Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Samia Suluhu Hassan
Mwandishi wetu,
Zimepita wiki nne tangu kampeni za uchaguzi mkuu wa 2025 zilipozinduliwa Agosti 28, 2025, hata hivyo vyama vya upinzani, vinaonekana kushindwa kufurukuta mbele ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Katika uchaguzi huo, CCM inashindana na vyama 17, vikiwAmo vikubwa vya ACT Wazalendo na CHAUMMA.
Vingine ambavyo hata hivyo havipewi umuhimu mkubwa kutokana na uchanga wake ni pamoja na NLD, NRA, UMD, UDP, UPDP, DP, CUF, SAU, DEMOKRASIA MAKINI, AAFP, TLP, NCCR Mageuzi, ADA TADEA, CCK, ADC.
Kama ilivyotarajiwa, CHADEMA hawakushiriki uchaguzi huo, kutokana na kampeni yao ya No Reforms No Election (hakuna mabadiliko, hakuna uchaguzi).
Wakati huo, Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu anakabiliwa na kesi ya uhaini mahakamani, huku chama hicho pia kikikabiliwa na kesi ya madai iliyofunguliwa na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Said Issa Mohamed na wenzake wawili na hivyo chama hicho kuzuiwa kufanya kazi zake.
CHADEMA ambacho ni chama kikuu cha upinzani, kilitarajia kuleta upinzani mkali kama kingeshiriki uchaguzi huo. Miongoni mwa maeneo ambayo chama hicho kina nguvu ni pamoja na Kanda ya Ziwa yenye mikoa saba ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, Kagera, Geita, huku Kanda ya Kati kikiwa na nguvu sehemu ya Mkoa wa Singida.

CHADEMA pia ina nguvu pia Kanda ya Kaskazini hususani Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro. Pia kina nguvu Mkoa wa Dar es Salaam na Kanya ya Nyanda za Juu Kusini yenye mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe, Ruvuma na Sehemu ya Kanda ya Magharibi hasa Mikoa ya Rukwa na Katavi.
Ilitarajiwa kuwa vyama vya ACT Wazalendo na CHAUMMA vingeziba pengo la CHADEMA katika maeneo hayo, lakini vyama hivyo vimeshindwa kujitutumua.
ACT Wazalendo
Chama cha ACT Wazalendo kilichosajiliwa mwaka 2014 kilianzishwa na baadhi ya makada kutoka CHADEMA wakiongozwa na Zitto Kabwe, kilipata nguvu Zaidi mwaka 2019 baada ya Chama cha Wananchi (CUF) kumeguka kufuatia mzozo uliokuwepo kati ya Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba na aliyekuwa Katibu Mkuu, Hayati Maalim Seif Sharif Hamad.
Hivyo, Maalim Seif aliondoka na kundi lake wengi wakiwa Wazanzibari na kujiunga na ACT Wazalendo.
Mwaka huu chama hicho kilipata bahati ya kumpata aliyekuwa kada wa CCM, Luhaga Mpina na kumfanya kuwa mgombea wake wa urais, lakini akawekewa na mapingamizi na hatimaye akaenguliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
Hata hivyo, chama hicho kimejitutumua kikidai kuleta upinzani mkali kwa CCM, jambo ambalo halijaonekana tangu kampeni zilipoanza Agosti 28, 2025.
Chama hicho kimeonekana kuwa na ushawishi zaidi visiwani Zanzibar, mkoani Kigoma na baadhi ya majimbo ya Mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara.
Akizungumzia mwenendo wa kampeni ndani ya ACT Wazalendo, Septemba 22, 2025, Kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu amesema chama hicho kimejiimarisha nchi nzima kwa kusimamisha wagombea maeneo yote japo hakutaja idadi kamili ya wagombea.

“Tangu tumeanza kampeni, tumefika kata kwa kata na majimbo yote. Ni bahati mbaya tumefika kwenye uchaguzi tukiwa na hali hii,” amesema Semu akiashiria kuenguliwa kwa mgombea wao wa urais, Luhaga Mpina.
Alipoulizwa kama wameweza kuziba pengo la kutokuwepo kwa CHADEMA, Semu amesema kutokuwepo kwa CHADEMA sio fursa kwao, bali walitamani chama hicho kishiriki uchaguzi.
“Bahati mbaya tumefika kwenye uchaguzi tukiwa na hali mbaya tuliyonayo. Sisi na CHADEMA tumekuwa tukipigania kupata mabadiliko kwa njia mbalimbali na sisi tumeamua kushiriki uchaguzi. Wao kutopiga kura ni pigo kubwa.
