Florence Majani, Wino Tanzania
Wizara ya Afya imetoa tahadhari ya uwepo wa magonjwa ya mfumo wa upumuaji na homa ya dengue nchini.
Hayo yameelezwa leo katika taarifa iliyotolewa na kusainiwa na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe
Katika taarifa hiyo imeelezwa kuwa, tangu Februari mwaka huu hadi Aprili, kumekuwa na visa vya UVIKO-19 kutoka asilimia 1.4 sawa na wagonjwa wawili kati ya watu 139 waliopimwa hadi asilimia 16.3 mwezi Februari ambako walibainika wagonjwa 31 kati ya 190 waliopimwa.
Kati ya mwezi Machi hadi Aprili, kulikuwapo na wagonjwa 31 kati ya watu 185 waliopimwa sawa na asilimia 16.8.

“Hali ya kuongezeka na kupungua kwa ugonjwa huu imekuwapo tangu kutangazwa kwa ugonjwa huo mwaka 2020, na katika kipindi hiki ongezeko hilo linaonekana zaidi katika mkoa wa Dar es Salaam” imesema taarifa ya Dk Magembe
Pamoja na Uviko-19, kadhalika Wizara imesema kumekuwapo na ongezeko la magonjwa yanayoenezwa na mbu kutokana na mvua zinazoendelea nchini, na hilo limechagiza uwepo wa malaria na homa ya dengue.
Wizara imeitaka jamii, kufanya yafuatayo:
- Kuangamiza mazalia ya mbu kwa kuondoa maji yaliyotuama karibu na makazi
- Kutumia vyandarua vyenye dawa
- Kuvaa nguo ndefu zinazofunika mwili hasa wakati wa jioni na alfajiri
- Kufunga madirisha na milango au kutumia wavu ili kuzuia mbu kuingia ndani ya nyumba
