
Mwandishi Wetu, Wino Tanzania
Pamoja na kuongezeka kwa ushiriki wa wanawake katika siasa na vyombo vya uongozi barani Afrika, bado wanawake wanaendelea kuwa na nafasi ndogo katika michakato ya maamuzi, diplomasia na utatuzi wa migogoro, hali inayozua maswali kuhusu nguvu halisi ya uwakilishi wao.
Hoja hiyo imeibuka katika Mkutano wa Kimataifa wa Wabunge Wanawake wa Ukanda wa Maziwa Makuu uliofanyika jijini Dar es Salaam, ambapo viongozi kutoka nchi mbalimbali wametoa wito wa kuimarisha ushiriki wenye tija wa wanawake katika ujenzi wa amani, utatuzi wa migogoro na maendeleo ya kikanda.
Makamu wa Rais wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, amesema nchi za ukanda wa Maziwa Makuu zinapaswa kuongeza ushiriki wa wanawake katika nafasi za maamuzi, ikiwemo mabunge na serikali, huku zikikuza diplomasia ya wanawake, mitandao ya wapatanishi na mifumo ya kulinda amani.
Akizungumza katika mkutano huo, Ndejembi amesema ushiriki wa wanawake ni nguzo muhimu katika kuimarisha uongozi, kudumisha amani na kufanikisha maendeleo endelevu.
“Mkutano huu pamoja na ajenda zake ni kielelezo cha jitihada kubwa zinazofanywa kuwainua wanawake na nafasi yao muhimu katika kuimarisha uongozi, kudumisha amani na kutetea maendeleo endelevu. Kwa njia hii tunathibitishia dunia kuwa wanawake ni kiungo muhimu wanaposhirikishwa katika mchakato wa maamuzi na ujenzi wa taifa.”amesema Ndejembi
Ndejembi ametaja maeneo matano yanayopaswa kupewa kipaumbele katika utekelezaji wa maazimio ya mkutano huo. Yakiwemo kuongeza ushiriki wa wanawake katika vyombo vya maamuzi, kukuza diplomasia na mitandao ya wapatanishi wanawake, kuimarisha ulinzi wa wanawake na wasichana dhidi ya ukatili wa kijinsia, kuwekeza katika elimu na uongozi kwa wanawake na vijana, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kikanda na uwajibikaji katika utekelezaji wa maazimio hayo.
Hata hivyo, wadau walioshiriki mkutano huo wameeleza kuwa pamoja na hatua zilizopigwa katika kuongeza uwakilishi wa wanawake, changamoto za ukatili wa kijinsia, ubaguzi na kunyimwa nafasi ya kutoa maoni na kushawishi maamuzi bado zinaendelea kujitokeza.

Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Masuala ya Wanawake, Amani na Usalama katika Ukanda wa Maziwa Makuu, Jhuan Zianha, amesema uwepo wa wabunge wanawake ni hatua muhimu katika kuhakikisha masuala yanayowahusu wanawake na wasichana yanapata uwakilishi katika mifumo ya uongozi na utatuzi wa migogoro.
Amesema wanawake na wasichana katika ukanda huo bado wanakabiliwa na changamoto zinazotokana na migogoro, ukosefu wa usawa wa kijamii na kiuchumi pamoja na ukatili wa kijinsia.
“Wanawake na wasichana bado wanakabiliwa na changamoto za kulazimika kuyahama makazi yao kutokana na migogoro, ukosefu wa usawa wa kijamii na kiuchumi, pamoja na ukatili wa kijinsia. Hali hii inatukumbusha umuhimu wa kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika michakato ya kutafuta suluhu ya migogoro, kujenga amani na kufanya maamuzi katika ngazi zote.”Zianha
Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha ukubwa wa pengo hilo. Ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Wanawake, Amani na Usalama ya mwaka 2025 inaeleza kuwa katika michakato ya amani mwaka 2024, wanawake walikuwa asilimia saba tu ya washiriki katika majadiliano, asilimia 14 ya wapatanishi na asilimia 20 ya waliotia saini makubaliano ya amani.
Takwimu hizo zinaashiria kuwa kuongeza idadi ya wanawake katika vyombo vya uongozi pekee hakutoshi, iwapo hawapati nafasi sawa ya kushiriki katika majadiliano na kushawishi maamuzi yanayohusu mustakabali wa jamii zao.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Judith Suminwa Tuluka, ameibua hoja hiyo kwa kuhoji iwapo wanawake wamepewa nafasi halisi katika michakato ya ujenzi wa amani, akisisitiza kuwa uwakilishi bila mamlaka ya kufanya maamuzi hauwezi kuleta mabadiliko yanayotarajiwa.
Kauli hiyo inaweka wazi changamoto inayokabili ushiriki wa wanawake katika uongozi: tofauti kati ya kuwapo kwenye meza ya mazungumzo na kuwa na uwezo wa kushawishi maamuzi yanayofikiwa.
Kwa nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu, ambako migogoro ya kisiasa na kiusalama imeendelea kuathiri maisha ya wananchi, utekelezaji wa maazimio matano ya mkutano huo utakuwa kipimo muhimu cha dhamira ya serikali katika kuhakikisha wanawake si washiriki wa mikutano pekee, bali pia ni sehemu ya maamuzi yanayoamua mustakabali wa amani, usalama na maendeleo ya kikanda.
