Rais Samia Suluhu Hassan akiwa katika moja ya mikutano ya kampeni
Alipoingia madarakani Machi 2021, Rais Samia Suluhu Hassan alifanya mageuzi makubwa kisiasa tofauti na mtangulizi wake, Hayati Rais John Magufuli, ikiwa pamoja na kufanya maridhiano na makundi mbalimbali vikiwamo vyama vya siasa.
Wakati wa Hayati Magufuli, mikutano ya hadhara na maandamano kwa vyama vya siasa vilizuiwa, vyama hivyo viliminywa kiasi cha kushindwa kufanya kazi zake.
Samia alipoingia madarakani, aliruhusu mikutano na maandamano, aliunda kikosi kazi chini ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kilichowaleta pamoja wadau wa vyama hivyo kujadili changamoto hizo na miwsho kutokana na ripoti.
Japo CHADEMA walisusia kikosi hicho, Samia aliruhusu kukutana na wajumbe wa CCM pembeni ilikusikiliza malalamiko yao. Japo mazungumzo hayo baadaye yalivunjika lakini nia ya kuzungumza nao ilikuwepo.
Samia pia alionyesha dalili za kurejeshwa kwa mchakato wa mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, lakini ukayeyuka.
Vyombo vya habari navyo vilipata unafuu kwa kufunguliwa vilivyokuwa vimefungiwa.
Kwa ujumla, Rais Samia alitangaza falsafa ya Falsafa hii inajikita katika masuala ya Maridhiano (Reconciliation), Ustahamilivu (Resilience), Mageuzi (Reforms), na Kujenga upya Taifa (Rebuilding).
Hata hivyo, hiyo ilikuwa ni fungate tu, kwani baada ya mwaka mmoja wa kuwa madarakani, mambo yakaanza kubadilika. Ule uhuru uliokuwepo ukaanza kuyeyuka na kufubaa.
Uhasama wa vyama vya siasa ukarejea, mikutano na maandamano ikaanza tena kuwa na masharti mengi.
Wakati huo ripoti ya kikosi kazi ilipotoka, suala la mchakato wa mabadiliko ya Katiba ikasogezwa mbele hadi mwaka 2026, huku pia mazungumzo kati ya CCM na CHADEMA ndio yakafa, kila upande iukawa unarusha lawama kwa mwenzake.
Mbali na siasa, tukaanza kushuhudia kuzorota kwa hali ya usalama, taarifa za watu kutekwa na kupotea zikaanza kuvuma, huku taarifa nyingine zikihusisha vyombo vya Dola.
Miongoni mwa watu waliotekwa ni pamoja na makada wa CHADEMA, wakiwamo Ally Kibao, Deus Soka, Mdude Nyagali na wengineo. Wamo pia baadhi ya makada wa ACT Wazalendo akiwamo Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana, Abdul Nondo lakini alipatikana na pia wamo pia makada wa CCM.
Wengine waliotekwa ni pamoja na mwanaharakati wa mitandaoni, Edgar Mwakabela aliyepona chupuchupu kuuawa baada ya kutupwa katika hifadhi ya Katavi na Shedrack Chaula aliyetekwa baada ya kuachiliwa huru gerezani.
Licha ya Rais Samia kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuchunguza matukio hiyo, lakini hakuna taarifa rasmi inayoonyesha waliotekwa wameishia wapi. Hata hivyo, ahadi nyingi anazotoa sasa ni za mambo yale yale aliyoanza kuyafanyia kazi alipoingia madarakani mwaka 2021 kana kwamba hakuwahi kushika wadhifa huo.
Kampeni mpya za uchaguzi
Wakati kampeni za uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 zikiwa zimeanza, Rais Samia ambaye ndiye mgombea wa CCM ameanza kutangaza ahadi zake, ikiwemo ile ya kuleta maridhiano.
Tume ya maridhiano
Akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni za chama chake uliofanyika Agosti 28, 2025 kwenye viwanja vya Tanganyika Packers jijini Dar es Salaam, Samia alisema “tukiongozwa na faslafa ya 4R tutaendeleza mashauriano na wadau wa siasa, taasisi za kiraia na sekta binafsi kwa kuunda tume ya kuanzisha mazungumzo ya maridhiano na upatanishi ili kuandaa mazingira ya kuanza mchakato wa Katiba Mpya.”
Kauli hii inazua maswali, kwamba: maridhiano kwa mgogoro aliouleta nani? Je, yale maridhiano aliyoingia nayo miaka mine iliyopita kupitia falsafa ya 4R yameishia wapi? Kwamba Samia ametumia miaka minne kukorofisana na watu na sasa anataka kuunda tume ya upatanisho na maridhiano?
Iwe iwavyo, kwa kauli hiyo ina maanisha kwamba Rais Samia na CCM wanakubali kuwa wamewakorofisha Watanzania, hivyo wanataka kuunda tume ya upatanisho na maridhiano.
Yaani Watanzania sasa wameshakuwa kama kichwa cha mwendawazimu, kwamba unaweza kukitimuatimua, ukajifunzia urais kwa miaka minne, halafu sasa ukifuzu ndio unaomba rasmi kuwa rais?
Lakini kwa nini hiyo tume iundwe baada ya uchaguzi? Inawezekana anahofia kwamba akiunda sasa hivi, inaweza kuhatarusha mbio zake za kurudi ikulu. Kwa hiyo ikulu ni bora kuliko hayo maridhiano na upatanisho.
