuchukua. Lakini simu ilipopigwa haikupokelewa.
Alipopiga tena, simu hiyo ilipokelewa na rafiki wa Diana, aliyemtaja kwa jina la Magreth.
Thomas alipoeleza kuwa alikuwa kaka yake Diana na alitaka kuzungumza naye, aliambiwa Diana hayupo.
Baadaye aliambiwa Diana alikuwa ameondoka siku iliyotangulia na mwanaume aliyekuwa mpenzi wake.
“Mbona Diana aliondoka jana, nani Msigwa alikuja kumchukua na pikipiki wakaondoka,” Thomas anakumbuka alivyoambiwa.
Awali hakudhani kuwa kuna tatizo kubwa kwa sababu alijua Diana alikuwa katika uhusiano na mwanaume huyo.
Thomas anasema alifikiri huenda Diana alikuwa ameenda kwa mpenzi wake na angeweza kurudi baada ya siku kadhaa.
Lakini baada ya muda simu ya Diana kutopatikana na pia kushindwa kumpata mwanaume huyo, alianza kuwa na wasiwasi.
Alikwenda kumtafuta
Thomas aliondoka kwenda Mzambarauni, eneo ambalo mwanaume huyo alikuwa akiishi.
Alipofika alikuta mlango umefungwa na simu ya mwanaume huyo haikupatikana.
Aliendelea kuulizia kwa watu waliokuwa wakimfahamu na kuelekezwa maeneo mbalimbali ambako alidhani angeweza kumpata.
Alimtafuta pia rafiki wa karibu wa mwanaume huyo, Zengo, lakini hakufanikiwa kupata taarifa iliyomsaidia kumpata.
Baadaye Thomas alipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kuwa ndugu wa Dickson.
Mtu huyo alisema Dickson hapatikani kwenye simu na kwamba walikuwa wakielekea Hospitali ya Mloganzila kuangalia kama huenda alikuwa amepata ajali.
Thomas anasema baada ya muda alipigiwa tena simu na kuambiwa kuwa hakuna mtu aliyelazwa au kufariki kutokana na ajali hiyo katika hospitali hiyo.
Taarifa hiyo iliongeza wasiwasi wake.
Mlango wavunjwa
Baadaye Thomas alipigiwa simu na kuambiwa watu walikuwa wakielekea katika nyumba ya Dickson ili kuvunja mlango.
Alisema alishangazwa na hatua hiyo kwa kuwa kwa wakati huo Diana alikuwa ametoweka kwa muda mfupi tu kwa mtazamo wake.
Hata hivyo, alikwenda Mzambarauni na kukuta ndugu wa Dickson, mwenye nyumba na viongozi wa eneo hilo.
Walimsubiri mjumbe na mwenyekiti wa eneo kabla ya kuanza kuvunja mlango.
Thomas anasema baada ya mlango kufunguliwa, alishuhudia jambo ambalo lilimfanya apoteze fahamu kwa muda.
“Baada ya kufungua mlango, mdogo wangu alikuwa amelala chini. Nikaona Diana huyu hapa, nilianguka na kupoteza fahamu,” anasema.
Baafaye alipozinduka anasema aliwaona polisi wakiwa wanakagua eneo hilo.
Kwa mujibu wa Thomas, polisi waliwaondoa watu waliokuwa wamejazana eneo hilo na kuanza kufanya uchunguzi wa ndani ya nyumba.
Walihoji ndugu, mwenye nyumba na watu wengine waliokuwa eneo hilo kabla ya kuondoka na kueleza kuwa wangewasiliana na familia pale watakapohitaji maelezo zaidi.
Historia ya uhusiano
Mjomba wa Diana, Lucas Christopher, anasema taarifa alizokusanya kutoka kwa familia na majirani zinaonyesha kuwa Diana na Dickson walikuwa na uhusiano wa kimapenzi ambao wakati mwingine ulikuwa na migogoro.
Anasema majirani walieleza kuwa wawili hao walikuwa wakigombana mara kwa mara.
Kwa mujibu wa rafiki wa Diana, Angel Mgonja, Dickson alimaliza masomo yake ya Clinical Officer mwaka 2023 na alihitimu.
Angel anasema alimfahamu Dickson tangu walipokuwa KIUT na baadaye alimwona mara kadhaa alipokuwa akimtembelea Diana.
Baada ya kumaliza chuo, Angel anasema Dickson aliwahi kufanya biashara ya chipsi kabla ya kuingia katika biashara ya samani, hasa vitanda, na pia kufanya kazi za utabibu katika zahanati za mitaani.
Angel pia anasema Diana aliwahi kuwaeleza marafiki zake kuwa alikuwa katika uhusiano na Dickson tangu mwaka 2017, baada ya kumaliza kidato cha nne.
Diana alivyopambana kumaliza masomo
Maelezo ya Angel yanaonyesha kuwa safari ya Diana ya elimu haikuwa rahisi.
Wawili hao walianza pamoja kozi ya udaktari KIUT mwaka 2021 na waliendelea hadi mwaka wa tatu.
Baadaye Diana alifiwa na mama yake ambaye alikuwa akigharamia masomo yake.
Kutokana na changamoto hiyo, Diana alilazimika kusitisha masomo kwa muda ili kutafuta namna ya kupata fedha za ada.
Angel anasema Diana aliamua kutumia kipaji chake cha ususi kwa kufungua saluni ya wanawake.
“Ilibidi Diana afungue salon ya kike kwa sababu yeye ni msusi mzuri,” alisema Angel, akieleza kuwa Diana alikuwa akimsuka tangu walipofahamiana.
