
Rais Samia Suluhu Hassan
Na Mwandishi wetu
Wakati bado kukiwa na mwangwi wa vurugu zilizosababishwa na maandamano ya Oktoba 29, jumuiya za kimataifa, balozi na mashirika ya kimataifa yamekosoa hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Tanzania, zilizosababisha mauaji, majeruhi na uharibifu wa mali.
Matamko hayo yameibua wasiwasi mkubwa kuhusu mustakabali wa kisiasa na haki za binadamu nchini Tanzania kufuatia uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk Faraja Kristomus amesema kuna uwezekano mkubwa kuwa mahusiano ya Tanzania na nchi wafadhili, taasisi za kimataifa na washirika mbalimbali wa kikanda na kimataifa yataathirika kwa kiasi kikubwa.
“Katika nchi nyingi duniani sera za kiongozi aliyeko madarakani hutoa mwelekeo wa mahusiano ya kidiplomasia. Tanzania inaweza kuathirika kwa sababu serikali za nchi hizo zinazoinyooshea vidole serikali ya Tanzania zinaweza kusitisha misaada yao, na pia kuwahimiza raia wao wasije Tanzania kwa shughuli za utalii na biashara.
“Pia mahusiano kati ya Watanzania na nchi hizo yataathirika kwa sababu masharti ya nyaraka za kusafiria yatakuwa magumu zaidi. Itakuwa vigumu kwa watanzania kusafiri kwa urahisi kwenda nchi hizo,” amesema Dk Kristomus.
Miongoni mwa nchi zilizotoa matamko ni Marekani ambayo imesema inatafakari kuhusu uhusiano wake wa kibalozi na Tanzania.
Katika taarifa yake iliyotolewa hivi karibuni, Marekani imezitaja hatua za serikali ya Tanzania, ikiwemo kunyanyasa uhuru wa dini na kujieleza, vizuizi kwa uwekezaji wa Marekani, na vurugu dhidi ya raia, kama sababu ya kufanya mapitio ya kina ya uhusiano wake kidiplomasia na nchi yetu.
Wengine ni wataalamu wa Umoja wa Mataifa wliolaani mauaji yaliyotokea wakati wa maandamano, wakisema ni kinyume cha sharia. Pia wamegusia suala la kuzimwa kwa mtandao wa intaneti, na kukamatwa kwa wingi wa waandamanaji, wanasiasa wa upinzani, na wanaharakati wa haki za binadamu.
Wataalamu hao wameitaka Serikali kutoa taarifa kuhusu waliopotea, kurejesha mabaki kwa familia, kuondoa vizuizi vya vyombo vya habari, na kufanya uchunguzi huru.
Pia, nchi ya Ghana na nchi za Magharibi, ikiwemo Uingereza, Canada, na ubalozi wa nchi 15 za Ulaya, zimetuma kauli kali zikisisitiza kuwa serikali ya Tanzania irejeshe miili kwa familia, waachilie wafungwa wa kisiasa, na kutekeleza mapendekezo ya Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kuhusu uchaguzi.
Kwa upande mwingine Jumuiya ya Hatua za Madola (CMAG) imeweka Tanzania kwenye ajenda rasmi kwa hatua za kisiasa za Machi 2026, ikiwa na masharti ya kutolewa kwa vizuizi vya uhuru wa kiraia na vyombo vya habari, kuruhusu mazungumzo ya kisiasa, uwajibikaji kwa vurugu za uchaguzi, na fidia kwa waathirika.
Hata hivyo, Serikali ya Tanzania imesema imepokea matamko haya na kuwa na mpango wa kuendelea na uchunguzi kupitia Tume ya Uchunguzi iliyoundwa, ikisisitiza kuwa ripoti yake itasaidia kuelezea matukio yasiyofaa na kuwa msingi wa ushirikiano wa kimataifa katika siku za usoni.
Matamko hayo yamekuja wakati Rais Samia Suluhu Hassan, akiweka msimamo mkali kwa nchi na jumuiya za kimataifa, kwamba hataki Tanzania ipangiwe cha kufanya. Aliyasema hayo Desemba 2, alipokuwa akizungumza na wazee wa Dar es Salaam.
