
Kauli za Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba kuhusu vurugu za uchaguzi wa Oktoba 29, 2025, sio tu zinatosha vidonda na maumivu ya Watanzania, bali pia ni ishara kwamba hakutakuwa na maridhiano ya dhati kama ambavyo Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akiahidi.
Dk Mwigulu amesikika katika ziara zake maeneo mbalimbali nchini, akirejea vurugu zile na kutupa lawama kwa wanaharakati wanaoishi nje ya nchi kuwa ndio wamehusika. Amelaumu pia vyama vya upinzani na mataifa ya nje kwamba yanaionea gere Tanzania kutokana na utajiri wa madini na rasilimali nyinginezo.
Bahati nzuri Serikali yenyewe imekiri mara kadhaa kuwa yalitokea mauaji na watu kujeruhiwa na mali kuharibiwa, lakini swali linabaki kuwa, hao wanaharakati ndio walishika bunduki wakaua na kujeruhi wananchi? Hayo mataifa ndio yalipambana na waandamanaji wakafa? Hao wapinzani ndio wameua?
Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na shirika la Amnesty International Desemba 19, 2025, ni kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vilitumia nguvu kubwa iliyosababisha mauaji na majeruhi bila sababu za msingi.
Lakini akizungumza na wazee wa Dar es Salaam, Desemba 2, Rais Samia Suluhu Hassan alisema nguvu iliyotumika ilistahili, kwani kama waandamanaji wangeachwa, wangeweza kuipindua serikali yake. Kwa maana nyingine, Rais Samia amehalalisha mauaji na majeruhi yale kwa lengo la kuilinda Serikali yake.
Turudi kwenye msingi wa malalamiko ya Dk Mwigulu kwamba wanaharakati na mataifa ya nje yanahusika. Ni kwamba, vyovyote itakavyokuwa, Jeshi la polisi linalodhibiti ghasia lina taaluma ya kudhibiti maandamano bila kuua, kwa kutumia mabomu ya machozi na hata risasi za moto lakini bila kuua. Kwa maana nyingine, ingewezekana kudhibiti maandamano yale bila kuua mtu.
Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) na Kanuni za Jeshi la Polisi (PGO) zinaelekeza matumizi ya nguvu kwa polisi pindi wanapokabiliana na vurugu au ukamataji au mashambulio. Nguvu inapaswa kuwa sawa na ile anayokabiliana nayo.
Haya sasa, mauaji yametokea, lakini Serikali haitaki kusema wamekufa watu wangapi. Dk Mwigulu amewalaumu wanaharakati wanaodai kuwa waliokufa ni watu 10,000, lakini hataki kusema idadi sahihi, maana yake nini? Nini kinafichwa?
Ukweli ni kwamba Serikali imeingia kwenye aibu kubwa, hali inayoiipa hofu ya kushitakiwa na hata kujikuta kwenye mtego wa kuwajibishwa kimataifa, ndio maana idadi ya vifo inafichwa.
Ni bahati mbaya sana, kuona Waziri Mkuu Mwigulu anatumia muda mwingi kurejea vurugu zile, wakati hawezi kujibu maswali ya msingi likiwemo la idadi ya vifo. Isitoshe, ni wakati huu ambao, Tume iliyoundwa na Rais Samia ya kuchunguza uvunjifu wa Amani kabla na baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, inaendelea na kazi yake.
Japo tume yenyewe haiaminiki kwa kuwa imeundwa na upande ambao pia unalalamikiwa, lakini kwa nini Waziri Mkuu Mwigulu asiiche hiyo tume ichunguze yaliyotokea ije na majibu yake? Hii inathibitisha Zaidi kuwa tume hiyo si lolote si chochote, kwani hata ikija kuleta matokeo, viongozi wa Serikali watataka yawe sawa na matakwa yao.
Tulitarajia Waziri Mkuu Mwigulu angejikita kuzungumzia kero za wananchi, kwa mfano hapa Dar es Salaam kuna shida ya maji, angejikita huko.
Kuna shida za barabara, kuna shida za masoko, wakulima hawana pembejeo, migogoro ya ardhi na matatizo chungu nzima. Waziri Mkuu angejikita huko, sio kupiga mipasho kwenye mambo yanayochunguzwa na tume.
Kwa kuwa Waziri Mkuu Dk Mwingi anaendelea na kauli zake kwa mambo yanayochunguzwa na tume, ni wazi kuwa, kwanza Serikali haitaki kukiri makosa iliyofanya, bali inatafuta mchawi wa kumbebesha lawama.
Pili, kuna dalili kuwa Serikali haitaki maridhiano na wapinzani au makundi mengine ya watu wanaoilalamikia mfumo wa demokrasia ya vyama vingi.
Kwa maana hiyo, hicho kinachoitwa maridhiano ni kiini macho tu, hakitakuja kutokea. Hata huo mchakato wa mabadiliko ya Katiba ulioahidiwa ndani ya siku 100, hatuutarajii kwa sababu hakuna dhamira ya dhati.
Kitakachofanyika badala yake ni kuendelea kuwalazimisha wananchi kuwa watiifu kwa Serikali kwa kisingizio cha kulinda amani.
