Heche Atoa Ushuhuda Kuhusu Mauaji, Utekaji Na Kesi Za Viongozi Wa Chadema
Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche, ameendelea kutoa ushahidi katika shauri la uhaini linalomkabili Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, akieleza kuhusu matukio ya mauaji, utekaji, kukamatwa kwa viongozi na wanachama wa chama hicho pamoja na kesi mbalimbali za kisiasa.
Heche alitoa ushahidi huo jana, Septemba 10, 2026, baada ya kuulizwa maswali na Lissu kuhusu matukio aliyodai kuwa yamekuwa yakitokea wakati wa chaguzi na katika vipindi tofauti vya kisiasa.
Akieleza kuhusu mauaji yaliyotokea wakati wa chaguzi, Heche alisema yapo matukio yaliyowahusisha viongozi na wanachama wa Chadema, huku akitaja pia wananchi wengine waliopoteza maisha.
Alitaja maeneo ya Tunduma na Shinyanga, pamoja na matukio ya Zanzibar yaliyotokea wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000.
Heche pia alizungumzia matukio ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana, akidai kuwa kulikuwa na mauaji makubwa katika maeneo mbalimbali nchini, yakiwemo Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Arusha, Tarime na Geita.
Watu 718 waliotekwa, kupotea
Katika sehemu nyingine ya ushahidi, Lissu alimuuliza Heche kuhusu madai ya utekaji na kupotezwa kwa viongozi na wanachama wa Chadema pamoja na watu wengine.
Heche alisema matukio ya uonevu ni mengi, akirejea ripoti aliyodai kuwa ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), ambayo alisema ilieleza kuhusu watu 718 waliotekwa na kupotezwa katika vipindi mbalimbali.
Alipoulizwa ripoti hiyo ni ya mwaka gani, Heche alisema ni ya mwaka 2026 na kwamba matukio yaliyomo yanahusu vipindi tofauti.
Lissu alimtaka aanze na matukio ya mwaka 2016 na 2017, ambapo Heche alitaja kutoweka kwa Ben Saanane, aliyekuwa msaidizi wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
Pia alimtaja mwandishi wa Mwananchi, Azory Gwanda, pamoja na Simon Kanguye, aliyekuwa mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya mkoani Kigoma.
Heche alisema watu hao bado hawajapatikana.
Aliendelea kutaja matukio mengine ya watu waliodaiwa kutekwa au kupotea, akiwemo aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Rwanda, Humphrey Polepole, Mdude Nyagali, aliyekuwa akiishi Mbeya, na aliyekuwa Mwenyekiti wa BAVICHA Temeke, Deusdedith Soka, pamoja na wenzake wawili waliodaiwa kutekwa miaka miwili iliyopita.
Kesi ya Mbowe
Heche pia alieleza kuhusu kesi iliyomkabili Mbowe mwaka 2021, akisema ilihusisha tuhuma za ugaidi na kupanga njama za kuwaua viongozi.
Alisema Mbowe alikaa gerezani kwa takribani miezi minane kabla ya kuachiwa.
Baadaye, alisema walimuona Mbowe katika picha akiwa Ikulu pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan.
Heche alisema wakati Mbowe alipokamatwa Mwanza, yeye pia alikamatwa pamoja na viongozi wengine na baadhi ya viongozi wa dini.
Alisema walishikiliwa katika vituo mbalimbali vya polisi Mwanza, huku yeye akikaa kwa siku tano katika Kituo Kikuu cha Polisi Mwanza.
Heche alipokamatwa nje ya Mahakama
Heche aliieleza pia mahakama kuhusu kukamatwa kwake Oktoba 22, 2025, nje ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, alipokwenda kuhudhuria shauri hilo.
Alisema aliambiwa amevuka mpaka kwenda Kenya bila kufuata taratibu za uhamiaji na angepelekwa Tarime, lakini njiani alifikishwa Dodoma na kuwekwa Kituo cha Polisi Mtumba.
Heche alisema alikaa kituoni hapo hadi Novemba 4, 2025, kabla ya kurejeshwa Dar es Salaam.
Alidai akiwa kituoni familia yake haikujulishwa alipo hadi alipoanza kugoma kula na kunywa kwa siku tatu, ndipo ndugu yake aliporuhusiwa kumuona.
