
Ni kilio kwa wafuasi wa aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei aliyeuliwa wakati wa shambulio la Marekani na Israel usiku wa kuamkia Machi. Leo Machi 2, wafuasi hao wamemiminika mitaani katika mji mkuu wa Iran kuomboleza.
Lakini kwa Wairani wengine, kifo hicho kimewafurahisha baada ya kupambana kwa muda mrefu kuukosoa utawala wake wa miaka 36 bila mafanikio.
Mashambulio ya Marekani na Israel yaliyoanza Februari 28, 2026 yalishatarajiwa kwa sababu Rais wa Marakeni, Donald Trump alishatangaza mara kadhaa mpango wa kuishambulia Iran, akitoa sababu za nchi hiyo kufadhili makundi ya kigaidi yakiwamo ya Hezbollah na Hamas, huku pia akijiapiza kuhakikisha mradi wa nyuklia wa Iran haufanikiwi.
Japo Iran imekuwa ikijitetea kwamba mradi wake wa nyuklia ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo kama umeme, lakini utetezi huo ulikataliwa na Marekani, wakidai kuwa ni kisingizio tu. Kutokana na mradi huo, Iran iliwekewa vikwazo vya kiuchumi na imekuwa ikijiendesha kibabe tu.

Ayatollah Khamenei
Ayatollah Khamenei aliyezaliwa mwaka 1939, aliingia madarakani kama kiongozi mkuu wa nchi mwaka 1988 kufuatia kifo cha Ayatollah Ruhollah Khomeini aliyefariki akiwa na miaka 86. Kabla ya hapo Khamenei alikuwa rais wa kwanza wa nchi hiyo tangu yalipofanyika mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979.
Khamenei ameshanusurika kadhaa kuuawa, likiwemo jaribio la mauaji likiwemo shambulio la Juni 27, 1981, ambnapo Khamenei, ambaye wakati huo alikuwa kiongozi mashuhuri wa kidini na mgombea wa urais, alinusurika kwa taabu jaribio la kumuua katika Msikiti wa Abuzar jijini Tehran.
Shambulio hilo lilitokea wakati akihutubia waumini, ambapo bomu lililokuwa limefichwa ndani ya kinasa sauti (tape recorder) lililipuka karibu naye. Mlipuko huo ulimjeruhi vibaya, ukaharibu mkono wake wa kulia (na kumwacha na ulemavu wa kudumu), pamoja na kuathiri nyuzi zake za sauti na mapafu.
Baada ya tukio hilo, alilazwa hospitalini kwa miezi kadhaa akipatiwa matibabu.
Ameshanusurika pia kwenye mashambulizi kadhaa ya Israel ambayo imekuwa ikiishambulia nchi hiyo mara kadhaa.
Uongozi wa Ayatollah Khamenei
Baada ya Ali Khamenei kuchukua nafasi ya Kiongozi mkuu, aliliimarisha na kuendeleza jeshi la Islamic Revolutionary Guard Corps (IRGC), akiibadilisha kuwa chombo kikuu cha udhibiti wa ndani na ushawishi wa kikanda.
Chini ya uongozi wake, Iran iliunga mkono muungano unaojulikana kama “Axis of Resistance” katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Syria, vita vya Iraq, vita vya Yemen na vita vya Gaza, pamoja na kuunga mkono Urusi katika vita vya Urusi na Ukraine.
Akiwa mkosoaji mkubwa wa Israel na Uzayuni, Khamenei aliunga mkono Wapalestina katika mzozo wa Israel na Palestina; matamshi yake yalijumuisha wito wa kuangamizwa kwa Israel pamoja na kauli zilizotajwa kuwa za chuki dhidi ya Wayahudi.
Katika kipindi cha uongozi wake, Iran ilihusika katika vita vya wakala (proxy wars) dhidi ya Israel na Saudi Arabia.
Kutokana na misimamo yake, mwaka 2025 na 2026, mvutano kati ya Iran, Israel na Marekani uliongezeka na kusababisha Vita vya Siku Kumi na Mbili pamoja na mzozo unaoendelea, ambapo katika mzozo huo Khamenei aliuawa.
Wakati akijenga uhasama na mataifa ya Magharibi, Khamenei pia alijikuta akipoteza umaarufu kwa wananchi wake. Mwaka 2009 baadhi ya wanamageuzi walipeleka barua ya malalamiko kwa Baraza la Wataalamu, wakitaka Khamenei achunguzwe kama bado anaweza kutawala.
Kama hiyo haitoshi barua nyingine iliyoandikwa na watu wasiojulikana, iliulaumu utawala wa Khamenei kwamba ni wa kidikteta na wa unyanyasaji.
Jambo la pili uchaguzi wa mwaka 2009 uliofanyika Juni 12 ,2009, ambapo rais aliyekuwa madarakani, Mahmoud Ahmadinejad, aligombea dhidi ya wagombea watatu wengine.
