
Mwandishi wetu
Dar es Salaam. Wakati kukiwa na malalamiko ya wananchi na jumuiya ya kimataifa kuhusu hatua zilizochukuliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuzima intaneti intaneti siku ya uchaguzi Oktoba 29, 2025, mamlaka hiyo imekanusha ikisema, “TCRA haikuzima intaneti bali ilichukua hatua za kiudhibiti kwenye baadhi ya huduma za mawasiliano zinazotolewa na mtandao wa intaneti.”
Japo siku ya Oktoba 29 ilianza kwa amani, huku maeneo mengi yakishuhudiwa kuwa na idadi ndogo ya wapiga kura, lakini ilipofika saa 5 asubuhi, maandamano yalizuka maeneo mbalimbali ya nchi, katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Kilimanjaro, Mbeya, na baadaye hali hiyo iliambukiza mikoa mingine kioni ya siku hiyo na kesho yake kama vile Njombe, Iringa, Geita na Ruvuma.
Kwa waandishi wa habari hali ilikuwa mbaya, baada ya intaneti kuzimwa kuanzia saa 7 mchana hali iliyosababisha washindwe kupokea na kutuma taarifa. Kutokana na halihiyo baadhi ya vyombo vya habari zikiwamo kampuni za kuchapisha magazeti, mitandao ya jamii, televisheni na redio zilifungwa kwa takribani siku tano.
Hata hivyo, baadhi ya vituo vya televisheni na redio vikiwemo vya Serikali (TBC), televisheni binafsi kama ITV, Star TV waliendelea na matangazo, wakidai kupewa maelekezo na Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Ripoti za awali za waangalizi wa uchaguzi wakiwamo aJumuiya ya Nci za Kusini mwa Afrika (SADC) na Umoja wa Afrika (AU) pamoja na Chama tawala cha Afrika Kusini (ANC), wametaja hatua ya kuzima intaneti kama kuvurugwa kwa uchaguzi huo na kuchochea uvunjifu wa haki za binadamu.
Mbali na madai ya kuzima intaneti, TCRA inalalamikiwa kwa kutoa maelekezo kwa redio na televisheni kuhusu maudhui ya kurusha, hali inayotajwa kuingilia uhuru wa vyombo vya habari.
Madai ya TCRA kuzima intaneti
Akifafanua kuhusu malalamiko hayo, Meneja wa Utangazaji wa TCRA, Mhandisi Andrew Kisaka amesema intaneti inatoa huduma nyingi za mawasiliano, ambapo miongoni mwa hizo kilichozimwa ni mawasiliano kwa njia ya mitandao ya kijamii (social media), huku nyingine zikiendelea.
Ametaja huduma nyingine alizosema ziliendelea kuwa pamoja huduma za kibenki ikiwa pamoja na miamala ya fedha; huduma za Afya kwa Umma ikijumuisha mifumo ya Bima ya Afya ya Taifa (NHIF); huduma za Utangazaji hii ikijumuisha mifumo ya utangazaji ikisomana na mifumo ya kifedha kwa ajili ya “pay tv” na huduma za kiofisi kwa Taasisi za Serikali.
TCRA yalalamikiwa kuingilia uhuru wa vyombo vya habari
Akizungumzia hali ilivyokuwa Oktoba 29, mwanahabari mkongwe, Neville Meena amesema licha ya kutoandaliwa kwa wanahabari kukabiliana na hali hiyo, TCRA waliingilia uhuru wa vyombo vya habari kwa kuanza kuwapingia watangazaji wa redio na televisheni vipindi vya kutangaza.
“Uchaguzi ulianza asubuhi na vyombo vya habari viliripoti kilichoendelea. Viongozi walionekana wakipiga kura, na baadhi ya vuongozi walizungumza.
“Baadaye kuanzia saa 4 asubuhi, vurugu zikaanza na zilirushwa mitandaoni. Ilipofika jioni, televisheni na radio vilionyesha matukio ya watu kupiga kura, lakini hawakuonyesha vurugu zilipotokea. Kwa hiyo walikuwa wanatangaza uongo.
“Kwa upande wa redio vituo vingi viliacha kutangaza, wakawa wakipiga muziki tu. Unajua redio nyingi zinaendeshwa kidigitali, yaani unapanga muziki na matangazo vinajipiga vyenyewe tu,” amesema.
Meena amesema pamoja na kwamba suala hilo lilikuja ghafla, lakini hawakutarajia intaneti izimwe.
“Tulijua kwamba, pamoja na vurugu zile, mambo yangeenda kama kawaida. Kwa mfano wakati wa mlipuko wa Uviko-19, mtandao uliendelea kuwepo, lakini safari hii walizima intaneti, tukajikuta hatuwezi kupata taarifa yoyote ndani na nje ya nchi wala huwezi kutuma taarifa yoyote,” amesema.
Maoni hayo yameungwa mkono na Mwenyekiti wa MISA-TAN, Edwin Soko akisema licha ya intaneti kuzimwa, TCRA ilikuwa ikitoa maenelezo kwenye vyombo vya habari kuhusu maudhui ya kutangaza.
“Kwanza kulikuwa na maagizo ya TCRA ya namna ya kuendesha vipindi na hata kuondoa vipindi vilivyokuwepo. Kuna baadhi ya televisheni na redio zilifungwa kwa siku kadhaa,” amesema.
Mkurugenzi wa Wakfu wa Waandishi wa Habari (TMF), Dastan Kamanzi anasema waandishi wa habari hawawezi kulaumiwa kwa hali iliyotokea.