Baada ya kurejeshwa Dar es Salaam, alisema alipelekwa Kituo cha Polisi Oysterbay, ambako alikutana na watu wengine waliokuwa wamekamatwa kwa sababu alizodai zilihusiana na uchaguzi.
Alisema baadaye alisomewa tuhuma za ugaidi, zikiwemo madai ya kupanga kuchoma vituo vya mabasi yaendayo kwa kasi, lakini tuhuma hizo hazikuendelea.
Heche alisema baadaye alipelekwa Mburahati na kukaa huko hadi Novemba 10, kabla ya kurejeshwa tena Oysterbay.
Akiwa Oysterbay, alisema alikutana na viongozi wengine wa Chadema waliokamatwa, akiwemo Naibu Katibu Mkuu Amani Golugwa, Godbless Lema na Boniface Jacob.
Alisema baadaye walipewa dhamana na kuendelea na majukumu yao.
Alipoulizwa kama anamfahamu kiongozi wa Chadema ambaye hajawahi kukamatwa, Heche alisema hana kumbukumbu ya kiongozi wa chama hicho ambaye hajawahi kukamatwa.
Kesi za Lissu
Kuhusu Lissu, Heche alisema shauri la sasa siyo kesi pekee anayomfahamu.
Alitaja kukamatwa kwa Lissu Tarime baada ya kutokea kwa mauaji katika eneo la mgodi wa Nyamongo, akisema Lissu alifika eneo hilo kama mtetezi wa wananchi waliokuwa kwenye mgogoro.
Heche alisema wakati huo Lissu alikuwa mbunge na Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu wa Chadema.
Alisema kesi hiyo ya uchochezi haikuendelea, kama ilivyokuwa kwa baadhi ya kesi nyingine alizozitaja.
Lissu alipouliza kama amewahi kuona akitiwa hatiani katika kesi hizo, Heche alisema hajawahi kuona akitiwa hatiani.
Lissu pia aliuliza kuhusu kinga dhidi ya kukamatwa kwa viongozi au wanachama wa Chadema, ambapo Heche alisema kwa ufahamu wake hakuna kinga hiyo.
Alipoulizwa kama anafahamu chama kingine ambacho viongozi na wanachama wake wamekuwa wakikamatwa na kufunguliwa kesi ambazo baadaye zinaishia bila kuendelea, Heche alisema hana kumbukumbu ya chama kingine.
Kwa mtazamo wake, alisema lengo la kukamatwa, kutekwa na kupotezwa kwa viongozi na wanachama wa Chadema pamoja na kufunguliwa kesi ambazo baadaye zinaishia bila kuendelea ni kuwatisha viongozi wengine, kuwakatisha tamaa na kuwarudisha nyuma katika shughuli za chama.
Alisema pia kwa ufahamu wake vitendo hivyo havina uhalali wa kikatiba wala kisheria.
Lissu Apigwa Risasi
Ushahidi wa Heche uliingia pia kwenye tukio la kushambuliwa kwa risasi kwa Lissu Septemba 7, 2017, jijini Dodoma.
Heche alisema siku hiyo alikuwa Bungeni pamoja na Lissu kabla ya Lissu kwenda nyumbani kwake mchana.
Alisema Lissu alikuwa akifuatiliwa na gari hadi nyumbani kwake, ambako baadaye alishambuliwa kwa risasi na kujeruhiwa vibaya.
Heche alidai eneo hilo lilikuwa likikaliwa pia na viongozi wengine na kulikuwa na askari, lakini washambuliaji waliondoka bila mtu kushtakiwa.
Baada ya tukio hilo, alisema Lissu alisafirishwa Nairobi kwa matibabu.
Heche alisema gharama za matibabu Nairobi na baadaye Ubelgiji zilitolewa na Chadema pamoja na TLS, wakati Lissu akiwa Rais wa chama hicho.
Alisema baadaye Lissu alivuliwa ubunge kwa sababu zilizotajwa kuwa alikuwa mtoro, wakati akiwa nje ya nchi kwa matibabu.
Pia alithibitisha kuwa Samia, aliyekuwa Makamu wa Rais wakati huo, alimtembelea Lissu alipokuwa akipatiwa matibabu Nairobi.
