
Mwandishi wetu,
Wakati ahadi ya maridhiano iliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan ili ikisubiriwa kutekelezwa, swali kubwa limekuwa, Je, ataanzia wapi?
Katika kampeni za uchaguzi mkuu mwaka huu, Rais Samia aliahidi kuunda Tume ya Maridhiano na upatanisho itakayozungumza na wadau wa siasa, sekta binafsi na asasi za kiraia, ikiwa ni njia kuelekea kwenye kupata Katiba mpya.
Ahadi hiyo inasubiriwa kwa hamu kutokana na vurugu zilizotokana na maandamano yaliyoanza Oktoba 29 hadi 31, 2025 yaliyosababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali za watu binafsi na za Serikali.
Akizungumzia katika Mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), aliomwakilisha Rais Samia kwa njia ya mtandao, Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi alisema Serikali imejizatiti kulinda amani na umoja na kwamba kwa sasa watajikita kwenye maridhiano.
Hata hivyo, baada tu ya uchaguzi kwisha, mamia ya vijana wamekamatwa na kufunguliwa kesi za uhaini, unyang’anyi wa kutumia silaha na uharibifu wa mali, hali inayozua hofu ya kutekelezeka kwa maridhiano hayo.
Kwa mujibu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), jumla ya vijana 641 wamefikishwa mahakakamani na kufunguliwa kesi za uhaini, unyang’anyi wa kutumia silaha na kufanya vurugu, huku mamia wengine wakishikiliwa kwenye vituo vya polisi, wengi wakiwa ni vijana wenye umri kati ya miaka 19 hadi 25.
Akizungumza na waandishi wa habri Novemba 11, jijini Dar es Salaam, Wakili Maduhu William, ameitaja mikoa yenye watuhumiwa hao kuwa ni Dar es Salaam (400), Dodoma (32), Iringa (89), Mara, Mwanza (200), Kilimanjaro (12), Tabora (5) Arusha (60), Njombe (10), Songwe (200) na Kigoma (11) na Mbeya (300).
Endapo vijana hao watatiwa hatiani kwa makossa hayo, adhabu yao ni kinyongwa hadi kufa, kifungo cha maisha au miaka 30 kutegemea na makosa.
Kesi hizo zinaendelea, huku kukiwa na giza nene kuhusu madhila yaliyotokana na maandamano vikiwemo vifo, ambavyo mpaka sasa Serikali haijataja idadi wala hata kukiri, majeruhi.
Pia kumekuwa na maswali mengi kuhusu mwenendo mzima wa uchaguzi mkuu uliompa ushindi Rais Samia wa asilimia 97.6, akiwaacha mbali wapinzani walioambulia kura chini ya asilimia 10.
Maridhiano yanaanzaje?
Mhadhiri wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda anasema kulingana na jinsi uchaguzi ulivyokwenda, matokeo yaliyotolewa yana utata, hivyo maridhiano hayakwepeki ili kuweka mambo sawa.
“Kwa kuangalia uchaguzi ulivyoendeshwa, awali ulikuwa halali kisheria, sio kisiasa. Tangu vituo vilipofunguliwa saa 1 asubuhi hadi saa 5 hali ilikuwa shwari maeneo mengi, lakini baada ya hapo yalitokea maandamano kwenye mikoa Zaidi ya 10 na kuvuruga kabisa upigaji kura.
“Kifungu cha 88 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani kinasema ikiwa uchaguzi utavurugwa, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) itarudia kwenye maeneo yaliyovurugwa. Sasa kama uchaguzi haukurudiwa, utasemaje ulikuwa huru na wa haki? Kwa maana hiyo, uchaguzi huu haukuwa na mshindi,” amesema.
Ameshauri kuanza haraka kwa mchakato wa maridhiano hasa kwa makundi yaliyokuwa yakiulalamikia uchaguzi wakiwamo CHADEMA na ACT Wazalendo ambao mgombea wao wa urais, Luhaga Mpina alienguliwa.
“Kwa kuwa Rais Samia aliahidi kuunda Tume ya Maridhiano, maana yake alishaona kuna tatizo. Awali nilishauri atafute maridhiano hayo kabla ya uchaguzi, lakini hata hivyo, bado anaweza kuanza mapema, kwanza kwa kuwafutia kesi viongozi wa vyama akiwamo Tundu Lissu.
