
Katika hatua ya kuwajengea wafungwa msingi wa maisha bora baada ya kifungo, Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza nchini, kimezindua rasmi programu ya mafunzo ya ujasiriamali na stadi za biashara kwa wafungwa, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuwawezesha kiuchumi na kijamii.
Uzinduzi wa programu hiyo umefanyika leo Mei 6, 2025 katika Gereza Kuu la Arusha, ukiongozwa na Kamishna Jenerali wa Magereza, CGP Jeremiah Katungu, ambaye ameipongeza IAA kwa kuchangia juhudi za serikali katika kuboresha maisha ya wafungwa kupitia elimu na ujuzi.
“Tangu tuliposaini makubaliano na IAA mwezi Septemba 2024, tumeshuhudia kasi ya utekelezaji na matokeo chanya. Programu hii ni mwanzo mzuri, na tuna dhamira ya kuwafikia wafungwa wengi zaidi nchini,” amesema CGP Katungu. Ameongeza kuwa juhudi hizi ni sehemu ya kubadilisha maisha ya wafungwa, kwa kuwapatia nyenzo muhimu za kuwa raia wema, wanaochangia katika maendeleo ya taifa.
Pamoja na kutoa mafunzo kwa wafungwa, Katungu amebainisha kuwa zaidi ya maafisa na askari 100 wa magereza tayari wamedahiliwa IAA kwa shahada ya uzamili kwa mwaka wa masomo 2024/2025, ikiwa ni hatua ya kuwaongezea uwezo kitaaluma.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha IAA, Prof. Eliamani Sedoyeka, amesema dhamira ya chuo si tu kutoa elimu kwa walio huru, bali pia kuwafikia walioko katika mazingira magumu. “Haya ni mafunzo ya mwanzo tu. Lengo letu ni kuanzisha programu za muda mrefu kwa wafungwa, kuanzia ngazi ya cheti hadi shahada ya uzamili,” amesema Prof. Sedoyeka.

Ameongeza kuwa kozi hii ya ujasiriamali ni hatua ya kwanza katika mchakato huo, na IAA inakusudia kupanua mafunzo hayo kwa kuongeza kozi nyingine kama udereva, ili kuhakikisha wafungwa wanapomaliza vifungo vyao wanarudi katika jamii wakiwa na maarifa na stadi za maisha.
Akizungumza wakati wa uzinduzi, Mkuu wa Kitivo cha Utawala na Usalama wa IAA, Dkt. Adonijah Abayo, amesema mafunzo hayo yameanza na wafungwa 40 katika Gereza la Arusha na yatadumu kwa wiki mbili, kabla ya kusambaa katika magereza mengine nchini. “Tunaamini kuwa kupitia mafunzo haya, wafungwa wataweza kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi wa familia zao na taifa kwa ujumla,” amesema Dkt. Abayo.
Kwa wafungwa hao, programu hii si tu elimu – ni nafasi ya pili ya maisha, matumaini mapya ya kesho yenye heshima, ufanisi, na mchango chanya kwa jamii.