“Vyombo vya habari vya Tanzania havipaswi kulaumiwa. Atakayelaumu kwanza aangalie kwanza vyombo hivyo vinafanya kazi katika mazingira gani.
“Tujiulize, vyombo vya habari vingefanyaje kazi wakati kuna makatazo ya Serikali? Kulikuwa na marufuku ya kutotoka nje na intaneti ilizimwa, watu wangefanyaje kazi? Kwa hali kama hiyo vyombo vya habari haviwezi kufanya kazi,” amesema.
TCRA wafafanua
Akizungumzia madai ya kutoa maelekezo kwa vyombo vya utangazaji ya vipindi kurushwa, Kisaka amesema TCRA kama msimamizi wa sekta ndogo ya huduma za utangazaji husimamia sekta hii kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Miongozo iliyopo.
“Sheria, kanuni na miongozo hii hutengenezwa kwa pamoja ikijumuisha wadau wote wa kisekta kwa kuzingatia mahitaji mbalimbali yanayojitokeza. Sheria, kanuni na miongozo hii hupitiwa na kuboreshwa kila baada ya muda ili kuhakikisha zinaendana na mabadiliko na ukuaji wa sekta,” amesema.
Ameendelea kufafanua kuwa, TCRA hufuatilia maudhui yanayorushwa na vituo vya utangazaji (content monitoring) ili kuhakikisha yanazingatia sheria na kanuni zinazosimamia sekta.
“Kwa wale wanaoenda kinyume na Sheria na kanuni za utangazaji, TCRA hutoa maelekezo ya kurekebisha dosari hizo. Vituo vya Utangazaji huelezwa vifungu vya Kisheria na Kanuni vilivyokiukwa ili kuondoa dosari zinazojitokeza. TCRA hutoa adhabu pale chombo cha utangazaji kinaporudia makosa na kukaidi kujirekebisha kadiri ya Sheria, Kanuni na miongozo iliyowekwa,” amesema.
Amesema TCRA imetoa leseni ya huduma za utangazaji wa maudhui (main stream) kwa redio 255 na TV 72 pia imetoa leseni za utangazaji wa maudhui mtandaoni 314.
“Katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu kuna dosari kadhaa zilijitokeza kwa baadhi ya vyombo vichache vya mtandaoni zilizopelekea vyombo hivyo kupewa maelekezo ya kurekebisha dosari hizo.
“Kosa kubwa lililojitokeza kwenye kipindi hicho ni kutoa habari za upande mmoja zikiwa na tuhuma nyingi zisizokuwa na mizania ambayo ni kinyume na taaluma ya uandishi wa habari inayotaka utoaji wa habari unaozingatia ukweli na uhakika ili kuzuia taharuki,” amesema.
TBC wajitetea
Wakati vurugu zikiendelea tangu Oktoba Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kupitia televisheni na redio zake, haikutangaza vurugu hizo, badala yake jioni ilijikita kutangaza matokeo ya uchaguzi.
Akizungumza katika mahojiano Novemba 25,2025 katika mahojiano kwenye Kipindi cha Jambo Tanzania cha TBC1, Mkurugenzi Mkuu wa Dkt. Ayub Rioba Chacha, amedai kuwa vyombo vya habari vilitishiwa na waandamanaji.
“Tuseme kwamba, labda TBC pekee ilitishwa, lakini kumbe vyombo vya habari vyote vilitishwa. Ndio maana hata wanaosema kwamba, CNN imefanya kazi yake, kwa nini ninyi hakumtoa habari zile?”
Amesema kuwa TBC walipeleka waandishi mitaani, lakini vurugu zilizpoanza, aliagiza waandishi warudi ofisini.
“Kwa sababu mnaambiwa wanakuja kuchoma TBC, sasa kama wanakuja kuchoma sisi tungerushia wapo hayo ambayo tunaambiwa hatukurusha?” amehoji.
Vyombo vya habari vya kimataifa
Wakati wanahabari wa ndani wakilalamika kubanwa na mamlaka za Serikali, vyombo vya habari vya kimataifa viliendelea na kazi kama kawaida.
Awali Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) liliripoti maandamano yalipoanza Dar es Salaam maeneo ya Kimara, lakini ilipofika saa 7 intaneti ilizimwa.
Aljazeera nao waliendelea kuripoti matukio ya vurugu hata baada ya intaneti kufungwa. Baada ya intaneti kurejeshwa, BBC Swahili walitoa ripoti iliyoonyesha mkusanyiko wa matukio ya vurugu yakiwamo ya polisi wakiwafyatulia risasi waandamaji, huku pia wakionyesha maiti zilizodaiwa kukusanywa.
Katika ripoti hiyo, BBC walidai kuthibitisha uhalali wa picha na video kwa kutumia teknolojia ya satelaiti. Walidai kuzitafuta mamlaka za Tanzania kufafanua lakini hawakupata ushirikiano.
Novemba 21, CNN nao walitoa ripoti yao wakionyesha mfululizo wa makabiliano kati ya polisi wenye sare na wasio na sare na waandamanaji. Walidai kuthibitisha picha na video kwa kutumia satelaiti na pia walidai kuzitafuta mamlaka za Serikali lakini hazikujibu.
Ripoti hizo ziliibua mjadala mkali ndani na nje ya nchi, hadi Novemba 23, Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa alipokuja kulalamikia mashirika ya habari ya kimataifa ya BBC, CNN, Aljazeera na DW kwa kutoa habari hizo bila kutafuta upande wa Serikali.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Msigwa aliwapongeza wanahabari wa Tanzania, akidai kuwa wameripoti vizuri habari za vurugu za uchaguzi.