“No Reforms, No Election”
Katika sehemu nyingine, Lissu alimuuliza Heche kuhusu mageuzi ambayo Chadema ilitaka yafanyike ili kushiriki uchaguzi.
Heche alisema chama kilitaka mabadiliko ya Katiba na sheria zinazoongoza uchaguzi, pamoja na namna Tume ya Taifa ya Uchaguzi inavyoundwa, akitaja Ibara ya 74 ya Katiba.
Alisema walitaka Tume huru ambayo ingewapa wananchi haki na usawa katika masuala ya uchaguzi.
Kuhusu msimamo wa “No Reforms, No Election”, Heche alisema ulifuatia maazimio ya chama yaliyotangazwa hadharani na Mbowe baada ya kile alichodai kuwa ni matatizo yaliyojitokeza katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Alisema Baraza Kuu la Chadema lilipitisha msimamo huo katika kikao cha Januari 20, kabla ya kuupeleka kwenye Mkutano Mkuu.
Heche alisema Mkutano Mkuu uliunga mkono msimamo huo na kuelekeza Kamati Kuu kuandaa mpango wa kuwafikia wadau, wananchi na wanachama kwa ajili ya kuwaelimisha kuhusu msimamo huo.
Katika kikao hicho, Heche alisema pia ulifanyika uchaguzi wa viongozi wa chama, ambapo Lissu alichaguliwa kuwa Mwenyekiti, Said Mzee kuwa Makamu Mwenyekiti Zanzibar na yeye kuwa Makamu Mwenyekiti Bara.
Ushahidi wa Heche unaendelea katika hatua ya utetezi, huku mahakama ikiendelea kusikiliza maelezo yake kuhusu matukio mbalimbali anayodai yana uhusiano na mazingira ya kisiasa na msimamo wa Chadema kuelekea uchaguzi.
Maswali na majibu
Lissu: Waeleze majaji kwamba katika vikao na wadau, kiongozi wa msafara wa chadema alikuwa mimi na nilikuwa mzungumzaji mkuu. Ufafanue zaidi ujumbe wetu kinagaubaga. Kote huko tulikwenda, kwa wadau waeleze majaji mazungumzo yangu kuhusu suala la tume ya uchaguzi ya nchi hii kutawaliwa na rais.
Heche: Waheshimiwa majaji kote tulipopata, kama kwa viongozi wastaafu kama mzee warioba, ujumbe wetu ulioongozwa na mwenyekiti Tundu Lissu alieleza kwa kina namna ambavyo tume ya taifa ya uchaguzi inayoteuliwa na rais ambaye ni mwenyekiti wa ccm inavyovuruga uchaguzi, kuonea wapinzani hasa chadema, kufanya upendeleo wa wazi kwa wagombea wa ccm, kuvunja sheria za uchaguzi hata hizi zilizopo kwa uwazi.
Lissu: Waeleze waheshimiwa majaji, mazungumzo yangu kwamba sisi chadema hatuko tayari kuendelea kushiriki au kuruhusu chaguzi za namna hii. (Waeleze wadau nilichokuwa kuhusu kushiriki kwetu kwenye chaguzi hizo)
Heche: Kote tulikopita na wote tulikutana nao mwenyekiti Tundu Lissu aliweka msimamo kwa niaba ya chama chetu cha Demokrasia na Maendeleo kwamba hatuko tayari kushiriki tena chaguzi za namna hii, ambazo matokeo yake ni mauaji, kuengua wagombea.
Lissu: Waeleze majaji tulichowaeleza wadau hao juu ya kuhamasisha watanzania kupinga uchaguzi ujao.
Heche: Mwenyekiti aliwaeleza wadau wote na watu tulikutana nao kwamba kila mtu kwa nafasi yake, ashiriki kuhakikisha kwamba mfumo wa uchaguzi unabadilika. (Waheshimiwa majaji mwenyekiti Tundu Lissu aliwaeleza wadau kwamba msimamo wetu wa chama kuhusu no refoms no election tutazungumza na wananchi kwenye mikutano ya hadhara ili kuwaelimisha.
Lissu: Waeleze waheshimiwa majaji kama nilitumia maneno kuhusu kuhamasisha uasi kwa watanzania dhidi ya mfumo wetu wa uchaguzi.
