
Kundi kubwa na lenye nguvu zaidi ya kisiasa ndani ya Bunge la Umoja wa Ulaya (The EPP Group) limependekeza jina la Tundu Lissu, kuwania Tuzo ya Sakharov 2026.
Lissu ameteuliwa kuwania tuzo hiyo na bunge la Ulaya (EPP Group) lenye wabunge 184 kutoka nchi za EU.
Kwa mujibu wa Kundi la EPP, suala laLissu linaakisi hali pana ya kudhoofika kwa demokrasia ya vyama vingi, ushindani wa kisiasa na uhuru wa kisiasa nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa EPP, Lissu anawakilisha mchanganyiko wa ujasiri binafsi, msimamo wa kidemokrasia na umuhimu wa kisiasa katika mahusiano ya kimataifa. Uteuzi wake unaonyesha msimamo wa Ulaya wa kuwaunga mkono watu wanaotetea demokrasia ya kikatiba na uhuru wa kisiasa barani Afrika na katika nchi nyingine washirika wa Umoja wa Ulaya.
Lissu anaelezwa kuwa mfano wa utetezi wa demokrasia, siasa za vyama vingi, utawala wa sheria na uhuru wa msingi wa binadamu, akifanya hivyo kwa gharama kubwa binafsi.
Mshindi wa tuzo hii hukabidhiwa cheti cha heshima (diploma) pamoja na zawadi ya fedha taslimu kiasi cha Euro 50,000 (sawa na takriban shilingi milioni 150+ za Kitanzania), na hafla ya kukabidhi tuzo hii hufanyika mwezi Desemba kila mwaka, katika ofisi za Bunge la Ulaya mjini Strasbourg, Ufaransa.
Miongoni mwa waliowahi kupata tuzo hii ni aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, Mwanaharakati Malala Yousofzai na Nadia Murad (Mwanaharakati wa Haki za Binadamu wa Iraq).
Tuzo hii ilianzishwa mwaka 1988 na kupewa jina la mwanasayansi na mpigania haki za binadamu wa Urusi, Andrei Sakharov.
