Mwandishi Wetu, Wino Tanzania
Dar es Salaam. Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania, (TAMWA) kimempongeza Mgombea urais kwa tiketi ya CCM,Samia Suluhu Hassan pamoja na wapeperusha bendera wanawake katika nafasi za ubunge na udiwani kwa kuonyesha nia ya kuwania nafasi za uongozi katika siasa.
Katika tamko lao TAMWA imempongeza mpeperusha bendera kwa tiketi ya CCM, Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mgombea wa kwanza mwanamke wa urais katika historia ya chama tawala.
“Hii ni hatua kubwa na ya kihistoria, inayoashiria mapinduzi na mwelekeo mpya wa ushiriki wa wanawake katika uongozi wa juu nchini.”limesema tamko hilo
Katika tamko hilo, TAMWA kadhalika imewapongeza wanawake wengine walioteuliwa kugombea urais pamoja na wagombea wenza akiwamo Mwajuma Noty Mirambo aliyechukua fomu ya kuwania urais kupitia Chama cha Union for Multiparty Democracy (UMD), akiwa na mgombea mwenza Mashavu Alawi Haji. Wagombea wenza w ni Eveline Wilbard Munis- NCCR, Husna Mohamed Abdallah-CUF, Aziza Haji Selemani-MAKINI, Amani Selemani Mzee-TLP, Chausiku Khatibu Mohamed-NLD, Sakia Mussa Debwa-SAU, Chuma Juma Abdallah na Devotha Minja- CHAUMA.
“TAMWA inatambua na kuthamini ujasiri na kujituma kwa wanawake wote waliojitokeza au kujaribu kugombea nafasi hizi, licha ya changamoto mbalimbali zinazowakabili” TAMWA