“Pili, iundwe Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa kuwapa nafasi vyama vya upinzani serikalini. Kwa mfano wanaweza kuwapa hata nafasi za uteuzi kama wakuu wa mikoa na wilaya. Watoe hata ¼ ya nafasi hizo. Hiyo itapunguza shinikizo kubwa lililopo sasa,” amesema.
Hata hivyo, mchambuzi mwingine wa siasa, aliyeomba asitajwe jina, amesema hatua ya Serikali kuwakamata na kuwahsitaki vijana wanaodaiwa kushiriki maandamano ni hatua ya kuonyesha umwamba waati ikielekea kwenye maridhiano.
Ametoa mfano wa vita ya Russia na Ukraine, akisema Russia inakamata maeneo kwa mpinzani wake, ili hata wakienda kwenye mazungumzo awe na nguvu ya kufanya maamuzi.
“Hiyo inaitwa madman theory (nadharia ya ukichaa), ukiwa dhaifu utapoteza kwenye mea ya maridhiano,” amesema.
Kuachiliwa kwa viongozi wa CHADEMA
Licha ya Jeshi la Polisi kuwasaka na kuwakamata viongozi wa CHADEMA, Novemba 10 walimwachia huru Makamu Mwenyekiti, John Heche aliyekuwa akishikiliwa tangu Oktoba 22, 2025 katika mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma.
Pamoja naye, viongozi wengine waliokamatwa Novemba 11, akiwamo Naibu Katibu Mkuu, Amani Golugwa, Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani, Jacob Boniface na Mjumbe wa Kamati Kuu Godbless Lema nao waliachiliwa kwa dhamana.
Kuachiliwa huko kunatajwa kuwa njia za kuanza kuwalainisha wapinzani ili wakubali kushiriki mazungumzo ya maridhiano.
Hata hivyo, akizungumza Novemba 11, wakati wakienda kuripoti katika kituo kikuu cha Polisi cha Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Heche alisema, mpaka wanaachiliwa hawakuwa wameelezwa kosa lao la kukamatwa na wala hakukuwa na makubaliano yoyote.
“Hakuna mtu tuliyefanya naye mazungumzo yoyote, nataka liwe very clear kwenye public, kwa sababu kuna watu wanaleta propaganda kwamba tumechiwa kwa makubaliano Fulani, hakuna malubaliano tuliyoachiwa nayo,” amesema.
Kauli ya Heche imekuja wakati kukiwa na mijadala mitandaoni kuwa viongozi hao wameachiliwa ikiwa ni sehemu ya CCM kutafuta maridhiano na CHADEMA.
Minong’ono hiyo pia ilikolezwa na hatua ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu kutofikishwa mahakamani kusikiliza kesi ya uhaini inayomkabili, kwa kile kilichoelezwa na mawakili wa Jamhuri kuwa ni kukosekana kwa usalama.
Licha ya Heche kusema kuwa hakuna makubaliano yoyote, taarifa kutoka kwa vyanzo vya uhakika zinasema kuwa kumekuwa na juhudi za Serikali ya CCM kutafuta maridhiano na CHADEMA, kupitia kwa Lissu kwa ahadi ya kumfutia kesi yake, lakini mwenyewe amegoma.
“Juhudi za kutafuta maridhiano zimeanza muda mrefu, hata Lissu mwenyewe alishasema mahakamani kuwa kuna watu walimfuata gerezani wakimwahidi kumfutia kesi lakini akitoka aondoke nchini na alikataa.
“Lissu hayuko tayari kupokea vyeo vya kupewa ili afutiwe kesi wakati Watanzania wameuawa na lwengine kujeruhiwa, huo utakuwa ni usaliti,” alisema mmoja wa maofisa CHADEMA ambaye hakutaka kutajwa jina lake.
Hata hivyo, kauli ya Heche imekuja pia kupoza joto la wananchi hasa kundi la vijana linalounga mkono maandamano yaliyoanza Oktoba 29, 2025 maarufu GEN-Z ambalo licha ya kutojulikana uongozi wake, limeonekana kupinga maridhiano bila kuwahusisha.
Kundo hilo ambalo pia linaratibiwa na wanaharakati wa mitandaoni wanaoishi nje ya nchi, akiwamo Mange Kimambi anayeishi Marekani na Maria Sarungi anayeishi ncini Kenya.
