
Mwandishi wetu
Rais Samia Suluhu Hassan ametangaza Baraza lake la Mawaziri 56 watakaohudumia wizara 27. Bara hilo limetangazwa Novemba 17, kufuatia uchaguzi mkuu wa Oktoba 29 wenye utata, uliogubikwa na vurugu za maandamano ya vijana katika mikoa mbalimbali nchini
Licha ya maandamano na vurugu hizo zilizosababisha mauaji, watu kujeruhiwa na mali za Serikali na watu binafsi kuharibiwa, Rais Samia, akatangazwa kuwa mshindi kwa asilimia 97.6, akifuatiwa kwa mbali na wapinzani wake.
Awali Rais Samia alipozungumzia vurugu zilizoanza Oktoba 29, alidai kuwepo kwa watu kutoka nje ya nchi walioshiriki. Hata hivyo madai hayo ambayo pia yalitolewa na Jeshi la Polisi, hayajawahi kuthibitishwa.
Akihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano Novemba 14, Rais Samia alieleza kusikitishwa na vurugu hizo, huku akimwagiza Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kuwafutia makosa vijana waliokamatwa na kufunguliwa makossa ya uhaini na kufanya vurugu kulingana na uzito wa makossa yao.
Rais Samia aliahidi kuunda wizara ya vijana ili kushughulikia changamoto zao. Wizara hiyo kweli imeundwa na iko chini ya Ofisi ya Rais.

Ukubwa wa Baraza la Mawaziri
Mjadala huu utajikita kwenye muundo wa Baraza la Mawaziri na hali ya sasa ya siasa. Je, Rais ameisoma hali ya siasa kabla ya kuunda baraza hili? Huu ulikuwa wakati wa kuunda baraza kubwa lenye mawaziri 57? Kuundwa kwa Wizara ya Nchi, Maendeleo ya Vijana ndio kutamaliza malalamiko ya vijana?
Kwanza, kwa hali ya sasa ya kisiasa na kwa lengo la kufanya maridhiano na vijana ambao wengi wao walihusika kwenye maandamano, hakukuwa na sababu ya kuunda baraza kubwa kiasi hiki. Tanzania yenye idadi ya watu Zaidi ya milioni 61, mawaziri 57 ni wa kazi gani?
Chukua mfano wa nchi tajiri duniani, tukianza na Marekani yenye watu milioni 341 Serikali yake ina mawaziri 25, ambapo manaibu wapo 10. Ufaransa yenye watu milioni 68 ina mawaziri 34, Japan yenye watu milioni 123.1 ina mawaziri 17 tu.
Hivi ni nchi tajiri ziazotupa misaada kila mara, lakini wamejitahidi kupunguza ukubwa wa Serikali zao na kuwekeza Zaidi kwenye maendeleo. Sisi nchi masikini, tunawekeza Zaidi kwenye ukubwa wa Serikali kuliko maendeleo.
Tukumbuke kuwa kumhudumia waziri mmoja tangu kumlipa mshahara, marupurupu ya safari na vikao, bado apewe gari na nyumba, ni gharama kubwa. Kwa hiyo Rais Samia amechagua kuwekeza Zaidi kwenye kuigharamia Zaidi Serikali kuliko hata wananchi.
Kwa ukubwa huu wa baraza la mawaziri, hata kuundwa kwa Wizara ya vijana kunapoteza maana. Kwa sababu kero kubw aya vijana ni ubora wa maisha. Vijana wanataka mitaji ya biashara, wanataka mifumo bora ya kujiajiri, wanataka ajira serikalini na kwenye sekta binafsi. Hayo yote yangeweza kufanya bila hata kuunda wizara.
Wizara ya Vijana
Maandamano ya Oktoba 29, yametoa picha kamili kwamba vijana wamechoshwa na ahadi za Serikali ya CCM kila mara ambazo hazitekelezeki. Ndio maana walikuwa tayari kutoka licha ya tishio la majeshi ya ulinzi na usalama, licha ya kuwepo kwa risasi za moto, licha ya mabomu ya machozi.
