Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila
Wino Tanzania, Reporter
Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Afrika50, na Jukwaa la Miundombinu Afrika(Infra for Africa Forum 2026) unatarajia kukusanya washiriki zaidi ya 12,000 kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika pamoja na viongozi wa taasisi za kifedha, wa serikali na wawekezaji.
Hayo yameelezwa leo na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila, wakati alipozungumza na wanahabari kuelekea mkutano huo kesho August 4.
Chalamila amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ndiye atakayekuwa mwenyeji wa kuwapokea viongozi mbalimbali watakaoshiriki mkutano huo, unaolenga kuimarisha ushirikiano wa Afrika katika uwekezaji na maendeleo ya miundombinu.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ndiye atakayekuwa mwenyeji wa kuwapokea viongozi wa mataifa mbalimbali watakaoshiriki mkutano huu muhimu kwa maendeleo ya Bara la Afrika,” amesema Chalamila.
Ameongeza kuwa miongoni mwa viongozi wanaotarajiwa kushiriki ni Marais wa Angola, Kenya, Msumbiji, Senegal na Nigeria, huku akibainisha kuwa jukwaa hilo litatoa nafasi ya kujadili masuala muhimu yanayohusu maendeleo ya miundombinu, biashara na uwekezaji pamoja na kutafuta suluhisho la changamoto zinazoikabili Afrika.
Mbali na mijadala hiyo, washiriki watapata fursa ya kubadilishana uzoefu, kujenga ushirikiano mpya wa kibiashara na kuainisha mikakati ya kuongeza mtaji kwa ajili ya utekelezaji wa miradi yenye tija katika sekta ya miundombinu.
