Vyombo vya habari vina mchango katika kupaza sauti kumaliza ukatili wa Kijinsia
Na Mwandishi Wetu
Katika enzi ya kidijitali, simu janja na mitandao ya kijamii vimekuwa sehemu ya maisha ya kila siku. Lakini pamoja na fursa zinazotolewa na teknolojia, wanawake na wasichana wengi wanakabiliwa na aina mpya ya ukatili unaofanyika kupitia majukwaa ya mtandaoni.
Takwimu za UNICEF zinaonesha kuwa kijana mmoja kati ya watatu duniani amewahi kukumbana na aina fulani ya unyanyasaji mtandaoni. Wataalamu wanaonya kuwa ukatili huu unaweza kusababisha hofu, msongo wa mawazo, kushuka kwa kujiamini, kujitenga na jamii, kushuka kwa ufaulu shuleni na hata mawazo ya kujidhuru.
Ni changamoto hiyo inayoshughulikiwa kupitia Mradi wa Sauti Zetu (Our Voices) unaotekelezwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ). Mradi huu unatumia nguvu ya vyombo vya habari kuhamasisha jamii kupinga ukatili wa kijinsia na kuwapa waathirika nafasi ya kusikika.
Katika mikutano ya jamii iliyofanyika mkoani Tanga, wanawake, vijana, wanafunzi, walimu na viongozi wa jamii walieleza namna ukatili wa kijinsia, hususan unaofanyika mtandaoni, unavyoathiri maisha ya wanawake na wasichana.
Mwanafunzi mmoja aliyeshiriki mjadala huo alisema vijana wengi hutumia muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii lakini hawajui wapi pa kupata msaada wanapokumbana na vitendo vya unyanyasaji.
“Wakati mwingine mtu anatukanwa, kutishiwa au kudhalilishwa mtandaoni lakini anaogopa kusema. Tunahitaji elimu zaidi kuhusu usalama wa kidijitali na namna ya kujilinda,” alisema.
Walimu walioshiriki katika majadiliano hayo walibainisha kuwa baadhi ya wanafunzi wanaokumbwa na unyanyasaji mtandaoni huathirika kisaikolojia, hupoteza kujiamini na wakati mwingine hujitenga na wenzao au kushuka kitaaluma.
Mama mmoja kutoka Tanga alieleza kuwa wanawake wengi huogopa kuripoti vitendo vya ukatili kutokana na hofu ya kuaibishwa au kutokuaminiwa na jamii.
“Wanawake wengi wananyamaza kwa sababu wanaogopa kulaumiwa au kuchekwa. Tunahitaji jamii inayowaunga mkono waathirika badala ya kuwahukumu,” alisema.
Akizungumza wakati wa moja ya vikao vya ushirikishwaji wa jamii, mwakilishi wa TAMWA, Sylvia Daulinge, alisema ukatili wa mtandaoni una madhara makubwa yanayoathiri maisha halisi ya watu.
“Ukatili wa mtandaoni si jambo la mtandaoni pekee; una madhara halisi. Waathirika hupitia hofu, msongo wa mawazo, kuharibiwa sifa zao na kupoteza fursa mbalimbali. Lengo letu ni kuhakikisha wanawake na wasichana wanatumia nafasi za kidijitali kwa usalama na bila hofu,” alisema.
Kupitia vipindi vya redio, midahalo ya jamii na kampeni za uelimishaji, Mradi wa Sauti Zetu unaendelea kuwafikia wananchi kwa ujumbe wa kupinga ukatili wa kijinsia na kuhamasisha matumizi salama ya teknolojia.
Aidha, mradi unahamasisha wananchi kuripoti matukio ya ukatili, kutafuta msaada kwa wakati na kushiriki katika kujenga jamii inayoheshimu haki na usalama wa wanawake na wasichana.
Kadri matumizi ya intaneti na mitandao ya kijamii yanavyozidi kuongezeka nchini Tanzania, wadau wanaamini kuwa elimu ya usalama wa kidijitali na juhudi za kupinga ukatili wa kijinsia zinapaswa kwenda sambamba ili kuhakikisha maendeleo ya teknolojia hayaachi nyuma usalama na ustawi wa jamii.
Akizungumza kuhusu umuhimu wa Mwongozo wa Kukabiliana na Ukatili wa Kijinsia Mtandaoni (OGBV Toolkit), Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dkt. Rose Reuben, alisema teknolojia inapaswa kuwa chombo cha maendeleo na si chanzo cha hofu kwa wanawake na wasichana.
“Sauti za wanawake na wasichana hazipaswi kunyamazishwa na hofu ya ukatili wa mtandaoni. Kupitia OGBV Toolkit, tunawapa maarifa na zana za kujilinda, kuripoti ukatili na kudai haki zao katika ulimwengu wa kidijitali,” alisema Dkt. Rose Reuben, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA.
Kadri Tanzania inavyozidi kuingia katika ulimwengu wa kidijitali, changamoto za ukatili wa kijinsia nazo zinaendelea kubadilika sura. Hata hivyo, kupitia juhudi za pamoja za jamii, vyombo vya habari, serikali na wadau wa maendeleo, kuna matumaini kwamba wanawake na wasichana wataendelea kupata sauti, kupata ulinzi na nafasi salama za kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Pamoja na vyombo vya Habari, kadhalika viongozi wa sekta ya elimu nao wameonyesha kujitoa katika kupaza sauti dhidi ya ukatili wa kijinsia. Ofisa Elimu Wilaya ya Bahi, Boniface Wilson, akizungumza katika mdahalo wa kielimu kuhusu ukatili wa kijinsia alisema, wanaume wanatakiwa kusimama na kuzungumza kuhusu ukatili wa kijinsia.
“Wanaume tukisimama, kulisemea suala la ukatili wa tutaweza kutokoeza ukatili dhidi ya Watoto na wanawake” Wilson.
Kadhalika, Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Polisi ambae pia ni Mkuu wa Dawati la Jinsia, Dodoma, Christa Kayombo, alizungumza na wanawake katika mdahalo wa kielimu wa ukatili wa kijinsia kwa wanawake, Dodoma na kuhimiza wanawake nao wapaze sauti wanapofanyiwa ukatili wa kijinsia.
“Kuna kesi tunazipokea za wanawake wanafanyiwa ukatili wa kijinsia lakini unapotaka kuwaisaidia wao wenyewe baadaye wanaomba kesi ifutwe, kisa wanaona mume au mwenza akifungwa ataathirika kiuchumi,” alisema Afande Kayombo
Kupitia Mradi wa Sauti Zetu, TAMWA na GIZ wanaendelea kuthibitisha kuwa mabadiliko yanaanza pale jamii inapothubutu kuzungumza. Kila sauti inayopazwa dhidi ya ukatili, kila simulizi inayosikika na kila hatua inayochukuliwa kumlinda mwanamke au msichana, ni hatua moja mbele kuelekea Tanzania yenye usawa, heshima na usalama kwa wote kwa mujibu wa Dira 2050.
