
Katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, ambapo shahidi wa tano ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, John Heche anaendelea kutoa ushahidi wake ikiwa ni siku ya tatu akijibu maswali ya mshitakiwa.
Katika maelezo yake leo Septemba 11, pamoja na mambo mengine, Heche amekanusha tuhuma kuwa Lissu ndiye aliyeitisha mkutano wa waandishi wa habari makao makuu ya CHADEMA Aprili 3, 2025.
Endelea…
Lissu: Tuhuma inadai mimi nilialika waandishi wa habari, wewe unasemaje?
Heche: Hiyo siyo kweli kwa sababu maandalizi ya mkutano huo yalifanywa chini ya Katibu Mkuu John Mnyika. Sisi hatukuwepo, tulikuwa ziarani.
Lissu: Waeleze majaji, hiyo siku ya tarehe 3 Aprili wewe ulikuwa wapi?
Heche: Mimi nilikuwa miongoni mwa wageni kwenye huo mkutano, na nilikuwa miongoni mwa waliopata nafasi ya kuzungumza kwenye huo mkutano.
Lissu: Waeleze majaji viongozi wengine waliokuwepo kwenye mkutano huo kwa kumbukumbu zako.
Heche: Nakumbuka alikuwepo Mwenyekiti wa Taifa wa chama Tundu Lissu, nilikuwepo mimi Makamu Mwenyekiti, alikuwepo Katibu Mkuu John Mnyika, alikuwepo Amani Golugwa, Naibu Katibu Mkuu Bara, alikuwepo Brenda Rupia, Mkurugenzi wa Habari, wakurugenzi wa chama kutoka makao makuu, Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani Boniphace Jacob pamoja na watia nia wenyewe.
Lissu: Waeleze waheshimiwa majaji, nje ya viongozi na watia nia, waeleze majaji uwepo wa watu wengine kwenye mkutano huo.
Heche: Walikuwepo waandishi wa habari.
Lissu: Waeleze waheshimiwa majaji, waandishi wa habari uliosema walikuwepo, walikuwa wangapi?
Heche: Siwezi kukumbuka idadi kamili, lakini nakumbuka walikuwa wengi kutoka vyombo mbalimbali.
Lissu: Waeleze waheshimiwa majaji hao waandishi wa habari walikuwa na nini?
Heche: Walikuwa na kamera, wengine walikuwa na kalamu na notebook na vinasa sauti.
Lissu: Waeleze waheshimiwa majaji, idadi ya watu wote waliokuwepo walikuwa wangapi?
Heche: Siwezi kuwa na uhakika wa namba, lakini ni zaidi ya watu 200.
Lissu: Waeleze majaji, huo mkutano ulifunguliwa na nani?
Heche: Ulifunguliwa na kiongozi wa sekretarieti, Katibu Mkuu.
Lissu: Waeleze majaji, baada ya Katibu Mkuu kufungua aliwakaribisha akina nani kuzungumza?
Heche: Alinikaribisha mimi. Mimi niliongea kwa muda kidogo na baadaye mimi ndiye nilimkaribisha Mwenyekiti.
Lissu: Mkutano wote kuanzia ufunguzi hadi mwisho, ulichukua muda gani?
Heche: Kwa ujumla yanaweza kuwa masaa manne na zaidi kidogo.
Lissu: Katika hayo masaa, mimi nilizungumza kwa muda gani?
Heche: Waheshimiwa majaji, Mwenyekiti wa chama cha Chadema alizungumza zaidi ya masaa mawili.
Lissu: Wanasema kitu kimoja sahihi hapa, wanasema mkutano huu unahamasisha uasi. Hayo maneno niliyosoma yamechukua muda gani?
Heche: Hayajamaliza hata dakika mbili.
Lissu: Waeleze waheshimiwa majaji, kimoja baada ya kingine, hayo mazungumzo marefu niliyofanya yalikuwa ni mambo gani?
Heche: Yalihusu namna ambavyo mfumo wetu wa uchaguzi umeharibika, hauwezeshi wananchi kupata viongozi wawatakao, ni mbovu, hauko huru, namna ambavyo ni vigumu kwa mgombea wa upinzani, hasa Chadema, kufanikiwa kushinda uchaguzi hata kama anakubalika, unavyosababisha maafa hasa ya uchaguzi, namna unavyoruhusu upendeleo wa wazi kwa wanachama wa CCM kuanzia Rais mpaka wenyeviti wa kata, namna ambavyo polisi wanatumika kuharibu uchaguzi, watumishi wa umma. Kwa ujumla alieleza namna ambavyo huu mfumo usivyo huru na hautendi haki na unavyopaswa kubadilishwa kabla ya uchaguzi mwingine wowote ule.