Heche: Waheshimiwa majaji sina kumbukumbu sana kwenye hilo. (Haku sehemu aliyotumia neno uasi lakini maneno yaliyokuwa na maana ya kupinga mfumo mbovu wa uchaguzi.
Lissu: waeleze waheshimiwa majaji katika mazungumzo yangu, nilizungumzia kwamba tutahamasisha wananchi kuzuia uchaguzi.
Heche: Waheshimiwa majaji aliyezungumza hayo. (Ndiyo waheshimiwa majaji).
Lissu: kwa ufahamu wako, mimi kusema tutavuruga uchaguzi huu ili kuhakikisha haufanyiki.
Heche: Ndiyo waheshimiwa majaji alisema tutauvuruga.
Lissu: waeleze majaji kwa kumbukumbu zako, mimi kutumia neno tutakinukisha.
Heche: Sikumbuki mahala popote kama alitumia neno tutakinukisha.
Lissu: Katika mazungumzo na wadau, waeleze majaji kuhusu mimi kuzu gumzo matatizo ya utengenezaji wa majimbo ya uchaguzi nchi hii.
Heche: Nakumbuka mwenyekiti alizungumzia kutenganisha majimbo kwa upendeleo, viongozi kujigawia majimbo.
Lissu: Waeleze majaji katika mikutano na wadau kumbukumbuzako kuhusu mimi kuzungumzia matatizo ya uteuzi
Heche: Tundu Lissu alieleza namna wadau wetu walivyoenguliwa kwa wingi, akatolea mfano wa uchaguzi wa 2020 ambao ulivunja rekodi kwa wagombea udiwani kuenguliwa.
Lissu: Waeleze majaji nilisema nini juu ya yanayofanyika siku ya uchaguzi?
Heche: Alieleza kwa undani namna ambazo zoezi la siku yenyewe ya kupiga kura linavyovurugwa kwa wasimamizi kuenguliwa, matokeo ambayo siyo halali na wagombea ambao hawajashinda kutangazwa wameshinda/ambao hawakuchaguliwa na wananchi.
Lissu: waeleze majaji nilisema nini kwa wadau kuhusu utaratibu wa kupinga matokeo ya uchaguzi mahakamani?
Heche: Waheshimiwa majaji, alieleza namna ambavyo ni vigumu kupinga matokeo ya uchaguzi mahakamani, kwanza kama umeenguliwa, hiwezi kwenda mahakamani kupinga matokeo hayo.
Lissu: Waeleze nilisema nini juu ya kupinga matokeo ya Uchaguzi wa Rais Mahakamani?
Heche: Waheshimiwa majaji, Tundu Lissu alieleza kwamba nchi hii huwezi kupinga matokeo ya Rais kwenye mamlaka yoyote ya nchi hii.
Lissu: waeleze nilisema nini juu ya haki ya wananchi wasiokuwa wanachama kugombea uongozi?
Heche: Alieleza kwamba nchi hii mtu au mgombea huru hawezi kuruhusiwa kugombea akiwa huru, inalazimika mpaka awe kwenye chama cha siasa.
Lissu: Waeleze majaji nilisema nini juu ya harakati mbalimbali za kubadili mfumo huu wa uchaguzi.
Heche: Alieleza harakati za kubadili mfumo wa uchaguzi zimekuwa tangu miaka ya 1993 ambapo alieleza kwamba harakati hizo zimekuwa zikizuiwa na cha mapinduzi kwa sababu kimekuwa kikinufaika na mfumo uliopo, ikiwemo harakati za jaji Nyalali, Tume ya jaji kisanga, Tume ya Jaji Joseph Sinde Warioba ya hivi karibuni ambazo zote zina mapendekezo kuhusu kubadili mfumo wa uchaguzi, kuhusu uhuru wa kuruhusu mfumo wa demokrasia ufanye kazi na kuondoa huu mfumo wa chama kimoja, kuwapa wananchi uhuru wa kufanya uchaguzi waweze kuchagua nani awe kiongozi wao.
Lissu: Ukisema kuondoa mfumo wa chama kimoja una maana gani?
