Mwandishi Wetu, Wino Tz
Dar es Salaam. Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa mkutano wa kimataifa kuhusu uhamaji wa nguvu kazi, unaojulikana kama Doha Dialogue, utakaowakutanisha nchi za Afrika pamoja na nchi za Ghuba ikiwamo Falme za Kiarabu, Oman, Qatar na Kuwait.
Akizungumza na wanahabari jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi na Ajira, Deus Sangu, amesema mkutano huo ni jukwaa muhimu la kimataifa litakalowezesha nchi washiriki kuimarisha ushirikiano katika usimamizi wa uhamaji wa nguvu kazi na kukuza ajira zenye staha.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano huo.
Kwa mujibu wa Waziri Sangu, Doha Dialogue ulifanyika kwa mara ya kwanza mjini Doha, Qatar, ukihusisha nchi 33, zikiwamo nchi 25 za Afrika.
“Tanzania ilishiriki katika mkutano huo wa kwanza uliofanyika Oktoba 2024, ambao ulihitimishwa kwa Doha Declaration, iliyoweka msingi wa kuendeleza majadiliano na ushirikiano kuhusu uhamaji wa nguvu kazi” amesema

Tanzania imekuwa nchi ya pili kuwa mwenyeji wa Doha Dialogue, baada ya Qatar, huku mkutano huo ukiwa unalenga kujadili namna ya kuimarisha mifumo ya uhamaji wa nguvu kazi na upatikanaji wa ajira.
Masuala yatakayojadiliwa
Waziri Sangu amesema mkutano huo utajadili masuala mbalimbali yanayohusu uhamaji wa nguvu kazi, ikiwamo kuimarisha mikataba ya ajira kwa wafanyakazi, mahitaji ya soko la ajira, mifumo ya kiteknolojia ya uhamaji wa nguvu kazi na upatikanaji wa ajira zenye staha.
Amesema mkutano huo utatoa fursa ya kimkakati kwa Tanzania na nchi nyingine kujadili namna ya kupanua fursa za ajira nje ya nchi, kulinda haki za wafanyakazi wahamiaji na kuongeza ushindani wa nguvu kazi ya Tanzania katika soko la kimataifa.
Aidha, amesema majadiliano hayo yanatarajiwa kuchangia utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050.
“Mkutano huu unatarajiwa kuongeza ushirikiano kati ya Tanzania na nchi za Ghuba, pamoja na kukuza uhamaji wa nguvu kazi ulio salama, rasmi, wenye haki, tija na endelevu,” amesema.
Amesema Tanzania pia inatarajia kutumia mkutano huo kuimarisha mifumo ya uhamaji wa nguvu kazi kwa haki na kuweka misingi ya ushirikiano wa muda mrefu kati ya nchi zinazohusika.
Uhamaji salama kwa Waafrika
Mkutano huo, ambao utafanyika kwa mara ya kwanza barani Afrika, pia unatarajiwa kujadili namna ya kuhakikisha Waafrika wanaohamia nchi nyingine kwa ajili ya ajira wanapata fursa salama, rasmi na zinazolinda haki zao.
Waziri Sangu amesema Tanzania tayari imechukua hatua mbalimbali katika kusimamia uhamaji wa nguvu kazi, ikiwamo kusimamia mikataba salama ya ajira na kuwaunganisha Watanzania wenye ujuzi na fursa za ajira katika nchi nyingine.
Amesema Serikali pia imeweka utaratibu wa kusimamia mawakala wanaohusika na kuwasafirisha wafanyakazi kwenda kufanya kazi nje ya nchi, ili kuhakikisha mchakato huo unafuata taratibu na unalinda maslahi ya wafanyakazi.
Aidha, Serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya kidijitali inayolenga kuboresha udhibiti na usimamizi wa wafanyakazi wahamiaji.
Kwa mujibu wa Waziri Sangu, hatua hizo ni sehemu ya juhudi za Tanzania kuhakikisha uhamaji wa nguvu kazi unakuwa salama, wenye tija na unaozingatia haki za wafanyakazi.
