
Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP31), umemalizika mwishoni mwa wiki iliyopita huko jijini Antalya, Uturuki bila kufikiwa kwa makubaliano ya mwisho, hali iliyoelezwa kuwa pigo jipya katika vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi duniani.
Mkutano huo ambao umeweka rekodi ya kuwa mrefu zaidi katika historia ya mikutano ya Umoja wa Mataifa (UN), kuhusu mabadiliko ya tabianchi baada ya kuongezewa siku mbili za ziada nje ya wiki mbili zilizopangwa, uligonga mwamba kutokana na mvutano mkali kuhusu matumizi ya nishati ya visukuku (Nishati itokanayo na mabaki).
Katika rasimu ya mwisho iliyowasilishwa haikutaja moja kwa moja suala la kuachana na mafuta ya mabaki, hatua iliyopingwa vikali na mataifa mengi yakidai kuwa inarudisha nyuma ahadi zilizokwishatolewa awali na kupuuza uharaka wa janga la tabianchi linaloikabili dunia.
Mataifa kadhaa, yakiwemo ya Umoja wa Ulaya (EU), yamekataa rasimu hiyo iliyopewa jina la ‘Antalya Pact’, yakisisitiza kuwa haikidhi vigezo vya kisayansi wala uzito wa dharura uliopo sasa.
Akizungumzia matokeo hayo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amekiri kuwa kushindwa kupatikana kwa muafaka ni hatua ya kurudi nyuma, lakini amesisitiza kuwa ukweli wa kisayansi kuhusu sababu na athari za mabadiliko ya tabianchi hauna mjadala.
Guterres ametoa wito kwa mataifa yote duniani kutokata tamaa, badala yake yaendelee kuchukua hatua za haraka na za makusudi ili kupunguza uzalishaji wa gesijoto.
Wachambuzi wa masuala ya mazingira na sera wanaeleza kuwa kukwama kwa COP31 kunadhihirisha kuwepo kwa pengo kubwa kati ya nchi zinazopigania kupunguzwa kwa kasi kwa matumizi ya mafuta ya visukuku na zile ambazo uchumi wake unategemea zaidi uzalishaji wa nishati hiyo.
Hali hiyo inatajwa kuwa huenda ikakwamisha pia upatikanaji wa fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa nchi zinazoendelea na zilizo katika hatari zaidi ya kuathiriwa na majanga yatokanayo na mabadiliko hayo, zikiwemo nchi za Afrika.
Wadau hao wamebainisha kuwa safari ya kufikia muafaka wa kimataifa utakaounganisha upunguzaji wa gesijoto, mpito wa kuachana na mafuta ya visukuku, na utoaji wa misaada ya kifedha na kiteknolojia kwa nchi zenye uwezo mdogo, bado ina kibarua kigumu mbele yake.