Hivyo, kipaumbele cha Rais Samia kinapaswa kuwa ni kuwawezesha vijana kupata hali bora za maisha. Lakini tukiangalia mapato ya Serikali kwa mwaka, ni ngumu kuwatimizia vijana mahitaji yao. Ikiwa Bajeti ya Serikali inategemea wafadhili kwa Zaidi ya asilimia 30, maana yake kama nchi bado hatujaweza kujitosheleza.
Rais Samia alipaswa kufikiria kupunguza matumizi ya Serikali: kwanza kupunguza ukubwa wa baraza la mawaziri na kubakiza angalau mawaziri 25 tu, halafu apunguza matumizi ya magari ya kifahari na pia apunguze posho na marupurupo kwa wabunge.
Fedha zitakazopatikana hapo azipeleke kwenye sekta zinazoajiri vijana kwa wingi. Wapewe mitaji kwa masharti nafuu. Kama ni kilimo wajiajiri huko, kama ni wafanyabiashara wapewe, na hata viwandani nako wapewe nafasi. Bila kufanya hivyo, malalamiko ya vijana hayataisha.
Upendeleo
Jambo la pili, muundo wa baraza hili una sura ya upendeleo. Rais ameonyesha upendeleo kwa familia yake na marafiki zake. Kuna minong’ono kuhusu uteuzi wa biti yake, Wanu Hafid Ameir kuwa Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, huku mumewe, Mohamed Mchengerwa akiwa Waziri wa Afya.
Hii si minong’ono ya bure na kwa kuzingatia yaliyotokea Oktoba 29, Rais Samia angepaswa kujiepusha nayo kabisa. Lakini inaonyesha bado Rais amelala usingizi, au ameziba masikio. Ni kweli anaweza kujitetea kwamba hao aliowateua wana sifa, lakini kwani kulikuwa na ulazima wa kumteua binti yake tena kwenye hali tete kiasi hiki? Kulikuwa na haja ya kuwaweka watoto wa marais wastaafu au ndugu jamaa na marafiki?
Akilihutubia Bunge Novemba 14, Rais Samia alisema vijana wengi walioandamana Oktoba 29, walikuwa wanafuata mkumbo, hivyo akasema Serikali imeunda Tume kuchunguza chanzo cha vurugu. Sasa hapo unachunguza nini, wakati sababu ziko wazi? Upendeleo kama huu ndio unazaa manung’uniko na ndio chanzo cha vijana kulalamika na hatimaye kuandamana.
Kwa dhana hii ya upandeleo, baraza limekuwa kubwa kwa sababu Rais anaona ndio sehemu ya kuwazawadia watu wake wanaomsifu na kumtukuza kila kukicha, hata kama wananchi hawawapendi. Hataishia hapo, ataendelea kuwateua watu hao wanaojipendekeza kwenye nafasi mbalimbali.
Manung’uniko kama haya yalikuwepo pia nchi ya Malawi, ambapo aliyekuwa Rais Lazarus Chakwera alilaumiwa kuteua ndugu jamaa na marafiki katika Serikali yake. Miongoni mwa mambo yaliyomfanya ashindwe uchaguzi wa mwaka huu ni pamoja na hilo.
Tatu, ni suala la mgawanyo wa mawaziri kwa kuzingatia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Kuna watu wanahoji, kwa nini Zanzibar iwe na Serikali yake na Rais wake na baraza la mawaziri, halafu baadhi ya Wanzibari wanateuliwa tena kuwa mawaziri katika Serikali ya Muungano?
Tumeona kwa mfano, mawaziri walioteuliwa katika baraza hilo wakipewa nafasi nyeti, kama Wizara ya Fedha na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Hayo ni baadhi ya mambo yanayolalamikiwa au ndio kero za Muungano wetu na ishara ya malalamiko ndio hayo maandamano yaliyotokea.
Kwa hiyo Rais Samia alipaswa kutambua mapema, wakati alionao sio wakati salama sana wa kujiachia kama ilivyokuwa kwa marais wengine. Akumbuke kwamba, kwa mara ya kwanza Watanzania wameandamana siku ya uchaguzi mkuu tangu nchi ilipopata uhuru mwaka 1961.
Vurugu hizo hazitamalizwa kwa mtutu wa bunduki tu, bali ni kwa kusikiliza malalamiko ya wananchi na kuyafanyia kazi.