Lissu: Waeleze majaji nilisema nini juu ya kuondoa hayo mambo wakati wa uchaguzi?
Heche: Alisema namna hiyo ni kutengeneza mfumo ambao hauna upendeleo, ambao ni huru na wa haki, unaotoa usawa bila upendeleo.
Lissu: Waeleze waheshimiwa majaji kuhusu Tume ya Uchaguzi, nilisema nini juu ya mabadiliko yanayotakiwa?
Heche: Alisema kwamba mabadiliko yanayotakiwa kwenye tume ni kutengeneza muundo mpya wa tume, ambao haumpi mamlaka Mwenyekiti wa CCM na viongozi wa CCM kuunda tume. Iwe na watumishi wake wanaojitegemea, isiwe inaazima watumishi wa Serikali ambao wote hupokea maelekezo kutoka kwa mwajiri wao, na hiyo tume ndiyo iwe na mamlaka ya kugawa majimbo kulingana na vigezo vinavyofaa na si upendeleo.
Lissu: Waeleze waheshimiwa majaji, kwenye hotuba yangu nilisema nini kuhusu masuala ya kampeni?
Heche: Waheshimiwa majaji, alieleza kwa kutoa mifano namna ambavyo uchaguzi unavurugwa na vyombo vya dola, mfano polisi, tume yenyewe kwa kutumia Kamati ya Maadili, na hapa nitatoa mfano wa yeye alivyosimamishwa kufanya kampeni zake katika uchaguzi mkuu wa 2020.
Lissu: Waeleze majaji nilisema nini suala la kuenguliwa kwa wagombea wa upinzani, hasa wa Chadema?
Heche: Alieleza kwa urefu namna wagombea wa upinzani wanavyoenguliwa kwa sababu zisizo za sheria wala Katiba. Akaeleza kwamba kwenye uchaguzi wa 2020 ulivunja rekodi kwa wagombea wengi kuenguliwa na hivyo CCM kupita bila kupingwa, na akawa anatoa mfano kwamba hiyo inawanufaisha CCM kwani mgombea wao hajawahi kuenguliwa.
Lissu: Waeleze waheshimiwa majaji, nilisema nini kuhusu mawakala wa vyama na wagombea?
Heche: Alisema kwamba wakala anapaswa kuwa mwakilishi wa mgombea na chama chake, lakini sasa taratibu zimewekwa ngumu kwa mawakala kuingia kwenye vituo, kuanzia kuwaapisha mpaka kusimamia kura.
Lissu: Waeleze majaji nilichosema juu ya kupinga mambo yote haya mahakamani.
Heche: Alieleza namna ambavyo ni ngumu kupinga mambo haya mahakamani. Akaeleza hatua ambazo zimechukuliwa na watu mbalimbali kujaribu kupinga kupitia njia za mahakama, alieleza namna ambavyo hata ushahidi ambao ungetumika mahakamani unavyokuwa umeharibiwa tangu mwanzo. Akaeleza gharama kubwa ambazo zinatakiwa kutolewa na walalamikaji, kwa hiyo wanakuwa hawawezi. Akaeleza pia uwingi wa kesi ambazo zingefunguliwa, akasema katika mazingira hayo utafungua kesi ngapi. Akasema matatizo ya kisiasa yanatakiwa kutatuliwa kisiasa na siyo lazima yaende mahakamani.
Lissu: Mkutano wa tarehe 3 Aprili inadaiwa ulirushwa live kwenye televisheni. Waeleze waheshimiwa majaji ufahamu wako juu ya hilo.
Heche: Mimi nilikuwepo na nafahamu waandishi wa habari walikuwepo, lakini sifahamu kama ulikuwa live.
Lissu: Eleza kuhusu rekodi ya huo mkutano kurekodiwa kwenye mitandao ya kijamii, hasa Jambo TV.
Heche: Nafahamu kuhusu chanzo, Mwanzo na Jambo TV yenyewe.
Lissu: Hicho ulichokiona huko kina urefu wa muda gani?
