
Serikali imesema uwekezaji kutoka kwa makampuni ya kigeni, hususan Ujerumani, haupaswi kuangaliwa kwa mtazamo wa mtaji unaoingia nchini pekee, bali pia teknolojia, ajira na fursa kwa wafanyabiashara wadogo na vijana wanaojihusisha na teknolojia.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amesema hayo Septemba 16 jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano na Waziri wa Shirikisho, Ulaya na Masuala ya Kimataifa wa jimbo la Hesse nchini Ujerumani, Manfred Pentz, aliyefika Tanzania akiwa na ujumbe wa wafanyabiashara kutoka nchini humo.

Kapinga amesema ziara hiyo ni mwendelezo wa mkutano wa Invest Africa uliofanyika mwezi uliopita, huku akieleza kuwa katika kipindi hicho thamani ya biashara kati ya Tanzania na Ujerumani imeongezeka kwa asilimia 56, na mauzo ya bidhaa kutoka Tanzania kwenda Ujerumani yameongezeka kwa asilimia 62.
“Tanzania tunahamasisha biashara na viwanda. Tumezungumza masuala ya biashara, viwanda, dawa na fursa nyingine ambazo wafanyabiashara wa Ujerumani wanaweza kunufaika nazo,” amesema.
Amesema Tanzania tayari ina uwekezaji kutoka kampuni za Ujerumani, ikiwemo Knauf na Twiga Cement, akieleza kuwa manufaa ya uwekezaji yanaonekana katika uhamishaji wa teknolojia, ajira na shughuli nyingine zinazochochea uchumi.
Ametoa mfano wa sekta ya saruji, akisema Twiga Cement iliyopo Tanga inatumia gesi asilia katika uzalishaji badala ya makaa ya mawe yanayotumiwa na baadhi ya viwanda.
“Kwa hiyo hata kuwa na teknolojia ambayo inatusaidia kutunza mazingira ni baadhi ya mambo ambayo tunanufaika nayo,” amesema.
Kwa upande wa ajira, Kapinga amesema uwekezaji huibua ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kupitia usafirishaji, mawakala, wasambazaji na wafanyabiashara.
Amesema Serikali pia inalenga vijana kunufaika na maendeleo ya teknolojia kupitia kampuni changa za teknolojia, maarufu kama startups.
“Tunapambana kwa ajili ya kufungua fursa kwenye mlengo huo na ndiyo maana suala la startup linapokuja. Tunaendelea ku-support startups kupitia initiatives mbalimbali,” amesema.
Kwa upande wake, Pentz amesema ujumbe wa wafanyabiashara wa Hesse umefika Tanzania kujenga ushirikiano wa muda mrefu kati ya kampuni za Ujerumani, Tanzania na Afrika Mashariki.
Amesema Hesse ina nguvu katika dawa, digitalization, akili bandia (AI), fedha na usafirishaji, huku akieleza kuwa wanataka kushirikiana na Jumuiya ya Afrika Mashariki katika teknolojia ya AI.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, James Ole Millya, amesema Tanzania ina nafasi ya kimkakati kwa wawekezaji kutokana na uanachama wake katika EAC na SADC.
“Tanzania tupo EAC na tupo SADC. Ukiwekeza kiwanda Tanzania, kiwanda kinapeleka bidhaa mpaka South Sudan. Kuna nchi nyingi zinazotuzunguka,” amesema.
Kapinga amesema Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya biashara na kutaka sehemu kubwa ya uwekezaji itoke katika sekta binafsi, ikiwemo kupitia ubia kati ya Serikali na sekta binafsi (PPP).
Amesema Serikali pia imeweka kalenda ya kodi kuongeza utabirika kwa wafanyabiashara, huku kikosi kazi kikishughulikia changamoto za kodi na juhudi zikiendelea kupunguza urasimu katika kodi na usajili wa biashara.
