Florence Majani,
Ninaingia katika mtaa wa Mori, Sinza, wilaya ya Ubungo. Nauliza watu wawili, watatu, na ninaelekezwa mahali anapoishi huyo ninayemtafuta.
Ni hatua chache kutoka ilipo hoteli ya Wanyama, mtaa wa Mamba, nyumba na 16 na hapo ndipo anapoishi ninayemtafuta, na si mwingine bali ni mwanamuziki mkongwe na mahiri Hassan Rehani Bichuka.
Ninapofika hapa ninapokelewa na mke wake, Zainab Salum, pamoja na mtoto wa pili wa Bichuka, Salma Rehani Bichuka.
Kilichotuleta hapa ni kuzungumza na Bichuka, ili kujikumbusha, kufahamu safari yake ya kimuziki, mafanikio, changamoto na alipo hivi sasa kimuziki.
Kwa bahati mbaya, tunapofika hapa kutaka kuyajua hayo yote kutoka kwake, tunaambiwa kuwa, Bichuka hakumbuki chochote, kwani kwa sasa anaishi na maradhi ya kupoteza kumbukumbu kitaalamu ‘Alzheimer’.
Hata hivyo Mke wake, Zainab Salum, anatueleza kwa ufupi historia yake ya kimuziki. Mwanamuziki huyu mkongwe, naambiwa amewahi kuimba katika bendi maarufu za zamani ikiwamo OTTU Jazz, Sikinde, Nationale na JUWATA.
“Safari yake ameianza kabla hata hajanioa, akiwa Arusha,akiwa katika bendi inayoitwa Nationale, baadaye akajiunga na NUTA JAZZ, na kisha akajiunga na bendi ya Mlimani Park, Ndekule na baadaye akarudi Juwata,” anasema
Zainab anasema Bichuka amefanya kazi na bendi nyingine ikiwamo OTTU JAZZ na Sikinde, lakini kabla hajaanza kuimba muziki rasmi, alikuwa kiongozi mzuri wa nyimbo katika shule ya elimu ya dini ya kiislamu, au madrasa.
Bi Zainab anakumbuka baadhi ya nyimbo ambazo Bichuka mwenyewe alizipenda, wakati mwingine, anaimba baadhi ya mistari.
“Mume wangu nyimbo zake ni nyingi, kwa mfano, kaka Selemani, Mpenzi Zarina, na Imba,” anasema
Hata hivyo, anasema maisha ya kimuziki ya Bichuka hayakumpa kipato cha kujipatia utajiri zaidi ya sifa za mdomo, kufahamika kwamba huyu ni mke wa Bichuka na hawa ni watoto pia.
“Tunashukuru tumepata sehemu ya kukaa lakini si zaidi ya hapo” anasema na kuongeza:
“Zipo baadhi ya taasisi zimetambua mchango wake na kumpa tuzo, kama ile pale ya Kilimanjaro aliipata mwaka 2009.”
Nahamisha mazungumzo yetu kwa Salma Hassan Bichuka, mtoto wa pili wa Bichuka, na yeye anasema baba yake alibahatika kupata watoto wanne, Salum, Masoud, Mwanaidi na yeye Salma.
Anasema licha ya kuwa baba yao, alikuwa mwanamuziki hodari lakini hakuna mtoto wake hata mmoja hakuna aliyefuata nyayo zake. Lakini yeye angalau alitamani kujaribu muziki.
“Miaka ya nyuma niliwahi kujaribu kuimba, nilienda nikafanya mazoezi na Didah Mashamsham, (marehemu Didah Shaibu)nikashiriki katika uzinduzi wa albamu ya muziki lakini Mzee alipojua alinizuia,” anasema
Salma anasema alikuwa anapenda kuimba na kucheza lakini baba yake alimkataza akimweleza kuwa maisha ya muziki ni magumu.
Hata hivyo, Salma anasema alipenda kazi za baba yake, tangu akiwa mdogo na alizishika kwa wepesi nyimbo zake.
Huku akiuimba wimbo wa ‘Dada Rehema’ Salma anaeleza nyimbo za baba yake zinamkumbusha mbali.
“Nyimbo za mzee zote nazipenda, lakini hakupenda niwe mwanamuziki kama yeye,” anasema
Wakati Salma akiimba wimbo wa ‘Dada Rehema’, baba yake aliyekuwa amekaa katika upande wa pili wa sebule, anasikika akisema.
“Sipendi kabisa Watoto wangu wafanye muziki,aa…hapana… nilikataa, sipendi tu…”
Hata hivyo katika mazungumzo haya yote ya furaha yanayoikumbusha familia hii mbali, ni mengi ambayo Bichuka hayakumbuki kutokana na maradhi yaliyompata.
Mke wake, Zainab anasimulia chanzo cha maradhi ya mume wake na kusema hapo awali, alianza kuumwa ugonjwa wa kisukari, shinikizo la damu na macho na baadaye taratibu akaanza kupoteza kumbukumbu.