Asubuhi iliyofuata, Islamic Republic News Agency (IRNA) ilitangaza kuwa baada ya kuhesabiwa theluthi mbili ya kura, Ahmadinejad alikuwa ameshinda kwa kupata asilimia 62 ya kura zote zilizopigwa, huku mpinzani wake mkuu, Mir-Hossein Mousavi, akipata asilimia 34 ya kura.
Hata hivyo, kulikuwa na madai ya dosari na kasoro kubwa katika matokeo hayo, hali iliyosababisha maandamano makubwa yaliyohusisha mamilioni ya Wairani katika miji mbalimbali ya Iran na pia katika nchi nyingine duniani, na hatimaye kuibuka kwa harakati ya upinzani iliyoitwa Iranian Green Movement.
Kufuatia malalamiko hayo, Juni 16, 2009 Baraza la Uongozi ilitangaza kuwa itahesabu upya asilimia 10 ya kura na baadaye ikahitimisha kuwa hakukuwa na dosari zozote, huku ikitupilia mbali malalamiko yote kuhusu uchaguzi huo.
Hata hivyo,mpinzani mkuu wa Ahmednejad, Mir-Hossein Mousavi alipinga suala hilo akidai kuwa kuna kura milioni 14 ambazo hazikuhesabiwa.
Kuona mambo yatakuwa magumu, Juni 19, Kiongozi Mkuu wa Iran, Ali Khamenei, alilaani maandamano ya wafuasi wa Mousavi na kuyataja kuwa ni haramu. Siku iliyofuata, maandamano hayo yalikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa vikosi vya usalama vya serikali na kusababidha vifo na watu kujeruhiwa.
Maandamano

Mwaka 2023 yaliibuka maandamano mengine dhidi ya serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, yaliyochochewa na kifo cha Mahsa Amini aliyekuwa akishikiliwa na polisi.
Maandamano hayo yalianza Septemba 16, 2022 na kuendelea hadi mwaka 2023. Hata hivyo, kufikia majira ya machipuko ya 2023, maandamano hayo yalikuwa kwa kiasi kikubwa yamepungua, na hatimaye uongozi wa kisiasa uliendelea kubaki madarakani bila mabadiliko.
Maandamano hayo yalikuwa makubwa kuwahi kutokea na yaliyoleta upinzani mkali kuwa kushuhudiwa tangu yalipofanyika mapinduzi wa kiislamu ya mwaka 1979.
Maandamano ya 2025
Kuanzia Desemba 28, 2025, maandamano yalizuka katika miji mbalimbali ya Iran, yakifuatia hali ya taharuki ya kitaifa dhidi ya serikali na kuzorota kwa uchumi. Tukio hilo limetajwa kuwa uasi mkubwa zaidi tangu yatokee Mapinduzi ya Kiislamu ya 1979.
Matumizi makubwa ya nguvu yalitekelezwa, ikiwamo matumizi ya risasi za moto dhidi ya waandamanaji, kwa amri ya Ali Khamenei na maafisa wengine waandamizi. Hatua hiyo ilisababisha mauaji makubwa yaliyoacha maelfu ya watu wakiwa wamefariki, yakitajwa kuwa miongoni mwa mauaji makubwa zaidi katika historia ya kisasa ya Iran.
Kundi la Human Rights Activists in Iran lilithibitisha vifo vya angalau watu 7,000, wakati serikali ya Iran ilikiri vifo 3,117. Taarifa nyingine zilikadiria idadi ya vifo kufikia 32,000.
Maandamano hayo yalianza kutokana na hasira juu ya mfumuko wa bei uliovunja rekodi, kupanda kwa bei ya vyakula na kushuka kwa thamani ya sarafu. Hata hivyo, haraka yakageuka kuwa harakati pana zaidi iliyodai kukomeshwa kwa utawala wa Kiislamu.
Yalianza na wafanyabiashara wa soko (bazaari) katika Soko Kuu la Tehran, kisha kuungwa mkono na wanafunzi wa vyuo vikuu, na baadaye kuenea katika miji mikubwa na midogo. Waandamanaji walipaza sauti kauli za kupinga serikali.
Ni furaha, huzuni
Licha ya hasira kali walizokuwa nazo Wairani, hawakuweza kuung’oa utawala wa Ayatollah Khamenei kwa kuwa ulikuwa ukijibu malalamiko yao kwa mtutu wa bunduki. Ila kwa mashambulio ya Israel na Marekani, imewekana kwa Ayatollah Khamenei kuhitimisha utawala wake wa miaka 36 kama kiongozi mkuu wa nchi hiyo.
Picha za video zimeonyesha baadhi ya wananchi wa Iran hasa wanaoishi nje ya nchi, wakiwa nchini humo na wengine nje ya nchi hiyo wakishangilia kifo cha kiongozi wao. Hiyo ni ishara kuwa, hawakuwa na namna yoyote ya kumntoa madarakani kiongozi huyo, hivyo wako tayari kushangilia mashambulio ya nchi nyingine dhidi ya kiongozi wao.
Hata hivyo, kifo hicho kimeibua msiba mzito kwa Wairani, ambao wamekusanyika katika mitaa ya jiji la Tehran wakiomboleza kwa kumpotez akiongozi wao.
