
Mwandishi wetu
Bagamoyo. Katika utafiti wa kihistoria uliyochapishwa katika jarida la Nature, wanasayansi wa Taasisi ya Afya Ifakara (IHI) na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa (NIMR) kwa ushirikiano na Imperial College London kupitia mpango wa Transmission Zero, wamefanikiwa kuzalisha mbu waliobadilishwa vinasaba nchini Tanzania ambao wanazuia uenezaji wa malaria.
Akizungumzia utafiti huo leo Desemba 10 wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani, Mkurugenzi wa Programu wa IHI, Dk Dickson Wilson Lwetoijera amesema hii ni mara ya kwanza kwa mbu walioandaliwa kwa teknolojia ya “gene drive” kutengenezwa barani Afrika na wanasayansi wa Kiafrika, wakilenga vimelea vya malaria vinavyosambaa katika jamii zetu.
“Tunajivunia kuongoza ubunifu huu hapa hapa nyumbani, tukitumia teknolojia ya kisasa kukabili changamoto mojawapo kubwa zaidi ya afya barani mwetu,” amesema.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Homa ya Malaria ya Shirika la Afya Duniani (WHO), Tanzania ni miongoni mwa nchi nne duniani zinazochangia zaidi ya nusu ya vifo vyote vya malaria, huku watu takribani asilimia 93 wakiwa hatarini kuambukizwa.
Mbinu za jadi kama vyandarua na kunyunyizia dawa ndani zimeokoa mamilioni ya maisha, lakini sasa zinakabiliwa na changamoto za kuongezeka kwa usugu wa dawa na ongezeko la idadi ya watu.
Utafiti huo uliofanyika katika Maabara Maalum ya Kisasa (Modular Portable Laboratory) na kituo cha juu cha usalama wa maabara (Containment Level 3) katika kampasi ya IHI, unatarajiwa kuleta mapinduzi makubwa katika mapambano dhidi ya malaria duniani.
Profesa George K. Christophides wa Imperial College London, amesema huo si utafiti wa teknolojia pekee, bali ni utafiti wa uongozi, uwajibikaji, na ushirikiano.
Safari ya utafiti
Mwaka 2023, watafiti wa Transmission Zero walizalisha mbu wa kwanza kabisa waliobadilishwa vinasaba barani Afrika, hapa Tanzania. Utafiti wa sasa unatoa suluhisho jipya kwa kubadilisha vinasaba vya mbu Anopheles gambiae(wabebaji wakuu wa malaria) ili kuzuia ukuaji wa vimelea vya malaria, hivyo kupunguza uwezo wao wa kusambaza ugonjwa.
Mabadiliko haya yanaweza kurithishwa kutoka kizazi kimoja cha mbu hadi kingine—kwa kifupi: mbu wanaendelea kuwepo, lakini hawawezi tena kusambaza malaria.
“Matokeo haya kwa Anopheles gambiae ni mwanzo wa kupanua teknolojia hii kwa mbu wengine muhimu kama Anopheles arabiensis na Anopheles funestus, na hata mbu wanaosambaza magonjwa kama Dengue na Chikungunya,” amesema Dk Lwetoijera.
Kwa mujibu wa Dk Lwetoijera, utafiti huo umefanyika kikamilifu katika mazingira ya maabara yenye udhibiti mkali na si katika mazingira ya nje.
“Wanasayansi walichanganya sifa za kupambana na malaria—molekuli zinazotokana kwa asili na vyura na nyuki—katika mbu wa eneo husika. Mbu hao waliobadilishwa walizuia kabisa ukuaji wa Plasmodium falciparum, vimelea vinavyosababisha malaria barani Afrika, hivyo kuweka kizuizi muhimu dhidi ya maambukizi.”
Hata hivyo, Dk Lwetoijera amesema, pamoja na matokeo hayo ya kutia moyto, hatua inayofuata ni tathmini za kina za hatari, mashauriano na wadhibiti, na mazungumzo ya jamii ili kuhakikisha usalama, ufanisi, na kukubalika kwa teknolojia.
Dk Nikolai Windbichler, Mkuu wa Utafiti wa Vinasaba Imperial College London, amesema la utafiti huo ni ni kutoa chombo kipya kitakachosaidia kuongeza nguvu mbinu zilizopo ili kutokomeza malaria Afrika.