“Tulitibu sukari na ‘pressure’ lakini wakati anapona hayo magonjwa, baadaye tukaanza kuona tatizo la kupoteza kumbukumbu linakuwa kubwa,” anasema na kuongeza:
“Daktari amesema tatizo lipo kwenye ubongo, madaktari wanavyosema ataendelea kutumia dawa kwa muda mrefu.”
Ni kweli, Bichuka hakumbuki vingi. Hapa ninamuuliza ni nyimbo yake ipi, anayoweza kuniimbia, na anasema hakumbuki chochote.
Lakini ghafla anaukumbuka wimbo huu na kuanza kuimba:
“Unanisengenya bure, bwana ooh, aeeh unaniteta na kunicheka, eeh na wala sijali tena hofu, mwisho wake utacheka… kila nipitapo unakereka na kusononeka lipi nilokuudhi,” anaimba Bichuka huku akisaidiwa na mke wake na mtoto wake Salma.
Mke wake, Zainab anapotumia mbinu kadhaa kumkumbusha anatuimbia wimbo wake mwingine wa Iba.
Kwa ustadi, na sauti yake ya kipekee Bichuka anaimba wimbo wa Iba.
“Iba nimelibeba pendo lako kama mwana na mbeleko, Iba ooh Iba, imekuwaje Iba, Iba ooh Iba, niende mbele oooh…”
Kuhusu wanamuziki wenzake, aliowahi kufanya nao kazi katika bendi yake ya Sikinde, OTTU, na nyinginezo Bichuka anasema
“Naona kama vile hawaji kunitazama, lakini jana kwenye msiba wa King Kiki, waliniona, wakajifanya rafiki zangu, lakini sio wa kweli…” anasema
Pamoja na kupoteza kumbukumbu kwa kiasi kikubwa lakini Bichuka alikuwa na neno la kumwambia Waziri wa sasa wa Utamaduni, Sanaa na Michezo.
“Mzee nakwambia hivi, mimi mpaka hivi sasa, ninakupenda sana, lakini wewe naona kama hunipendi, wewe naona kama hunipendi, nimekaa nyumbani sikuoni…” anasema
Ninapomuuliza kuhusu nyimbo zake zenye mchango kwa serikali wakati ule mara tu baada ya uhuru, Bichuka anasema anachokumbuka ni kuwa alikuwa akizitunga na kuziimba lakini kwa sasa amezisahau zote.
“Mi nasahau, hata nikiulizwa, kila kitu …” anasema
Kuhusu maradhi haya ya kusahau mke wake, Zainab anasema alianza kuyaona miaka ya nyuma ambapo Bichuka alikuwa akisahau vitu vidogo vidogo, lakini awali ilidhaniwa kuwa hali ya kawaida.
“Alikuwa anasahau baadhi ya ndugu wa karibu waliokuwa wakija nyumbani, tukawa tunadhani labda ubize na mambo mengi, lakini baadaye hali ilivyokuwa mbaya tukakumbuka kumbe tatizo lilianza zamani,” anasema
Salum Bichuka, mtoto wa kwanza wa Rehani Bichuka, anaeleza historia ya Rehani Bichuka.
Anasema alizaliwa Desemba Mosi, 1950, eneo la Kigoma Ujiji. Awali kipaji chake kilianzia kwenye soka, ambapo alicheza nambari mbili, timu ya Breweries, Arusha.
“Baadaye alikutana na Said Mabela, mpiga gitaa la Solo wa bendi ya Msondo, ambaye akigundua kipaji chake cha kuimba hasa akivutiwa na sauti yake mfano wa kinanda,” anasema
Baadaye, Bichuka alijiunga na bendi ya OSS Safari Sound, iliyokuwa ikimilikiwa na Hugo Kisima.
Salum anasema, kupitia sanaa yake ya muziki, baba yake amewahi kuandikwa katika kitabu cha Chuo Kikuu cha Florida kilichopewa jina la The Legends of Tanzanians Musicians( Wakonhgwe wa Muziki Tanzania) kilichoandikwa na Frank Goodson.
Salum anamtaja baba yake kuwa, mwislamu safi, na miongoni mwa wanamuziki wachache wasiokunywa pombe wala kuvuta sigara.
“Wanamuziki wenzake walikuwa wanamwita mshamba, lakini katika muziki wake siku zote ametunza heshima yake, na ana mke mmoja na sisi Watoto wake wanne,” anasema na anaongeza:
“Mzee alikataa sisi tuimbe, mimi nilishaanza kujiingiza kwenye muziki, alikataa.”
Kupoteza kumbukumbu
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ubongo na Mishipa ya Fahamu, kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Mnacho Mohamed, amesema magonjwa ya kupoteza kumbukumbu yamegawanyika katika sehemu, mbili, ugonjwa unaosababishwa na kufa kwa seli zinazotunza kumbukumbu katika ubongo, kutokana na protini katika eneo hilo kwisha, kitaalamu Alzheimer.
“Kundi la pili katika maradhi haya ni dementia, ambao husababisha mtu kupoteza kumbukumbu kutokana na aina ya magonjwa ikiwamo, ajali, kisukari, kiharusi, kifafa,” amesema
