
Berlin / Dar es Salaam, Novemba 19, 2026 – Upatikanaji wa maji safi katika miji inayokua kwa kasi nchini Tanzania, upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa kaya na biashara, vituo salama kwa wanawake na watoto wanaokimbia ukatili, pamoja na fursa mpya katika uchumi wa kidijitali ni miongoni mwa maeneo ambayo Tanzania na Ujerumani zimekubaliana kuyaimarisha kupitia ushirikiano wa maendeleo.
Makubaliano hayo yamefikiwa katika mazungumzo ya kiserikali yaliyofanyika mjini Berlin, Ujerumani, Novemba 18 na 19, 2026.
Ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Asha Khamis Abdulla, huku ujumbe wa Ujerumani ukiongozwa na Dkt. Bärbel Kofler, Katibu wa Jimbo wa Bunge katika Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (BMZ).
Mazungumzo hayo yanaashiria mwelekeo mpya wa kimkakati katika ushirikiano wa nchi hizo mbili, ambapo zimekubaliana kuelekeza nguvu katika maeneo yenye maslahi ya pamoja na ambayo msaada wa Ujerumani unaweza kuleta matokeo yanayoonekana.
Maeneo hayo ni pamoja na miundombinu ya kisasa ya maji na nishati, sera za mapato na kodi zilizo wazi na zinazotabirika ili kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji, uchumi wa kidijitali, pamoja na upatikanaji wa haki na ulinzi kwa wanawake na watoto.

Kama sehemu ya mkakati huo mpya, Ujerumani itatoa mikopo yenye riba nafuu kwa ajili ya miradi mikubwa ya miundombinu kwa kushirikiana na nchi nyingine za Ulaya.
Ushirikiano na sekta binafsi, ikiwemo kampuni za Tanzania na Ujerumani, pia utaimarishwa.
Makubaliano hayo yanaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na uchumi wa kipato cha kati cha juu, pamoja na Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP IV).
Ujerumani imekuwa mshirika wa maendeleo wa Tanzania tangu nchi ilipopata uhuru mwaka 1961 na inaendelea kuwa miongoni mwa washirika wake muhimu wa maendeleo.
Katika makubaliano hayo, Ujerumani imeahidi jumla ya euro milioni 116 katika ufadhili mpya, ambapo euro milioni 100 zitatolewa kama mikopo yenye riba nafuu kwa ajili ya sekta za maji na nishati, huku euro milioni 16 zikiwa ni ruzuku kwa ajili ya ushirikiano wa kiufundi.
Miradi hiyo itatekelezwa kupitia Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) kwa upande wa ushirikiano wa kifedha na Shirika la Ujerumani la Ushirikiano wa Kimataifa (GIZ) kwa upande wa ushirikiano wa kiufundi.
Maji na nishati: Uwekezaji wenye matokeo kwa wananchi
Kupitia mpango wa Team Europe na kwa kushirikiana na washirika wengine wa Ulaya, Ujerumani itasaidia kugharamia miradi mikubwa ya maji na nishati kwa kutumia mikopo yenye riba nafuu.
Katika miji mingi nchini Tanzania, huduma ya maji inakabiliwa na changamoto ya kuendana na kasi ya ongezeko la watu. Uwekezaji mpya unatarajiwa kuwezesha mamia ya maelfu ya wananchi kupata maji safi na salama pamoja na huduma za usafi wa mazingira.
Katika sekta ya nishati, Ujerumani itasaidia kuboresha mifumo ya uzalishaji na usambazaji wa umeme ili Watanzania wengi zaidi wapate umeme safi na wa uhakika kwa matumizi ya majumbani, mashambani na katika viwanda vya ndani.
Hatua hiyo pia inalenga kuongeza thamani ya malighafi zinazozalishwa nchini kabla ya kuuzwa katika masoko ya nje.
Uwekezaji huo unajengwa juu ya uzoefu wa miaka mingi wa ushirikiano kati ya nchi hizo mbili. Kupitia msaada wa Ujerumani, idadi ya kaya zilizounganishiwa huduma ya maji katika miji ya Kigoma na Lindi imeongezeka mara mbili au hata tatu, huku ujenzi wa njia mpya ya kusafirisha umeme katika Ukanda wa Ziwa ukisaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa upotevu wa umeme.
Zanzibar pia inaendelea kunufaika na ushirikiano katika huduma za maji na usafi wa mazingira.
Haki, mazingira ya uwekezaji na uchumi wa kidijitali
Upatikanaji wa haki: Maelfu ya wanawake, watoto na makundi mengine yaliyo katika mazingira hatarishi tayari yamepata ushauri wa kisheria kupitia programu zinazoungwa mkono na Ujerumani.
Kuanzia mwaka 2027, Ujerumani pia itasaidia kuanzishwa kwa nyumba salama kwa waathirika wa ukatili ili kuwapatia ulinzi na huduma wanazohitaji.
Mazingira ya uwekezaji na usimamizi wa fedha za umma: Kampuni na wawekezaji wanahitaji mfumo wa kodi unaotabirika na unaoaminika.
Kupitia programu mpya, ushirikiano huo utaelekezwa katika mageuzi yanayogusa moja kwa moja shughuli za kampuni na wawekezaji, ikiwemo kuboresha utendaji wa mamlaka za kodi ili ziwe na huduma zinazozingatia mahitaji ya walipa kodi, uwazi katika manunuzi ya umma na ushindani wa haki.
Hatua hizo zinalenga kupunguza gharama na hatari kwa wafanyabiashara na wawekezaji, pamoja na kupanua wigo wa mapato ya ndani yatakayoiwezesha Tanzania kugharamia maendeleo yake.
Uchumi wa kidijitali: Teknolojia za kidijitali ni miongoni mwa vichocheo muhimu vya ukuaji wa uchumi chini ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kupitia awamu mpya ya Kituo cha Mabadiliko ya Kidijitali Tanzania (Digital Transformation Center Tanzania), Ujerumani itashirikiana na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kampuni za Kitanzania, kampuni changa za teknolojia na vituo vya ubunifu katika kuendeleza mifumo ya malipo ya kidijitali, biashara mtandaoni na matumizi yenye uwajibikaji ya akili unde (Artificial Intelligence – AI).
Ushirikiano huo pia unalenga kuhakikisha wanawake hawaachwi nyuma katika mabadiliko hayo ya kiteknolojia.
Tangu mwaka 2024, kituo hicho kimewapatia mafunzo zaidi ya watu 450, wengi wao wakiwa wanawake, katika ujuzi wa kidijitali na teknolojia.
Aidha, kimewafikia karibu wanawake 18,000 kwa kuwapatia taarifa kuhusu haki zao katika matumizi ya teknolojia za kidijitali
