
Ripota, Wino Tanzania.
Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Bakari Steven Machumu kuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, akichukua nafasi ya Sharifa Bakari Nyanga ambaye amepangiwa majukumu mengine.
Machumu ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni ya BSM Washauri, ni mwanahabari mkongwe aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa kampuni ya Mwananchi Communications Ltd inayochapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dkt. Moses M. Kusiluka leo Novemba 19, imesema pia Rais Samia amemteua mwanahabari mkongwe Tido Mhando aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Azam Media, Mwananchi Communications Ltd na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC).
Kabla ya hapo aliwahi kufanya kazi Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) kabla ya kwenda kufanya kazi Shirika la Utangazaji la Kenya (KBC) na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).
Balozi Kusiluka pia amesema Rais Samia ameteua mbunge na waziri wa zamani, Lazaro Nyalandu kuwa Balozi. Nyalandu amewahi kuwa Mbunge wa Singida Kaskazini kwa vipindi kadhaa na amewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii.
