
Serikali ya Tanzania imefungua rasmi Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi, unaolenga kujadili ulinzi wa mazingira ya bahari na maeneo ya pwani katika ukanda wa Bahari ya Hindi Magharibi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Oktoba 6, 2026, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhandisi Hamad Masauni, amesema Tanzania inajivunia kuwa mwenyeji wa mkutano huo unaowakutanisha zaidi ya wajumbe 500 kutoka nchi za ukanda huo na washirika wa kimataifa.
Masauni amesema mkutano huo pia unaadhimisha miaka 40 tangu kupitishwa kwa Mkataba wa Nairobi mwaka 1985. Amesema mkataba huo umeendelea kuwa mfumo muhimu wa kikanda katika usimamizi wa mazingira ya bahari na pwani, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa nchi wanachama.
Kwa mujibu wa Waziri Masauni, mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la joto na tindikali baharini, uchafuzi wa plastiki, uvuvi usio endelevu na uharibifu wa makazi ya viumbe vya baharini ni miongoni mwa changamoto zinazohitaji hatua za pamoja katika ukanda wa Bahari ya Hindi Magharibi.

Amesema Tanzania, katika kipindi cha uongozi wake, imesimamia hatua mbalimbali zikiwamo kukamilishwa kwa Itifaki ya Bioanuwai za Bahari na Pwani pamoja na Maeneo Yanayolindwa, Mpango wa Kikanda wa Kukabiliana na Mafuta Baharini na Mkakati wa Kikanda wa Plastiki na Kemikali Zinazohusiana nayo.
Masauni pia amewataka wajumbe kuhakikisha ripoti zinazojadiliwa zinazingatia ushahidi, huku maamuzi yatakayopitishwa yakiwa machache, yanayoeleweka na yanayotekelezeka. Pia amesisitiza umuhimu wa kuunganisha uhifadhi wa mazingira na maisha ya wananchi, usalama wa chakula, miundombinu yenye ustahimilivu na uchumi wa buluu.
Aidha, amewataka washiriki kuzingatia ushirikishwaji wa jamii za pwani, wanawake na vijana katika utungaji wa sera na uwekezaji unaohusu mazingira ya bahari. Amesema maamuzi ya Mkutano wa 12 yataathiri afya ya bahari na ustawi wa wananchi kwa miongo ijayo
