
Machi 29, 2025, Mohammed Dewji, maarufu kama MO, mfanyabiashara wa Kitanzania, alitajwa kwa mara nyingine na jarida la Forbes, kuwa tajiri namba 12 Afrika na namba moja Afrika Mashariki kwa mwaka 2025.
MO anashika nafasi ya 12 katika orodha ya mabilionea wa Afrika ya 2025, akiwa na utajiri wa Dola za Marekani Bilioni 2.2, akiongezeka kwa Dola za Marekani milioni 400 kutoka mwaka jana.
Ukiachana na utajiri huo, Mo akiwa ni mkurugenzi mtendaji wa Mohamed Enterprises Tanzania Limited (METL), ameajiri maelfu ya Watanzania, akiwa mmoja wa waajiri wakubwa nchini, na kupitia kampuni yake amewasaidia wengi kupata ajira na fursa za kiuchumi.
Mo Dewji, ameweka alama kubwa katika jamii ya Watanzania kupitia michango yake mbalimbali. Anaendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa kubadilisha maisha ya watu kwa kuwawezesha vijana na familia za Watanzania kupitia miradi mbalimbali ya kijamii na biashara.
Ameboresha sekta za kilimo na biashara, hasa kwa kufufua mashamba ya mkonge yaliyotelekezwa na kuanzisha biashara ya vinywaji ya Mo Cola, ambayo imeleta mabadiliko katika sekta ya vinywaji nchini Tanzania. Kwa kuanzisha na kuwekeza katika biashara hizi, ameunda ajira nyingi, na kupitia mpango wake wa kuongeza ajira, anatarajia kuajiri watu 100,000, hivyo kutoa mchango mkubwa katika kupambana na umaskini nchini.
Mohammed Dewji pia anajulikana kwa michango yake katika sekta ya huduma za kijamii na misaada. Kwa kupitia taasisi yake, Mohamed Dewji Foundation (MDF), ameleta mabadiliko makubwa katika upatikanaji wa maji safi na salama kwa Watanzania wengi, hasa vijijini.
Pamoja na Wizara ya Maji, MDF imechimba visima vingi, na kutatua changamoto kubwa za upatikanaji wa maji kwa zaidi ya watu 11,350. Aidha, taasisi hii imejikita katika utoaji wa huduma za afya, ikifanya kambi za matibabu ya macho na kusaidia watu wengi kurejesha uwezo wao wa kuona, hivyo kuboresha maisha yao.
Katika medani za michezo, Dewji ameleta mapinduzi katika timu ya soka ya Simba, akiboresha miundombinu ya timu hiyo na kuifanya kuwa moja ya timu bora barani Afrika. Amewezesha wachezaji kupata mishahara bora na ametunga mikakati ya maendeleo ya wachezaji. Mo Dewji pia ana mipango ya kuhamasisha vijana na jamii kupitia michezo, akichukua hatua za kuhamasisha ushiriki wa kizazi kipya katika michezo na kufanya soka kuwa jukwaa la maendeleo ya kijamii.
Pia, MO alijiunga na The Giving Pledge mwaka 2016, na ameahidi kutoa angalau nusu ya mali yake kwa madhumuni ya hisani, akionyesha dhamira yake ya kusaidia jamii na kuthamini imani ya hisani aliyojifunza kutoka kwa wazazi wake.
Kwa ujumla, kupitia shughuli zake za biashara, misaada ya kijamii, michezo, na uwekezaji, MO amekuwa mchezaji muhimu katika kuboresha maisha ya Watanzania na kubadilisha jamii kwa ujumla.
Orodha ya Forbes
Katika orodha hiyo mpya ya 2025 iliyotolewa na Forbes Machi 29, 2025, MO anashika nafasi ya 12, akiwa utajiri wenye thamani halisi ya mali ya Dola za Marekani Bilioni 2.2 akipanda kwa Dola za Marekani 400 million ikilinganishwa na Dola za Marekani Bilioni 1.8 mwaka jana.

Katika orodha hiyo, raia wa Afrika Kusini, Johann Rupert, anakamata nafasi ya pili akiwa na utajiri wa Dola za Marekani Bilioni 14, sawa na ongezeko la asilimia 39.
Anafuatiwa na mfanyabiashara wa Afrika Kusini, Nicky Oppenheimer na familia yake, wanaokamata nafasi ya tatu kwa Dola za Marekani Bilioni 10.4.
Orodha ya mabilionea wengine wa Africa na thamani ya utajiri wao kwenye mabano ni: Nassef Sawiris kutoka Misri ($9.6 bilioni), Mike Adenuga kutoka Nigeria ($6.8 bilioni), Abdulsamad Rabiu wa Nigeria ($5.1 bilioni), Naguib Sawiris kutoka Misri ($5 bilioni), na Koos Bekker kutoka Afrika Kusini ($3.4 bilioni).
Pia wamo Mohamed Mansour kutoka Misri ($3.4 bilioni), Patrice Motsepe wa Afrika Kusini na Rais wa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) ($3 bilioni), Issaad Rebrab kutoka Algeria na familia yake ($3 bilioni), Mohamed Dewji wa Tanzania ($2.2 bilioni), Michael Le Roux wa Afrika Kusini ($2.2 bilioni), na Othman Benjelloun na familia yake kutoka Morocco ($1.6 bilioni).