Heche: Zinatofautiana, lakini kwenye Jambo ulikuwa masaa mawili, kwenye Mwanzo kipande kingine dakika 45, nyingine saa moja. Zilikuwa zinatofautiana.
Lissu: Waeleze majaji katika hizo YouTube channel ulizoziona, uwepo wa maneno haya, wanasema kitu kimoja sahihi hapa, wanasema hivi…
Heche: Hayo ni miongoni mwa maneno ambayo yapo, ndiyo.
Lissu: Waeleze majaji yale mengine uliyosema niliyazungumzia.
Heche: Mengine yote yapo, kwa hiyo ni hotuba ndefu ya maneno mengi.
Lissu: Shtaka nililoshtakiwa nalo la uhaini linasema mimi ndiye niliyerusha hayo matangazo na kuweka kwenye hiyo mitandao ya Jambo na mingine. Wewe unasemaje?
Heche: Hiyo siyo kweli, kwa sababu Mwenyekiti siyo mhariri wa hizo channel za YouTube.
Lissu: Waeleze majaji kuhusu mimi kugusa chochote cha waandishi wa habari.
Heche: Hakugusa chochote cha habari kama kamera na maiki na mengine.
Lissu: Wanasema hivi, “Msimamo huu unaashiria uasi.” Ni kweli? Waeleze majaji kwa ufahamu wako uwepo wa uasi kutokana na maneno haya kwenye Katiba hii.
Heche: Sina ufahamu wowote wa uwepo wa uasi kutokana na maneno hayo kwenye Katiba hii.
Lissu: Waeleze uwepo wa kosa la kuhamasisha uasi kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Heche: Sina ufahamu wowote kwenye Katiba hii juu ya kosa la kuhamasisha uasi.
Lissu: Waeleze kwa ufahamu wako, uwepo wa kosa linaloitwa kuvuruga uchaguzi kwenye Katiba hii.
Heche: Kwa ufahamu wangu hakuna kosa la kuvuruga uchaguzi kwenye Katiba hiyo anayoisema.
Lissu: Waeleze ufahamu wako kuhusu uwepo wa kosa la kuzuia uchaguzi kwenye Katiba hii.
Heche: Kwa ufahamu wangu hakuna kosa la kuzuia uchaguzi kwenye Katiba ya mwaka 1977.
Lissu: Waeleze kwa ufahamu wako uwepo wa kosa la kuhamasisha watu kuzuia uchaguzi kwenye Katiba hii.
Heche: Kwa ufahamu wangu hakuna kosa la kuzuia uchaguzi kwenye Katiba hii.
Lissu: Waeleze waheshimiwa majaji, kwa ufahamu wako uwepo wa kosa la kukinukisha kwenye Katiba hii.
Heche: Kwa ufahamu wangu hakuna kosa la kukinukisha kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Lissu: Waeleze majaji kwa ufahamu wako uwepo wa kosa linaloitwa kuzuia watu kwenda kupiga kura kwenye Katiba hii.
Heche: Sijawahi kuona na sifahamu kama kuna hilo kosa kwenye Katiba.
Lissu: Waeleze waheshimiwa majaji kwa ufahamu wako uwepo wa kosa la uasi kwa Kanuni ya Adhabu.
Heche: Sina ufahamu huo wa kosa la uasi.
Lissu: Waeleze waheshimiwa majaji kwa ufahamu wako uwepo wa kosa la kuhamasisha uasi kwenye Penal Code.
Heche: Sina ufahamu huo.
Lissu: Waeleze ufahamu wako kuhusu kosa la kuvuruga uchaguzi kwenye sheria hii, Kanuni ya Adhabu.
Heche: Sina ufahamu huo.
Lissu: Waeleze majaji uwepo wa kosa la kutengeneza nia ya kuzuia uchaguzi kwenye Kanuni ya Adhabu.
Heche: Sina ufahamu huo.
Lissu: Waeleze majaji uwepo wa maneno yaliyotaja Rais, Makamu wa Rais, Waziri, majeshi ya ulinzi, polisi, mgambo, Jeshi la Akiba na mengine kwenye hotuba yangu ya Aprili.
Heche: Hakuna maneno yaliyowapata hao.
Lissu: Sasa maneno niliyoyataja, akayataja tena yamekuwa nani? Kwa ufahamu wako, hayajamtishia mtu?
Heche: Waheshimiwa majaji, kwa ufahamu wangu, hayajamtishia mtu.