“Nje huko wanakaa, ooh, Tanzania ifanye moja, ifanye mbili ifanye tatu, halafu ndiyo itakuwa hivi, Who are you?!” alisema huku akishangiliwa na wazee hao.
“Niwaulize ndugu zangu, kwao hayatokei? Tumenyanyua sauti sisi kusema ya kwao? Wanadhani wao bado ni masters au wakoloni kwetu? Kitu gani ni fedha chache wanayotugawia? Na fedha yenyewe sasa hivi haipo, wanafanya biashara wao wapate na sisi tupate, ndipo tunaposimamia.
Tunajenga au tunabomoa?
Akizungumzia matamko hayo na hali ya siasa nchini, mchambuzi wa masuala ya kimataifa, Denis Konga amesema ni wazi kwamba Tanzania itaathrika.
“Kitu cha msingi ni kuimarisha utengamano wa kimataifa, lakini ukiangalia matamko haya na hatua zinazochukuliw ana Serikali ni wazi kwamba tunajiondolea nafasi yetu tuliyokuwa tunajivunia kwa miaka mingi kama msuluhishi inapotokea migogoro kwa wengine,” amesema.
Amegusi suala la kuchumi, akisema hata wadau wa maendeleo wataiuliza mara mbili wanapotakiwa kutusaidia.
“Wadau wa maendeleo watajiondoa na hata watakapotaka kutusaidia watakuwa wanajiuliza kama kweli watusaidie au watakuwa wanaunga mkono vunjifu wa haki za binadamu?”
Akizungumzia kauli ya Rais Samia kuhusu misaada ya nchi wahisani, Konga amesema kwa ujumla hotuba ile imejenga taswira mbaya kwa uhusiano wa kimataifa.
“Rais Samia alikuwa na nafasi nzuri siku ile kumaliza suala hili, kwa kutoa kauli zinazolenga kuunganisha wananchi, lakini kauli zake zilikiri kwamba Serikali imesababisha uvunjifu wa haki za binadamu,” amesema.
Katika hotuba yake, Rais Samia alisema nguvu iliyotumika kwa waandamanaji ilistahili. “Nguvu inayotumika inaendana na tukio lililopo. Tunapoambiwa tulitumia nguvu kubwa sana kwenye tukio lile, nguvu ndogo inakuwa ipi? Ilikuwa tuwaangalie waandamanaji waliojiandaa kufanya mapinduzi mpaka wafanikiwe?” alisema.
Kwa upande mwingine, Konga amesema hata Serikali inaposema kuwa itatuia vyanzo vya ndani kujikimu kibajeti, amesema bado italeta shida kwa sababu bado pia inategemea kukopa vyanzo vya ndani, hivyo kuna uwezekano mkubwa wa kuwaumiza wananchi.
“Kama Serikali itaendelea na msimamo huu, huenda Tanzania itakwenda kuwa kama Zimbabwe wakati wa Hayati Rais Robert Mugabe,” amesema.
Akizungumzia hatua zilizochukuliwa na Rais Samia ikiwa pamoja na uundwaji wa Tume ya kuchunguza uvunjifu wa Amani wakati wa uchaguzi, Konga amesema bado hakujawa na utahi wa kisiasa kumaliza tatizo.
“Ukiangalia tume ile utaona watu wengi hawana Imani nayo kwa sababu ya muundo wake,” amesema.
Katika hilo, Dk Kristomus anamuunga mkono Konga akisema matatizo yaliyotokea ni makubwa sana kuliko hatua ambazo serikali imechukua.
“Kauli za viongozi wetu hasa wa ngazi ya juu zimekuwa za kutonesha zaidi vidonda kuliko kuponya. Hata kama tume imeundwa lakini kutokana na kauli za Rais Samia za kuonyesha kuwa aliridhia askari kufanya mauaji yale zinafanya tume hiyo kukosa uhalali na kukosa imani ya wananchi.
“Kupuuza maumivu ya wananchi wasio na hatia katika hotuba zake kumeongeza zaidi hasira za wananchi,” amesema.
