

Mwandishi wetu
Wakati Tanzania ikitajwa kuwa miongoni mwa nchi kadhaa duniani zenye mfumo wa usafiri wa mabasi ya mwendo wa haraka (BRT), utekelezaji wake umekuwa kizungumkuti kiasi cha kukiweka katika wakati mgumu Chama cha Mapinduzi (CCM), hasa wakati huu wa uchaguzi mkuu wa 2025.
Mbali na Tanzania, nchi nyingine za Afrika zenye BRT ni pamoja na Afrika Kusini katika miji ya Johannesburg, Cape Town, Pretoria, Nigeria katika jiji la Lagos, wakati katika nchi ya Senegal mradi upo katika jiji la Dakar na kwa nchi ya Cameroon mradi upo Douala.
Nchi nyingine ni China, Indonesia, India, South Korea, Taiwan, Jordan, Colombia, Brazil, Mexico,
Ecuador, Marekani, Canada, Australia, Ufaransa, Uholanzi, Uingereza na Ujerumani.
Tangu kuanza rasmi Mei 10, 2016 kwa mradi wa mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam, zaidi ya nchi tano za Afrika zimetuma viongozi wake kujifunza namna ya uendeshaji wake.
Mfumo huo ulizinduliwa na Hayati Rais John Magufuli Januari 17, 2017, ukilenga kupunguza foleni katika barabara za jiji hilo linaokua kwa kasi.
Usafiri huo ulivutia baadhi ya mataifa yakiwamo ya Ethiopia, Malawi, Uganda na Kenya na Rwanda yaliyotuma maofisa wao kuja kujifunza Tanzania.
Licha ya ya kuwa na abiria wengi kutoka Kimara hadi katikati ya jiji, mradi huo unaonekana kusuasua, kwani utoaji wa huduma umeshindwa kukidhi mahitaji ya abiria hao
Matokeo yake abiria hao hutumia muda mrefu kusubiri mabasi vituoni na hata mabasi yakifika yanakuwa yameojaa.
Imekuwa kawaida sasa kuona mabasi yanayotoka kituo cha Kimara mwisho yakiwa yamejaa kiasi cha milango kubaki wazi kinyume na utaratibu.
Wakati uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 ukiendelea kwa wagombea kufaya kampeni, usafiri huo sasa umeonyesha wazi aibu ya CCM inayoshindwa kutekeleza ahadi yake ya kukamilisha mradi huo kama ilivyojiwa.
Maelezo ya RC Chalamila
Kutokana na kero hiyo, Julai 24, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alitembelea mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) katika kituo cha Kimara Mwisho na alikiri kuwa huduma mbovu za mradi huo zinahujumu juhudi za serikali za kuboresha usafi ri kwa wananchi wa Dar es Salaam.
Chalamila alisema huduma za kampuni ya mabasi hayo (UDART) zimekuwa zikidorora tangu zilipoanzishwa miaka tisa iliyopita na wananchi wanakosa huduma bora ya usafiri wa mabasi ya mwendokasi.
“Mradi wa awali wa mwendokasi ulikuwa na urefu wa kilometa 20 ukijumuisha barabara ya Kivukoni, Kimara na Gerezani uliogharimu Sh bilioni 613 na ulipoanza mabasi 200 yaliletwa lakini hadi sasa mabasi yanayofanya kazi yamepungua na kubaki 60 tu hali inayowaumiza wananchi,” alisema.
Aliongeza: “Miaka tisa hamjabadilisha magari, hata mtu binafsi tu gari la miaka tisa limeshachakaa, lakini hili ni basi la abiria linakwenda linarudi, miaka tisa hamjawahi kubadilisha gari…mnasubiri mpaka gari linyeshewe ndani, livunje mavioo kila kitu halafu ninyi ndio muagize mabasi, hiyo si dharau kwa Watanzania? Hivi tukisema mnafaa kuendesha, mnafaa kweli UDART? Kwa sababu hii mwendokasi imepoteza hata ladha”.
Chalamila alisema kama UDART itakuwa miongoni mwa kampuni zilizopewa fursa ya kutoa huduma ya usafiri wa mwendokasi, yeye atapendekeza wasipewe kazi hiyo.
Alisema kampuni ya TransDar inatarajiwa kuanza kutoa huduma ifikapo Oktoba Mosi mwaka huu kwa kuingiza mabasi mapya 177 yatakayofanya safari katika maeneo yenye changamoto kubwa ya usafiri.
