
Joseph Gervas, Wino Tanzania
Katika jamii ya Tanzania kumekuwa na imani juu ya uwepo wa nguvu za kishirikina zinazofahamika kama “Chuma Ulete” maeneo ya biashara, hasa kwenye maduka makubwa na madogo. Imani hii mara nyingi inahusishwa na upotevu wa fedha za wafanyabiashara au wanunuzi katika mazingira ya kutatanisha na yasiyoelezeka.
Soko Kuu la Kariakoo lililopo jijini Dar es Salaam, likiwa kitovu kikuu cha biashara ndani na nje ya nchi, linasifika kwa mwingiliano mkubwa wa watu na mzunguko mkubwa wa fedha kila siku. Hali hii inalifanya soko hili kutajwa kama moja ya maeneo yenye chuma ulete.
Kutokana na dhana hiyo, mnamo Juni 15, 2026, Wino Tanzania ilifika sokoni hapo na kufanya mahojiano na baadhi ya wafanyabiashara. Lengo kuu likiwa ni kufahamu kama imani ya uwepo wa chuma ulete katika Soko la Kariakoo ina ukweli wowote wa kiuhalisia au ni dhana tu za kufikirika.
Katika mahojiano hayo baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa na maoni tofauti. Mmoja wa wafanyabiashara aliyeomba uhifadhiwa jina lake, alisema licha ya kufanya kazi Kariakoo kwa muda mrefu, hajawahi kukumbana na changamoto hiyo.
Ingawa amekuwa akisikia kuwa watu wanaoomba chenji ndio wanaohusishwa na suala hilo, yeye binafsi huwa hatoi nafasi ya hofu na hutoa chenji kama kawaida kwa sababu hana imani na ya chuma ulete.
”Huwa ninasikia tu kwamba kuna chuma ulete lakini huwa siamini kama hicho kitu kipo. Watu wanadai kwamba ukiomba chenji ndiyo chuma ulete, lakini mimi huwa nawapa chenji. Kwa imani yangu ya dini, hilo jambo halipo,” alieleza.
Mbali na maeneo ya biashara, maeneo yenye mkusanyiko mkubwa wa watu kama vile vituo vikuu na vidogo vya mabasi nayo yanatajwa kuhusishwa na imani hii.
Katika maeneo hayo, mbinu ya watu kuomba au kutafuta chenji inatajwa zaidi na wengi kama ishara ya chuma ulete.
Mfanyabiashara mwingine sokoni hapo alibainisha kuwa, ingawa hajawahi kukumbana na hali hiyo moja kwa moja, anaamini kuwa suala hilo lipo kutokana na ushuhuda wa watu wake wa karibu. Alieleza kuwa ameshuhudia malalamiko kadhaa kutoka kwa marafiki waliopoteza fedha zao kimiujiza baada ya kupiga mahesabu na kubaini upungufu wa fedha ambazo awali zilikuwepo.
”Wapo ndugu na marafiki wanaongelea kwamba jana kaweka kiasi fulani leo anakuta hakipo, au kinapotea katika mazingira ambayo hayaelewi. Wakati alipiga mahesabu yakaenda sawa, akirudia tena mahesabu anakuta hayako sawa… kwa hiyo vipo,” alisisitiza mfanyabiashara huyo.
Naye Theofrida Timoth, ambaye ni mfanyabiashara wa nguo za wanawake na watoto Kariakoo, anaamini kuwa suala la chuma ulete linategemea kile ambacho mtu amekubali kukiamini moyoni mwake, na amesisitiza kuwa ukiwa na misingi mizuri ya kidini, mambo hayo hayawezi kukudhuru.
”Kwa suala la chuma ulete ni vile wewe mwenyewe utakavyojijengea, na ukiwa na Yesu huwezi kuona chuma ulete. Ni imani vile utakavyojijengea ndicho utakachokipata lakini chuma ulete hakuna,” alisema Theofrida Timoth, huku akiongeza kuwa katika muda wake wote wa biashara hajawahi kuona mambo hayo.
Msimamo huo ni tofauti na wa mfanyabiashara mwingine aliyedai kuwa chuma ulete ipo na inatumiwa na baadhi ya watu wenye imani hiyo ili kujipatia mitaji kirahisi.
Alitoa mfano wa namna ambavyo mtu anaweza kuomba chenji ya fedha, lakini baada ya kupewa, yule aliyetoa chenji anajikuta akibakiwa na kiasi kidogo cha fedha tofauti na hesabu halisi, maoni hake yaliwiana na mfanyabiashara wa mwanzoni.
”Ili ujue kuwa chuma ulete ipo, wewe nenda sehemu ya mkusanyiko wa biashara ukawa hata na elfu tano yako uombe chenji. Hata kama anayo anaweza kukwambia sina, yaani kuna uwezekano mdogo sana wa kupata chenji kwa mtu asiyekujua kwa sababu anajua ni nia ya chuma ulete. Unajua mjini kuna akili nyingi, watu wanatumia hiyo chuma ulete kwa ajili ya kupata mitaji mingine,” alieleza.
Kama namna ya kujihami, mfanyabiashara huyo ametaja mbinu wanazotumia baadhi ya watu kulinda fedha zao kutokana na imani hiyo ya chuma ulete, ikiwemo kuchanganya fedha na tunda pori linaloitwa Tulatula.
Tunda hilo linalofanana na nyanya chungu, linaaminika kuwa na uwezo wa kuzuia upotevu wa fedha katika mazingira ya kutatanisha.
”Wafanyabiashara wengi mauzo yao wanapouza unakuta wanaweka tulatula. Mimi nimewahi kushuhudia sehemu moja hivi soko la Bonanza la samaki, kuna huyo mfanyabiashara sisi tulikuwa tunawahi asubuhi kushusha mzigo. Nilishuhudia amewahi sana halafu alikuwa na chupa ya maji na ilikuwa siyo kawaida yake, yale maji kamimina kwenye kitambaa cheusi kafuta pale mezani. Kwa hiyo ukiona vile unajua hayo ni mambo ya kishirikina na huyo ni chuma ulete,” alisimulia kwa kirefu.
Lcha ya mgawanyiko wa mitazamo kati ya wanaomini na wasioamini uwepo wa chuma ulete, pande zote mbili kupitia maelezo tao zimeonesha mwelekeo mmoja kwani kwa nyakati tofauti wote walihitimisha kwa kusema kuwa imani hizo hazitakiwi katika maeneo ya biashara
