
Wino Ripota.
Novemba 14 baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutangaza baraza jipya la mawaziri, macho na masikio yameelekezwa katika majina yanayounda baraza hilo.
Miongoni, mwa sura mpya ni Rahma Riyadh Kisuo, aliyeteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Wizara mpya ya Kazi, Ajira na Mahusiano.
Kilichowavutia wengi kwa jina hili ni majukumu aliyopewa, umri wake mdogo na uchanga wake katika siasa.
Hata hivyo wakati wengi wakidhani ni mchanga katika siasa, Rahma alianza harakati zake chini kwa chini akianzia katika asasi za kiraia za vijana.
Rahma Riyadh Kisuo ni nani?
Akiwa na umri wa miaka 22 pekee, Rahma aliandika kitabu cha dini kwa ajili ya wasichana wa Kitanzania. Zaidi ya hapo, alianzisha jukwaa kubwa la vijana linalolenga maendeleo ya kisiasa kwa vijana mwaka 2019, lijulikanalo kama Muungano Plus/Positive.
Lengo kuu la jukwaa hilo ni kufanya mijadala ya pamoja na wadau kuhusu faida na manufaa chanya ya Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar. Walengwa wakuu wa mijadala hii ni wanafunzi wa vyuo vikuu, kwa ajili ya kupima uelewa wao kuhusu Muungano huu na kuchochea ubunifu wao katika kuimarisha na kuendeleza Muungano huo.
Rahma pia ameandaa tamasha la Taarab pamoja na chakula cha jioni kwa ajili ya hisani, ambalo lilianza mwaka 2020 katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam. Tamasha hili linalenga kuheshimu urithi wetu wa muziki unaotutambulisha kama Watanzania katika jukwaa la kimataifa, sambamba na kuwa jukwaa la ukusanyaji wa fedha kwa ajili ya kusaidia shughuli mbalimbali za kijamii.

Mwaka 2020, Rahma alielekeza fedha hizo kununua vifaa vya msingi vya kujifungulia akina mama katika wodi ya wazazi ya Hospitali ya Amana, Dar es Salaam. Mwaka uliofuata, 2021, tamasha lililofanyika Zanzibar lilichangia ujenzi wa vyoo vya shule huko Pemba. Aidha, tamasha la mwaka 2023 la Taarab With Dinner Charity Night liliwezesha upatikanaji wa vifaa vya usafi binafsi kwa wanawake wafungwa katika gereza la Segerea, Dar es Salaam.
Kupitia Shiraz Foundation mwaka 2023, Rahma alizindua jukwaa muhimu lijulikanalo kama Kigoda Cha Wasichana, kwa ajili ya kuwawezesha wasichana kwa kujadili changamoto zao na kuwapatia fursa. Tukio la kwanza lilifanyika tarehe 1 Oktoba 2023 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) likihudhuriwa na wasichana 1500 kutoka maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam.
Rahma pia anapanga kuanzisha jukwaa kubwa la kidijitali la wasichana lijulikanalo kama AJIRAKADA APP, lenye lengo la kuwawezesha na kuwatia nguvu wasichana wa Kitanzania.
Rahma ni kijana mwenye kujituma na mjasiriamali anayeimiliki chapa ya mavazi iitwayo Shiraz Designs, yenye makao yake katika jengo la Dar Free Market, Oysterbay, Dar es Salaam.
Rahma pia ni Wakili wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, na amepata mafunzo ya kidiplomasia katika ngazi ya stashahada ya juu katika Kituo cha Mahusiano ya Kimataifa (Centre for Foreign Relations) jijini Dar es Salaam. Aidha, anashikilia Shahada ya Uzamili ya Biashara ya Kimataifa (Master of International Business) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Pamoja na jina lake kutokuwa maarufu katika medani za siasa, huenda wasifu huu ndicho chanzo cha kuwekwa katika wizara nyeti ya mahusiano akisaidiana na Clement Sangu.
Rahma mwenye umri wa miaka 29, ni wakili wa Mahakama Kuu ya Zanzibar. Kielimu ana shahada ya uzamili ya Diplomasia aliyoipata katika Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim (Centre for Foreign Relations) jijini Dar es Salaam, na pia ana shahada ya uzamili ya Biashara ya Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Pia ni Mbunge wa Viti Maalum na Mtetezi wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGO’s)