Kuhusu awamu ya pili ya mradi huo, Chalamila alisema serikali imekamilisha mradi wa awamu ya pili wa barabara yenye urefu wa kilometa 20.3 kutoka Halmashauri ya Jiji hadi Mbagala Rangi Tatu na ujenzi unaendelea kwenye daraja la Kigogo unaogharimu Sh bilioni 363.6.
“Serikali imeingia ubia na sekta binafsi kuongeza ushindani. Tayari tumefikia makubaliano na Kampuni ya Mofat ambayo italeta mabasi 200 ya kisasa yenye urefu wa meta 18 yatakayotumia gesi. Kati ya hayo, mabasi 99 yatakuwa yamewasili nchini ifikapo Agosti 15 na yataanza kutoa huduma kabla ya Agosti 30,” alisema.
Kuhusu awamu ya tatu, Chalamila alisema barabara yenye urefu wa kilometa 23.6 kutoka Halmashauri ya Jiji kupitia Tazara hadi Gongo la Mboto, ujenzi umefikia asilimia 85 na itakapokuwa tayari serikali itatangaza zabuni kumpata mtoa huduma ili kuongeza ufanisi.
Katika awamu ya nne alisema ujenzi wa barabara ya Tegeta–Mwenge hadi Bagamoyo yenye urefu wa kilometa 30.1 umefikia asilimia 30 na ikikamilika itatangazwa zabuni kupata waendeshaji.
Mambo yaibuka upya
Licha ya kauli za RC Chalamila, mambo yamezidi kuwa mabaya, kwani abiria wameendelea kulalamikia huduma mbovu za mabasi hayo. Katika video moja iliyorushwa Septemba 28, 2025 abiria walionekana wakiwa wamejaza basi kiasi cha kutoa vichwa madirishani na kwenye dari, huku wengine wakiwa wameninginia milangoni.
Basi hilo lilisimamsihwa na polisi katika Mtaa wa Msimbazi na kuwashusha abiria hao waliokuwa wakiimba “Hatumtaki, Hatumtaki,” japo haikujulikana walimaanisha kwamba hawamtaki nani.
Septemba 30, ilionekana video nyingine ikionyesha basi likiwa limejaa na abiria wakiimba, “Hatuitaki CCM hatuitaki CCM.”
Kutokana na hali hiyo, Oktoba Mosi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alifika tena Kimara Mwisho kushuhudia adha ya usafiri na malalamiko ya abiria.
Akiwa hapo, Chalamila amewaomba radhi wananchi wanaotumia mabasi hayo, huku akisisitiza kuwa hakuna serikali ambayo ina nia mbaya ya kuwadhuru wananchi wake.
Amegusia video zilizotolewa zikionuesha kwamba baadhi ya watu hawaitaki CCM, akisema hizo ni hasira za muda mfupi na mara serikali itakapokuwa imeingiza mabasi haya barabarani, kero hiyo itakuwa imekwisha kabisa.
Amesema kwa sasa wanaangalia uwezekano wa mabasi machache ya mwendokasi ya njia ya Mbagala yahamishiwe kwenye njia ya Kimara ili kuondoa kero kubwa wanayopitia Abiria wa Kimara kwa sasa.
“Serikali imetambua uchakavu wa Mabasi yale ya UDART na kwa mantiki hiyo imeidhinisha pesa kidogo ili yale Mabasi yaliyokwama yatengenezwe ili yaokoa changamoto iliyopo sasa, naamini mpaka mwezi wa 11 hapo yule Mtoa huduma aliyepata tenda hiyo atakuwa tayari ameshaanza kuingiza Mabasi,” amesema.
Rais awatengua mabosi DART/UDART
Wakati hayo yakiendelea Oktoba 2 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kupitia taarifa yake kwa umma alitangaza kuwaondowa kazini wakuu wa Wakala wa Mabasi ya Mwendokasi, DART, Mtendaji Mkuu Athumani Kihamia na Mkurugenzi Mkuu Waziri Kindamba na nafasi zao kuchukuliwa na Saidi Tunda Habibu na Pius Andrew Ng’ingo.
Kadhalika siku hiyo hiyo ya Oktoba 2, mabasi mengine mapya ya mwendokasi yenye rangi ya kijani yalianza kufanya safari katika maeneo unakopita usafiri huo.
Serikali inakwama wapi?
