Mgombea urais wa ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina
Mwandishi Wetu, Wino Tanzania
Baada ya mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano kupitia chama cha ACT Wazalendo, Luhaga Mpina kushinda kesi aliyoifungua kupinga kuzuiwa kurejesha fomu zake katika Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) jijini Dodoma, sasa ameenguliwa kabisa baada ya tume hiyo kukubaliana na pingamizi la Serikali.
Mpina alizuiwa kurejesha fomu za kugombea urais, alipofika katika makao makuu ya INEC jijini Dodoma Agosti 28, 2025 na kuzuiwa kuingia kwenye lango la ofisi hiyo, akiambiwa kuwa tume imepata barua kutoka Msajili wa Vyama vya Siasa.
Awali, Mpina aliyetangazwa kuwa mgombea urais wa chama hicho Agosti 6, 2025 alilalamikiwa na kada wa chama hicho, Monalisa Ndala akidai kuwa Mpina hakuwa na sifa ya kugombea kwa amekiuka kanuni za chama hicho ikiwemo ya kuwa mwanachama angalau mwezi mmoja kabla ya kugombea nafasi hiyo.
Monalisa alipeleka malalamiko yake kwa Ofisi ya Msajili wa vyama vya Siasa, ambaye naye alikitaka chama hicho kujibu.
Ndipo Agosti 26, 2025 alipotoa uamuzi, akikubaliana na malalamiko ya Monalisa na hivyo Mpina akatajwa kutokuwa na sifa ya kuwa mgombea.
Hapo ndipo INEC ilipomkatalia kupokea fomu zake na yeye alishitaki mahakamani kupinga zuio hilo.
Septemba 11, 2025 Mahakama Kuu Masijala Kuu ya Dodoma iliyokuwa ikisikiliza kesi hiyo ilimpa ushindi Mpina na kuitaka INEC kupokea fomu za Mpina.
Mpina alirejesha fomu zake ofisi za INEC za Dar es Salaam Septemba 13, 2025.
Mapingamizi mapya
Septemba 12, 2025 tayari INEC ilishapokea mapingamizi matatu kutoka wagombea urais wa NRA na AAFP na pingamizi lingine likitoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari.
Taarifa iliyotolewa na ACT Wazalendo, ilisema kuwa imeyapokea na inayajibu. Kama hiyo haitoshi, Mpina naye alimwekea pingamizi mgombea wa CCM, Samia Suluhu Hassan akidai kuwa alikiuka utaratibu wa kumteua kuwa mgombea katika chama chake.
Katika uamuzi wake wa Septemba 15, 2025, INEC ilisema imeketi kikao siku hiyo hiyo na kuyatupilia mapingamizi matatu, mawili yakiwa ni ya AAFP na NRA yaliyompinga mgombea urais wa ACT Wazalendo na pingamizi la Mpina aliloweka kwa mgombea urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan.
Hata hivyo, INEC ilikubaliana na pingamizi la AG Hamza Johari la kumpinga Mpina kuwa mgombea halali wa urais.

Hapo tena safari ya Mpina kugombea urais kupitia ACT Wazalendo ndio imekwisha.
Safari ya Mpina kutoka CCM
Tangu awali ilionekana kuwa Mpina hawezi kuishi CCM kwa amani na hapo ndipo alipotua ACT Wazalendo Agosti 4, 2025, zikiwa ni siku chache tu baada ya jina lake kukatwa kwenye kura za maoni za CCM.
Mpina aliyeingia bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2010 alionekana kuwa mchungu katika Bunge la 12 la Spika Dk Tulia Ackson.Luhaga Mpina, ACT-Wazalendo
Moto wake ulianza katika Bunge la 10 ambalo lilikuwa chini ya Spika Anne Makinda pale alipoamua kuigomea bajeti ya Serikali, kwa alichokieleza kuwa mambo hayakuwa yakienda sawa ikiwemo matumizi serikalini.
Aliyekuwa Waziri wa Fedha, marehemu Dk William Mgimwa alishindw akujibu hoja zake, jambo lililozua mjadala mrefu kiasi cha kutofikia mwafaka.
Katika Serikali ya awamu ya tano chini ya hayati John Magufuli, Mpina aliteuliwa kuwa Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira kabla ya kupewa jukumu la Waziri wa Mifugo na Uvuvi, anakokumbukwa kwa sakata la upimaji wa samaki kwa kutumia rula kwenye mgahawa wa Bunge jijini Dodomada ya a.
Baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani Machi 2021, Mpina hakuteuliwa kuwa Waziri na hivyo akaendeleza moto wake bungeni.
Baadhi ya mawaziri walimuona Mpina kama shubiri kutokana na hoja zinazowagusa katika wizara zao, ambazo nyingi huhitaji utulivu ili kuweza kulipatia jambo husika ufumbuzi wake bila kukurupuka.
Miongoni mwa mawaziri waliowahi kuingia ‘anga’ za Mpina ni wale wa sekta za fedha, ujenzi na miundombinu, kilimo, nishati na wa katiba na sheria.
Kutokana na mabomu anayoporomosha kwa mawaziri, Januari 2024, alisimamishwa kuhudhuria vikao 15 bungeni akidaiw akumdharais Spika Dk Tulia Ackson.
Hatua hiyo ilifikiwa baada ya Mpina kufikishwa kwenye Kamati Maadili, Haki na Madaraka ya Bunge kwa kosa la kumtuhumu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kuwa alilidanganya Bunge kuhusu sakata la kuagiza sukari nje.
Licha ya kwenda mahakamani kupinga hatua hiyo, Mpina pia hakufanikiwa, kwani mahakama ilisema haiwezi kuingilia madaraka ya Bunge.
Aliporudi Novemba 2024, Mpina aliendeleza moto wake kwa mwaziri, huku pia uhusiano wake na baadhi ya viongozi wa CCM ukidorora.
Matumaini ya Mpina kuendelea kuwa Mbunge wa Kisesa yalipotea, baada ya Rais Samia kufanya ziara mkoani Simiyu, ambapo akiwa Kisesa 17 Juni, 2025 alimkosoa mbunge huyo.
Rais Samia alisema mbunge huyo amekuwa akirukaruka na kwamba anafaa kuwa mbunge wa Taifa.
Wakati wa kura za maoni, kulikuwa na kila dalili za Mpina kuachwa na ndivyo ilivyotokea. Hapo ndipo alipojiondoa CCM na kwenda ACT Wazalendo.
