
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza, ameunga mkono kauli ya Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, kuwa kuna rushwa ndani ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) huku akihoji kama Waziri huyo amewachokoza vijana au ameichokoza rushwa.
Bagonza ameeleza hayo kupitia chapisho aliloweka kwenye ukurasa wa mtandao wake wa kijamii wa Facebook, ambapo amesema mchanganuo huo wa Waziri umegusa tatizo sugu linalozidi kuenea na kutishia taasisi nyingi za Taifa.
Katika maelezo yake, Dk Bagonza amehoji iwapo Mchengerwa “kawachokoza vijana au kaichokoza rushwa,” akisema kwamba Waziri huyo anashambuliwa na pande zote mbili na labda kuna sababu za kushambuliwa kwake.
Amefafanua kuwa Mchengerwa anapigwa na vijana waliohisi kudhulumiwa, pamoja na mtandao wa watu wanaotaka suala la rushwa lisichunguzwe ili kulinda maslahi yao.
Askofu Bagonza ameeleza kuwa rushwa imekuwa kama kansa ya taifa ambayo haiko UVCCM pekee, bali imesambaa katika vyama vya siasa, Serikali, taasisi za dini, vyombo vya habari, mahakama na hata katika sekta ya elimu.
Ameongeza kuwa Mchengerwa hakusema kitu kibaya kwa kuonyesha UVCCM imezama katika rushwa, bali “kawasingizia ukweli watu kwa njia mbaya,” huku akisisitiza kuwa rushwa sasa hivi inatumika kama chungu cha kupikia viongozi katika vyama vyote.
Tuhuma hizo za Mchengerwa zimeibua majibu ya ukali kutoka kwa viongozi wa UVCCM ambapo Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Dodoma, Abdulhabibi Mwenyemba, alikataa vikali madai hayo akisema vijana wa CCM hawawezi kukubali kuhusishwa na vitendo vya rushwa.
