
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezihimiza nchi zilizoendelea na wadau wa kimataifa kuhakikisha Mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP31 unakuwa hatua ya mabadiliko halisi kutoka kwenye ahadi kwenda kwenye utekelezaji wa vitendo na matokeo yanayopimika.
Rais Samia ameeleza hayo Novemba 11, 2026 wakati akihutubia mkutano huo uliofanyika jijini Antalya, nchini Uturuki. Rais Samia amebainisha kuwa Tanzania kama zilivyo nchi nyingine zinazoendelea inaendelea kukabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ukame wa muda mrefu, mabadiliko yasiyotabirika ya msimu wa mvua, na kupanda kwa kina cha bahari.
Athari hizo za kiuchumi na kimazingira amesema zinakadiriwa kuigharimu nchi takriban asilimia 2 hadi 3 ya Pato la Taifa (GDP) kila mwaka, jambo linalofanya hatua za haraka na za haki za kimataifa kuwa za lazima.
Katika hotuba yake, Rais Samia amesisitiza kuwa hatua zote za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi lazima zizingatie haki ya mazingira, usawa, na kanuni ya majukumu ya pamoja lakini yaliyotofautiana kulingana na uwezo wa kila nchi.
Ili kufikia azma hiyo, ameeleza vipaumbele vitatu vikuu ambavyo Tanzania inavipa kipaumbele katika ushirikiano wa kimataifa. Kipaumbele cha kwanza amesema ni upatikanaji wa fedha za uhakika, zinazotabirika, na rahisi kupatikana, hususan kupitia misaada na mikopo nafuu kwa ajili ya kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi, pamoja na uhamishaji wa teknolojia na ujuzi.
Rais ameeleza kuwa Tanzania ina fursa kubwa za biashara ya hewa ukaa kupitia sekta za usafirishaji, usimamizi wa taka, nishati mbadala, na hekta milioni 48.1 za misitu, hivyo akataka utekelezaji wa Ibara ya 6 ya Mkataba wa Paris ulenge kuhakikisha bei ya haki ya hewa ukaa na ugawaji wa faida unaozingatia mazingira na jamii za mitaa.
Kipaumbele cha pili amesema kinajikita katika haki ya nishati na upatikanaji wa nishati safi, ambapo Rais ameeleza kuwa mchakato wa dunia kuelekea nishati safi lazima uzingatie mazingira na mahitaji ya maendeleo ya nchi za Afrika ili kuhakikisha kila mwananchi anapata nishati ya bei nafuu, ya uhakika, na endelevu. Amesema Tanzania inaendelea kutekeleza Mfumo wake wa Nishati ili kusambaza umeme kote nchini, hususan maeneo ya vijijini.
Kipaumbele cha tatu Rais Samia amesema kinahusu uwekezaji kwa vijana na maendeleo yanayostahimili mabadiliko ya tabianchi kupitia ubunifu, viwanda, na uchumi endelevu. Amesema Tanzania inalenga kuwapa vijana ujuzi wa kijani, ajira, na teknolojia rafiki kwa mazingira katika sekta za nishati mbadala, kilimo hifadhi, na viwanda ili kuandaa fursa kwa vizazi vijavyo.
Rais Samia amehitimisha kwa kuthibitisha tena dhamira thabiti ya Tanzania katika kufikia malengo ya Mkataba wa Paris, huku akiomba mkutano wa COP31 uwe hatua ya kugeuza kurasa kutoka kwenye ahadi kwenda kwenye utekelezaji, kutoka kwenye dhamira kwenda kwenye vitendo, na kutoka kwenye maazimio kwenda kwenye matokeo yanayopimika kwa maslahi ya dunia nzima.