Kwa njia hiyo, Diana aliweza kuendelea na masomo huku akijilipia ada.
Wakati wa kifo chake, alikuwa akijiandaa kufanya mitihani na alikuwa akihitaji fedha za ada.
Siku ya mwisho
Magreth Wayega, aliyesoma na Diana kuanzia kidato cha tano na sita na baadaye KIUT, anasema siku ya tukio Oktoba 1, 2026, Diana alikuwa nyumbani kwake Gongolamboto akisuka mteja.
Kwa mujibu wa Magreth, majira ya saa nne asubuhi Dickson alifika na kumwomba Diana waondoke mara moja.
Alisema mwanaume huyo alimweleza Diana kuwa walikuwa wanakwenda kushughulikia malipo ya ada ya chuo.
Diana alimwacha mteja aliyekuwa akimsuka na kumuahidi kuwa angerudi. Lakini hakurudi.
Magreth anasema hadi saa sita mchana Diana alikuwa bado hajarejea.
Baadaye watu waliokuwa wakimtafuta walianza kuwa na wasiwasi.
Alipokwenda katika eneo ambalo Dickson alikuwa akiishi, Magreth anasema alikuta mlango umefungwa.
Baadaye, Dickson alirejea na kusema alikuwa amekuja kuchukua baadhi ya vitu vya Diana.
Magreth alikataa kumpa vitu hivyo akisema alitaka Diana mwenyewe aje kuvichukua.
“Alikuja akisema amefuata vitu vya Diana. Mimi nilimkatalia nikamwambia siwezi kumpa mpaka aje Diana mwenyewe,” alisema.
Kwa mujibu wa Magreth, mwanaume huyo aliondoka baada ya kukubaliana na hali hiyo.
Simu iliyobaki saluni
Moja ya mambo yaliyoibua maswali katika familia ni simu ya Diana.
Kwa mujibu wa maelezo ya familia na marafiki, Diana aliiacha simu yake kwa rafiki yake Magreth kabla ya kuondoka na Dickson.
Thomas alipoanza kumtafuta, simu hiyo ilipokelewa na Magreth.
Kwa mujibu wa Christopher , baadaye Dickson alikwenda kwa Magreth akiitaka simu ya Diana pamoja na baadhi ya nguo zake.
Hata hivyo, Magreth alikataa kumpa simu hiyo.
Simu hiyo baadaye ilichukuliwa na polisi kwa ajili ya uchunguzi.
Christopher anasema anaamini huenda simu hiyo ilikuwa na mawasiliano ambayo Dickson alitaka kuyaona au kuyafuta, lakini anasisitiza kuwa hiyo ni hisia yake na kwamba majibu ya kweli yako katika uchunguzi wa polisi.
Mzozo wa kimapenzi
Christopher anasema kwa mtazamo wa familia, wivu wa kimapenzi unaweza kuwa sehemu ya mazingira yaliyopelekea tukio hilo.
Anasema kulikuwa na madai kuwa Dickson alihisi Diana alikuwa na mtu mwingine.
Christopher pia anasema baada ya mlango wa nyumba kufunguliwa, mazingira yalionyesha kana kwamba kulikuwa na mapambano ndani.
Anadai kulikuwa na dalili zinazoashiria kuwa Diana huenda alichomwa kisu, lakini matokeo rasmi ya uchunguzi wa kitabibu hayakuwa yamekabidhiwa familia wakati wa maelezo hayo.
Katika hilo, Angel anasema wiki mbili kabla ya kufikwa na umauti, Diana aliondoka kwa Dickson na kwenda kuishi kwa rafiki yake ambaye hakumtaja.
“Kwanza Diana alikuwa akijiandaa na mitihani, halafu kutokana na mizozo, alihitaji kupata utulivu ndiyo maana aliamua kuhamia kwa rafiki yake.
“Hiyo siyo mara ya kwanza, wamekuwa wakizozana mara kwa mara na wakati mwingine Diana alikuwa akihamia kwa rafiki zake mpaka mzozo uishe,” amesema.
Hata hivyo, Magreth Wayega aliyesoma pia na Diana, anasema alikuwa akienda nyumbani kwake kujisomea na wanafunzi wengine kwa ajili ya maandalizi ya mitihani.
Polisi waanza uchunguzi
Baada ya mwili kugundulika, polisi waliuchukua na kuufanyia uchunguzi wa kitabibu katika Polisi Barracks.
Christopher anasema familia haikupewa ripoti ya ‘postmortem’ na kwamba taarifa hiyo ilibaki kwa mpelelezi wa kesi.
Familia ilipewa kibali cha mazishi na kukabidhiwa mwili.
Thomas anasema mpelelezi alimweleza kuwa mtu anayehusishwa na tukio hilo alikuwa bado hajakamatwa.
Pia aliombwa kutoa taarifa zake binafsi ili aweze kupatikana iwapo angehitajika kutoa ushahidi mahakamani.
Familia baadaye iliendelea na taratibu za mazishi.
Tetesi za kutoroka
Katika kipindi ambacho familia ilikuwa ikimtafuta Dickson, zilianza kusambaa taarifa kwamba alikuwa ameonekana maeneo mbalimbali, ikiwamo Mwanza.
Thomas anasema alifuatilia baadhi ya taarifa hizo lakini hakupata uthibitisho.
Alipowasiliana na watu aliowafahamu Mwanza, aliambiwa hakuna taarifa ya Dickson Msigwa kuwa amekamatwa huko.
Hatimaye alihitimisha kuwa baadhi ya taarifa hizo zilikuwa tetesi ambazo hazikuthibitishwa.