Heche: Mfumo uliopo kwa sasa ni ule ambao umhodhiwa na chama cha mapinduzi na viongozi wake, ambapo mgombea wa ccm ambaye ndiye anaamua nani awe mwenyekiti wa tume, nani awe makamu mwenyekiti wa tume, na wawe makamishna kwenye tume na wengine wote mpaka ngazi ya kata, na wengi wao kama siyo wote ni wanachama wa chama cha mapinduzi.
Lissu: elezea hicho ulichosema, juu ya mchungaji Christopher Mtikila kwenda mahakama ya Afrika.
Heche: Kwa uelewa wangu, kuna mikataba ya kimataifa ambayo tuna saini, kuna sheria pia ambazo zinatufunga kimataifa, pamoja na kesi ya askofu Mtikila kuna kesi ya Freeman Mbowe, (Akataja na kesi nyingine kuhusu wasimamizi wa uchaguzi ambao ni wana CCM).
Lissu: Waeleze majaji kwenye mazubgumzo yangu na wadau hilo nililizungumziaje kuhusu mahakama za nje au za kikanda?
Heche: Waheshimiwa majaji, alieleza kwamba kumekuwa na majaribio ya watu wengi kubadili mfumo wa uchaguzi kupitia mahakama na watawala wamekuwa wakipuuza maelekezo ya mahakama, ndiyo maana akasema mahakama hakuendeki.
Lissu: Waeleze majaji nilizungumza nini na wadau juu ya adha ya kuahirisha uchaguzi wa 2025?
Heche: Alisema kwa sababu ungaunga matatizo, unaleta mauaji na matokeo ambayo wananchi hawakutegea sisi tulikuwa tayari uchaguzi usogezwe mbele ili mabadiliko yafanyike ambayo yangeruhusu kufanyika uchaguzi hiru na haki, kuepusha maafa ambayo yanaweza kujitokeza kama kwenye chaguzi zilizopita.
Lissu: waeleze majaji, hizo jitihada za kuwashirikisha wadau wa nje unazozifahamu.
Heche: Nakumbuka tulisafiri mpaka Nairobi Kenya, mimi pamojana na Tundu Lissu na Godbless Lema.
Lissu: Waeleze majaji mkakati wa kuzungumza na wananchi ulikuwaje?
Heche: Ilikuwa ni kufanya mikutano ya hadhara.
Lissu: waeleze majaji katika ziara ya kanda mimi na wewe tulikuwa pamoja.
Heche: Ulikuwa ni kufanya mkutano pamoja Mbeya mjini na Iringa mjini
Lissu: Waeleze majaji huo mkutano wa Mbeya ulikuwa tarehe ngapi?
Heche: Sikumbuki tarehe ila ulikuwa mkutano wa kwanza.
Lissu: Waeleze Iringa je?
Heche: Sikumbuki tarehe lakini nakumbuka ulikuwa mkutano wa mwisho.
Lissu: Baada ya hapo Ratiba ilikuwaje? Wewe ulienda wapi na mimi nilienda wapi?
Heche: Mimi nilikwenda Njombe na baadhi ya maeneo ya Iringa na Tundu Lissu alikwenda Rukwa Sumbawanga, Tunduma na Songwe.
Lissu: Waeleze majaji kwenye hiyo mikutano tuliyokuwa pamoja, nilizungumza nini?
Heche: Kwa kiasi kikubwa ilijikita kwenye matatizo ya uchaguzi, historia ya uchaguzi wa nchi hii. (NI mambo yaleyale, hakuna tofauti yoyote ya hotuba ni yaleyale)
Lissu: Waeleze majaji kuhusu mkutano wa mwisho Iringa tofauti ya mkutano huo na mikutano mingine
Heche: Hakuna utofauti wowote kati hotuba hizo
Lissu: Mkutano wa tarehe 3 apili 2025, weleze majaji wewe ulipataje habari za huo mkutano?
Heche: Nilipigigiwa simu na Naibu katibu Mkuu Bara amani Golugwa.
About the Author
Wino Tanzania
Author
WINO Tanzania is a nonprofit, non-government, media organization registered on 11th August 2022 under non-Government Organizational Act of 2002, with Registration No. 00NGO/R/3681. WINO seeks to bridge the gaps in a media industry in Tanzania, by providing grants for Investigative Journalism, training and mentorship programs so as enable them to perform with greater professionalism and hence impact journalism