“Hatuoni kama kutoshiriki kwenye uchaguzi kwa chama hicho ni fursa kwetu, sisi tulitamani wangekuwepo,” amesema.
CHAUMMA
Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kilichoanzishwa mwaka 2012 kilipata nguvu zaidi mwaka 2025 baada ya kundi la makada wa CHADEMA hasa wale waliokuwa wakimuunga mkono Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Freeman Mbowe kujiunga nacho.
Makada hao akiwemo aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Zanzibar, Salum Mwalimu na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu (Bara), Benson Kigaila walidai kutengwa ndani ya chama hicho, huku pia wakipinga uamuzi wa kutoshiriki uchaguzi mkuu wa Oktobva 29, chini ya kampeni ya No Reforms No Election.
Makada hao walitamba kwamba wanakwenda kuendeleza kazi walizokuwa wakizifanya CHADEMA na kuiinua CHAUMMA kupitia uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Hata hivyo, wakati mwezi mmoja wa kampeni ukiisha, bado hawajaonyesha kuziba pengo kwenye ngome za CHADEMA.
Alipotafutwa kwa simu Septemba 22, Mkurugenzi wa Habari na Taarifa kwa Umma wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), John Mrema alisema yuko kwenye safari za kampeni, hivyo atafutwe jioni.
Hata alipotafutwa jioni, pia aliahidi kujibu maswali aliyotumiwa kupitia WhatsApp, jambo ambalo hakutekeleza, licha ya kukumbushwa Septemba 23.
Akizungumzia hali hiyo, mchambuzi wa siasa na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Faraja Krisostom ametaja mambo matatu yanayosababisha vyama hivyo vishingwe kufurukuta kwenye ngome za CHADEMA.
“Kwanza vyama hivyo havina mizizi kwenye maeneo mengi na hivyo haviwezi kutamba kwenye ngome za CHADEMA kwa urahisi, kwa sababu havikuwa vimejiandaa.
“Pili, aina ya watu waliomo kwenye vyama hivyo hawana ushawishi kwa wapiga kura kiasi cha kuwavutia na kuwaona kama chama mbadala, na tatu ni dhana iliyojengeka kwa wananchi kwamba, hivyo vyama vina watu wanaotumiwa na CCM,” amesema.
Kampeni za CCM
Kwa upande wa CCM waliozindua kampeni zao Kawe jijini Dar es Salaam, wameonekana wakifanya kampeni kwa nguvu, ikiwa pamoja na kuweka mabango makubwa ya wagombea wao katikati ya miji na kusomba watu kwa magari ili wajaze mikutano yao.
Akizungumzia kampeni hizo, Dk Krisostom amesema chama hicho kinafanya kampeni kwa nguvu ili kuuhalalisha uchaguzi huo.
“Kwa sababu kumekuwa na malalamiko ya kudai mabadiliko kabla ya uchaguzi, CCM wanataka kuhalalisha uchaguzi huu na ndio maana wanatumia nguvu kubwa kwa kuweka mabango na kukusanya watu wengi kwenye mikutano yao,” amesema.
Tishio la maandamano
Katikati ya kampeni hizo kumekuwa na tishio la kufanyika kwa maandamano, yakiwamo ya Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) na maandamano yanayoratibiwa na wanaharakati wa mitandao akiwamo Mange Kimambi.
Akihutubia katika mkutano wa hadhara wilayani Chackechake kisiwani Pemba mwisho wa wiki iliyopita, Rais Samia Suluhu Hassan, aliwaonya watu wanaotaka kuvuruga Amani akisema vyombo vya Dola viko imara kuwakabili.
“Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita hii tunayomaliza, tumejitajidi sana kusimamia utulivu wa kisiasa, usalama na Amani. Hamjasikia pepepe, mkisia labda ni ajali, imetokea labda wamekufa sita, wamekufa wangapi na labda mtu mwenyewe amekwenda kuchokoza na ameshughulikiwa, lakini hamjasikia vurugu katika nchi hii
“Hata wale waliovuka mipaka na kutaka kuleta vurugu ndani kwetu tuliwashughulikia na hawajathubutu kurudi tena,” alisema.
Akizungumzia tishio la maandamano hasa yanayopangwa kufanyika Oktoba 29, 2025, Krisostom anasema yanaweza yasifanikiwe kutokana na nguvu kubwa ya polisi iliyowekwa.
“Kwanza maandamano ya TLS yameshadorora kwa sababu wanaoandaa wenyewe wamegawanyika. Wapo makada wa CCM ambao hawayapendi, lakini pia polisi wameweka nguvu kubwa kuyapinga.
“Hayo maandamano ya mitandaoni, uzoefu unaonyesha huwa yanaishia huko huko mitandaoni,” amesema
