
Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche, leo Septemba 14, 2026 amekabiliwa na maswali makali kutoka kwa mawakili wa Serikali na upande wa mashtaka katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu.
Heche, ambaye ni shahidi wa tano wa upande wa utetezi, aliendelea kuhojiwa katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, akitoa majibu kuhusu uchaguzi, madai ya mauaji, utekaji, ripoti za waangalizi wa uchaguzi na matukio ya Oktoba 29, 2025.
Katika hatua ya awali, Wakili wa Serikali Mkuu Ignas Mwinuka alimuuliza Heche kuhusu uzoefu wake katika uchaguzi, ambapo alisema amewahi kushiriki chaguzi tatu zilizosimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), na katika chaguzi mbili alitangazwa mshindi.
Heche alisema hakuwahi kuwasilisha kesi kupinga matokeo ya uchaguzi wa 2020, huku akikubali kuwa kujaza fomu ni mojawapo ya vigezo vya kugombea nafasi ya ubunge.
Shambulio la Lissu
Katika sehemu nyingine, Mwinuka alimuuliza Heche kuhusu shambulio la Lissu la Septemba 7, 2017, akitaka kujua kama anakumbuka kauli za viongozi mbalimbali akiwamo Rais wa wakati huo, John Magufuli, Katibu Mkuu wa CCM wa wakati huo, Humphrey Polepole na Spika wa Bunge.
Heche alisema hakumbuki kauli za Magufuli na Polepole, lakini alikumbuka taarifa iliyotolewa na Spika pamoja na ziara ya aliyekuwa Makamu wa Rais kumtembelea Lissu wakati akipatiwa matibabu Nairobi.
Alipoulizwa kuhusu tukio lenyewe, Heche alisema hakuwa eneo la tukio na kwamba baadhi ya maelezo aliyotoa kuhusu kilichotokea aliyapata kutoka kwa Lissu mwenyewe.
Mauaji na utekaji
Mwinuka pia alimuuliza Heche kuhusu orodha ya watu aliowataja katika ushahidi wake kuwa waliuawa, akitaka kujua kama alishuhudia mauaji hayo kwa macho yake.
Heche alisema hakumbuki idadi ya mauaji aliyoshuhudia na alikiri kwamba katika baadhi ya matukio aliyoyataja, ikiwamo la Arumeru na tukio alilomhusisha Ezekiel Wenje, hakuwa eneo la tukio.
Alipoulizwa kuhusu chanzo cha vifo kwa mujibu wa taarifa za kitabibu, Heche alisema hakueleza taarifa hizo za kitabibu.
Aidha, alikiri kuwa hajawahi kushuhudia mtu akitekwa kwa macho yake wala mtu yeyote kati ya aliowataja akipotea.
Kuhusu Tume ya Rais iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Mstaafu Joseph Chande kuchunguza matukio ya Oktoba 29, Heche alisema msimamo wa Chadema ulikuwa kutoamini tume hiyo kwa sababu, kwa mtazamo wa chama, iliundwa katika mazingira ya kuficha ukweli kuhusu waliohusika. Alisema kwa sababu hiyo chama hakikutoa ushirikiano kwa tume hiyo.
Ripoti za uchaguzi
Mwinuka alimuuliza Heche kuhusu ripoti mbalimbali za uchaguzi wa mwaka 2025, ambapo shahidi alisema baadhi ya taarifa alizipata kupitia vyombo vya habari.
Heche alitaja ripoti za taasisi na mashirika mbalimbali za kikanda na kimataifa, akisema nyingi ziliandikwa kwa Kiingereza na yeye alizieleza kwa Kiswahili mahakamani.
Mwinuka alitaka kujua kama Heche ana utaalamu wa kutafsiri kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili na kama alieleza mahakamani uwezo wake wa kufanya hivyo.
Heche alisema hakueleza suala hilo.
Maswali kuhusu maisha binafsi na fedha
Baada ya Mwinuka kumaliza, Wakili wa Serikali Mkuu Nassor Katuga aliendelea kumuuliza Heche maswali kuhusu elimu yake, mali na shughuli zake za kipato.
Heche alisema ana shahada ya Bachelor of Arts with Education na kwamba ni mwalimu. Alikanusha kuwa na malori yanayofanya kazi Kenya na pia akakanusha kuwa na magari manne, ingawa alisema anamiliki magari mawili.
Wakati wakili akimuuliza kuhusu magari hayo, Heche alitaja kuwa moja ya Prado ilikuwa na thamani ya Sh80 milioni, trekta Sh80 milioni na Mitsubishi Sh60 milioni.
Alisema hakulipwi mshahara wala posho kwa nafasi yake ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema.
Madai kuhusu mauaji ya mdogo wake
Katuga pia alimuuliza Heche kuhusu kifo cha mdogo wake, Suguta, ambaye alisema aliuawa na polisi.