Akizungumzia mkwamo huo, Profesa wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Abel Kinyondo, amesema kwa ujumla mradi huo unasimamiwa vibaya na huenda kuna hujuma.
“Usimamizi mbaya unaanzia kwenye bodi ya UDART na menejimenti na watendaji wote, maana haiwezekani ukawa na biashara yenye wateja wengi, halafu ushindwe kuiendesha,” amesema.
Kuhusu upungufu wa mabasi, Profesa Kinyondo amesema sio sababu, kwani walipaswa kutumia mabasi waliyoanza nayo kukuza mtaji na kununua mengine.
“Wanasema mabasi ni machache, lakini pia wanasema mengine yameharibika, sasa kwa nini kusiwe na mpango wa kuyakarabati mabasi hayo ili yaendelee kufanya kazi? Faida inayopatikana ni lazima ipangwe kufanya ukarabati na kununua manasi mengine.
“Ndivyo zinavyofanya pia kampuni za mabasi, kwamba zinauza magari makukuu na kununua mapya na biashara zinaendelea vizuri,” amesema.
Amesema kuna uwezekano pia wa hujuma, ili kuonyesha kuwa mradi umeshindikana kwa lengo la kupata masilahi yao binafsi.
Aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa DART, Dk Kihamia alipoulizwa kuhusu hujuma au kama kuna mpango wa kumaliza kero zote zinazolalamikiwa, amesema maswali yote aulizwe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Chalamila.
Kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter), Mbunge na Waziri mstaafu, Profesa Anna Tibaijuka amehoji sababu ya usafiri huo kuwa kero badala ya kuwa mkombozi.
“Kulikoni kugeuka kero kubwa badala ya ukombozi? Tutambue usafiri wa umma si biashara ya faida. Ni huduma,” amesema.
Profesa Tibaijuka aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa (UN- Habitat), amesema nchi za Ulaya hutoa ruzuku kwa usafiri huo
“Ulaya serikali hutoa ruzuku. Asia waendeshaji makini ufidia kwa umiliki majengo karibu na vituo. Ukiuacha ujifadhili wenyewe, ati sijui kuna mwekezaji ni vigumu kufanikiwa. Tuutafakari upya. Misingi yake inajulikana ili mradi izingatiwe,” amesema.
Ahadi mpya za kampeni
Akiwa mgeni rasmi katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni za udiwani Kata ya Kimara, Mtaa wa Kirunge, mgombea ubunge wa Ubungo kupitia CCM, ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amewahakikishia wakazi wa eneo hilo na ukanda mzima wa Kimara hadi Manzese kuwa changamoto ya usafiri wa mwendokasi iko mbioni kupatiwa suluhu.
“Tunayo kero ya kutosha ya mwendokasi, inayosababushwa na upungufu wa mabasi ya mwendokasi. Jambo tunalitambua, linakera wananchi wetu, hususani wananchi kutoka Ubungo, Sinza, Manzese mpaka Magomeni na kwa kweli Dar es Saaam nzima kwa sababu hii ni barabara kubwa
Tunatambua kero hiyo na Serikali imechukua hatua kwa kuagiza mabasi 177 yanayotarajiwa kuingia mwishoni mwa mwezi huu ama mwanzoni mwa Novemba, yapo kiwandani yakikamilika, kama ya wenzenu ya Mbagala yakija, wananchi wanashangaa yana kiyoyozi na intaneti, yatakuja pia Kimara,” alisema huku akishangiliwa na wananchi.
Alisema kinachochelewesha mabasi ni kwa kuwa hayatengenezwi nchini bali yanaagizwa na kalenda iliyotolewa ni mwishoni mwa Oktoba na mwanzoni mwa Novemba.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni katika jimbo la Kibamba jijini Dar es Salaam, mgombea mwenza wa urais kupitia CCM, Dk Emanuel Nchimbi, amesema serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Dk Samia Suluhu Hassan serikali itashirikiana na watu binafsi wenye uwezo wa kununua na kuendesha mabasi ya mwendo wa haraka ili kuhakikisha barabara zinakuwa na mabasi ya kutosha na wananchi wanasafiri kwa usalama na ustawi.
Dk Nchimbi alisema tayari serikali imetenga fedha za kukarabati mabasi ya mwendokasi yaliyoharibika ili yarudi barabarani kwa ubora kama mapya, huku sekta binafsi ikitarajiwa kuingiza mabasi 177 mapya kwa lengo la kupunguza changamoto za usafiri wa mwendokasi.