Mchakato wa Katiba mpya
Kuhusu ahadi ya Katiba mpya iliyopo pia kwenye ilani ya CCM, imeshapigwa danadana sana. Inaonyesha ni kikwazo kwa CCM kuendelea kuwa madarakani, lakini ili kuonyesha Samia amefanya kitu,huenda ikatekelezwa kimtego mtego, ila rais atakayekuja baadaye kupitia CCM, naye aendelee kupambana na suala hilo.
Kama Rais Samia angekuwa na nia ya kupatikana kwa katiba mpya, angeendeleza mchakato uliokuwepo tangu mwaka 2012 ukakwama mwaka 2025 katika kipengele cha kura ya maoni.
Huduma za afya
Ahadi nyingine ni kuzindua awamu ya majaribio ya mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, ikiwalenga awali wazee, watoto, wajawazito, na watu wenye ulemavu, huku gharama za matibabu zikifadhiliwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
Samia alisema Serikali itagharamia kikamilifu matibabu na vipimo vya uchunguzi kwa wananchi wasioweza kumudu matibabu ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza, ikiwa ni pamoja na saratani, figo, moyo, kisukari, mifupa, na magonjwa ya neva.
Hii nayo sio ahadi mpya kwa Samia. Tangu ameingia madarakani, Serikali imekuwa ikiahirisha mara kwa mara ahadi ya kupatikana kwa Bima ya Afya kwa wote.
Tulichotarajia kusikia ni utekelezwaji wake baada ya kupitishwa kuwa sharia.
Ahadi ya kutolipia maiti hospitali nayo sio kitu kipya, kwani Serikali kupitia iliyokuwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ilishatoa mwongozo wa suala hilo.
Katika waraka uliotolewa Oktoba 4, 2021na aliyekuwa Katibu wa Afya katika wizara hiyo, Profesa Abel Makubi ulikataza hospiali kuzuia maiti.
Leo Samia anakuja kuahidi kitu hicho hicho, kwani hakujua kamba kuna mwongozo?
Ahadi ya kuajiri wafanyakazi 5,000 wapya wa afya, ikiwemo wauguzi na wauguzi wa mama, ndani ya siku 100 nayo siyo kitu kipya.
Akiwasilisha bungeni hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka wa fedha 2025/26 alisema Waziri wa Afya, Jenista Mhagama alisema Julai 2024 hadi Machi 2025, Serikali imeajiri watumishi 13,564 katika sekta ya afya na kufanya jumla yao kufikia 177,711.
Ongezeko hilo alisema limepunguza upungufu wa watumishi wa sekta ya afya kutoka asilimia 64 hadi kufikia asilimia 55 ya mahitaji ya watumishi wote 391,950 wanaohitajika katika sekta hiyo.
Hizo ajira 5,000 ni za kawaida tu na wala hazizibi pengo la upungufu mkubwa uliopo.
Ununuzi wa matrekta milioni 10
Akizungumza Agosti 31, 2025, mbele ya maelfu ya wananchi wilayani Chemba Mkoa wa Dodoma, Samia aliahidi mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo kwa kuhakikisha serikali inanunua matrekta milioni 10 pamoja na zana nyingine za kisasa ndani ya kipindi cha miaka mitano.
Alisema mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi, wenye lengo la kumrahisishia mkulima upatikanaji wa huduma bora za kilimo na kuongeza tija katika uzalishaji.
Alisema serikali itahakikisha wakulima wanalimiwa kwa gharama nafuu zaidi kuliko sekta binafsi. “Kwa ekari moja, baadhi ya watu binafsi wanatoza hadi shilingi 80,000, na baada ya serikali kuanzisha vituo vya zana gharama zimeanza kushuka hadi shilingi 40,000. Lakini kwa bei yoyote sekta binafsi itakayowatoza wakulima, serikali itatoza nusu ya bei hiyo,” amesisitiza.
Hata hivyo, hoja ya kununua matrekta milioni 10, imeibua mjadala, ikielezwa kuwa idadi hiyo ni kubwa mno. Wakati ahadi hiyo ikitolewa, Ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2025 hadi 2030 imeahidi kutoa matrekta 10,000 kwa mkopo kwa wakulima.
Kwa mujibu wa mtandao wa Indexbox, uzalishaji wa dunia uliongezeka kwa haraka sana mwaka 2023 – kiasi hicho kiliongezeka kwa takriban 13 % ikilinganishwa na mwaka 2022
Mwaka 2021 ndiyo ulikuwa kilele cha uzalishaji, ulifikia kiasi cha takriban 5.1 milioni za matrekta
2013–2024, uzalishaji umeongeza kwa wastani wa takriban asilimia 2.0 kila mwaka. Baada ya kilele cha 2021, uzalishaji uliendelea kushuka kidogo kwenye miaka ya 2022–2024.
Kwa takwimu hizo, bado haijajulikana Samia atatoa wapi matrekta milioni 10.
Isitoshe, gharama ya kununua milioni 10 kwa bei wastani $30,000 (sawa na Sh75, milioni) ingefikia $300 bilioni (zaidi ya Sh750.7 trilioni), zaidi ya GDP ya Tanzania inayokadiriwa kufikia $89 bilioni (zaidi ya Sh222.7 trilioni).
Pengine huu ungekuwa wakati wa Rais Samia kutangaza mafanikio aliyoyapata kwa miaka minne ya kuwa madarakani na Watanzania wangeonyesha mapenzi ya kweli kwake.