Heche alikiri kuwa hakuwepo wakati mdogo wake alipokamatwa wala wakati alipochomwa kwa singe, akisema baadhi ya taarifa hizo alipewa na RPC.
Alipoulizwa kama polisi huyo aliyedaiwa kumuua mdogo wake alieleza kuwa alifanya hivyo kwa lengo la kumzuia Heche katika shughuli za kisiasa, Heche alisema polisi huyo hakusema hivyo.
Hata hivyo, Heche alisema anaamini mdogo wake aliuawa kwa sababu waliotenda kitendo hicho walitaka kumkomoa yeye na kumtisha ili aache siasa.
Akaunti na michango
Katika hatua nyingine, Katuga alimuuliza Heche kuhusu akaunti ya benki yenye namba 0152220057400, ambayo shahidi alikubali kuwa ni yake.
Heche pia alikubali akaunti hiyo ilipokea fedha kutoka kwa mtu aliyemtaja kama Salma, lakini akasema hamfahamu mtu huyo.
‘No Reforms, No Election’
Katuga aliuliza pia kauli ya Chadema ya “No Reforms, No Election”, akimkabili Heche na ushahidi wa Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chadema, Brenda Rupia.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa mahakamani, Rupia alisema kauli hiyo ililenga kuzuia uchaguzi, huku Heche katika ushahidi wake wa awali akieleza kuwa ilikuwa ikimaanisha kutaka mabadiliko.
Heche alisema mitazamo hiyo miwili haifanani.
Baadaye Katuga alimuuliza kama kauli “Hakuna Mabadiliko, Hakuna Uchaguzi” ilikuwa na maana ya kwenda kuzuia uchaguzi au kuhamasisha uasi.
Heche alisema kauli hiyo yenyewe haina maneno ya kusema wanaenda kuzuia uchaguzi, huku kuhusu suala la kuhamasisha uasi akisema maana yake inategemea mtu anavyoielewa.
Matukio ya Oktoba 29
Katika sehemu nyingine ya mahojiano, Katuga alimuuliza Heche kuhusu madai ya kuhusika katika kupanga na kuratibu matukio ya Oktoba 29, 2025.
Heche alisema hajui kama ushahidi uliokusanywa unaonyesha kuwa yeye au viongozi wengine wa Chadema walihusika katika kupanga matukio hayo.
Alikiri pia kuwa alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo wakati wa kuhojiwa, alikataa kutoa maelezo, akisema kufanya hivyo ilikuwa ni haki yake.
Heche alisema pia alisikia hotuba ya Jaji Chande iliyosema matukio ya Oktoba 29 yalipangwa na kuratibiwa, lakini alipoulizwa kama hilo linaendana na ushahidi unaodai yeye alihusika katika mipango hiyo, alisema hajui.
Wenje na Kenya
Katuga alimuuliza pia Heche kuhusu taarifa kwamba aliyekuwa Mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje, alinusurika kuuawa na baadaye kwenda Kenya.
Heche alisema hakuwapo wakati tukio hilo lilipotokea na kwamba taarifa hiyo aliipata kutoka kwa Wenje mwenyewe alipofika Tarime.
Passport na safari ya Kenya
Heche pia alikiri kuwa aliwahi kutaka kwenda Kenya lakini hakuvuka mpaka.
Alisema alikamatwa kwa tuhuma za kutaka kwenda Kenya, na baadaye alisafirishwa hadi Dodoma ambako aliwekwa katika selo ya peke yake.
Alisema passport yake ilichukuliwa Oktoba 18, 2025 na baadaye kurejeshwa baada ya chama kuandika barua kupitia Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Dk Rugemeleza Nshala.
Ripoti ya SADC
Katika sehemu nyingine, Katuga alimhoji Heche kuhusu ripoti ya waangalizi wa uchaguzi ya SADC ambayo shahidi aliitumia katika ushahidi wake.
Heche alikubali kuwa ripoti hiyo iliandikwa kwa Kiingereza na kwamba aliieleza mahakamani kwa Kiswahili.
Wakati sehemu ya ripoti ikisomwa mahakamani, Heche alisema taarifa hiyo ilizungumzia matumizi ya nguvu na vitendo vya utekaji kabla na baada ya uchaguzi.
Hata hivyo, alieleza kuwa ripoti hiyo pia ilizungumzia kwa ujumla masuala ya demokrasia, akisema utekaji ni kinyume na demokrasia.
Muda wa shahidi kuhojiwa waisha
Mahojiano hayo yalifikia kikomo baada ya Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, kusimama na kueleza kuwa shahidi alikuwa amechoka na muda wa mahakama ulikuwa umeisha.
Jaji alimuuliza Heche kama amechoka, huku Lissu akisema si shahidi pekee aliyechoka.
Heche naye alikubaliana kwamba amechoka na kusema kama muda ulikuwa umeisha, yuko tayari kuendelea wakati mwingine.
