
Mahakama Kuu ya Mombasa nchini Kenya imempata na hatia mchungaji Paul Mackenzie pamoja na washtakiwa wenzake 28 kwa mauaji ya watu 191 wakiwemo watoto 190 katika mkasa ulioshitua ulimwengu wa msitu wa Shakahola.
Akitoa hukumu hiyo, Jaji Diana Kavedza Mochache ameeleza kuwa upande wa mashtaka umethibitisha ushahidi dhidi ya washtakiwa wote 29 bila kuacha shaka yoyote ya kisheria. Mahakama imetupilia mbali hoja ya utetezi iliyodai kuwa wahanga waliamua kufunga kula kwa hiari yao, ikifafanua kuwa watoto walioathirika hawakuwa na uwezo wa kisheria wa kufanya maamuzi kama hayo.
Ushahidi uliowasilishwa mahakamani umeonyesha kuwa Mackenzie ndiye aliyeanzisha na kuongoza utaratibu huo wa kufunga kula hadi kufa katika shamba lake lenye ukubwa wa ekari 800 eneo la Shakahola. Mfumo huo uliwataka watoto kuanza kufunga kwanza, wakifuatiwa na vijana, wanawake, na hatimaye wanaume.
Ripoti za uchunguzi wa miili zilibaini kuwa watoto wengi walifariki kwa njaa, huku vifo vingine vikisababishwa na kukosa hewa, kwa kubanwa shingo, pamoja na majeraha ya kichwa. Ingawa miili 110 haikuweza kubainika chanzo chake moja kwa moja kutokana na kuharibika vibaya, mahakama hitimisho lake ni kwamba wote walifariki kutokana na mfumo huo wa njaa.
Licha ya Mackenzie kukana mashtaka hayo na kudai hakumlazimisha mtu yeyote, mahakama imeshikilia kuwa kitendo hicho kilikuwa sehemu ya Mfumo wa Dini wenye nia ya kudhuru na kuangamiza maisha.
Baada ya kumpata na hatia hizo, Mahakama imepanga Novemba 6, 2026 kuwa tarehe rasmi ya kutoa adhabu dhidi ya Mackenzie na wenzake.
Mbali na kesi hiyo, Mackenzie bado anakabiliwa na mashtaka mengine tofauti yanayohusiana na vifo vya watu 52 katika eneo la Kwa Binzaro, mashtaka ambayo pia ameyakana.

